KABLA YA MAANGAMIZI, KRISTO HUWA ANAONYESHA KWANZA NJIA YA KUTOROKEA.

KABLA YA MAANGAMIZI, KRISTO HUWA ANAONYESHA KWANZA NJIA YA KUTOROKEA.

Luka 21:20 “Lakini, hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia.

21 Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie.

22 Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa.

23 Ole wao wenye mimba na wanaonyonyesha katika siku hizo! Kwa kuwa kutakuwa na shida nyingi katika nchi, na hasira juu ya taifa hili.

24 Wataanguka kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote; na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia.”

Japokuwa mji wa Yerusalemu ulimkataa Kristo, kiasi cha kumsulibisha, lakini yeye hakuacha kuwaonya juu ya mabaya yaliyokuwa yanakuja mbele yao na sio tu kuwaonya bali pia aliwaonyesha na njia ya jinsi ya Kuyakwepa mabaya hayo.. Ni upendo wa namna gani huo..

Bwana Yesu aliona kuwa mji wa Yerusalemu utakuja kuzungukwa na majeshi ya Rumi, na baadaye kuja kuteketezwa na kuchomwa moto na kibaya Zaidi watu walio ndani ya mji watauliwa vibaya sana, wengine watatekwa nyara, na wengine watatawanywa katika mataifa yote duniani..

Luka 19: 41 “Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia,

42 akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.

43 Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote;

44 watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako”

Lakini Pamoja na taarifa hiyo mbaya, hakuwaacha tu hivyo juu juu, bila suluhisho lolote.. Ndipo akawaambia sasa wakati huo watakapoyaona hayo majeshi tu yameuzunguka mji, basi wajue kuwa ndio ule wakati wa uharibifu umefika..Hivyo walio ndani ya mji huo wautoke haraka wakimbilie milimani (yaani makazi mengine yasiyokaliwa na watu)..Na walio katikati yake, yaani wale wanaoishi ndani yake, wenye manyumba basi wakatafute miji mingine ya kuishi, na wale walio katika mashamba( yaani wenye miradi yao, na biashara zao) wakatafute sehemu nyingine lakini sio pale Yerusalemu tena, kwasababu Yerusalemu unakwenda kuteketezwa siku si nyingi…

Jambo hilo lilikuja kutokea kama lilivyo miaka isiyozidi 33 baada ya Kristo kuondoka duniani..Ili kuelewa vizuri jinsi muda ulivyokuwa mfupi tangu alipotoa unabii huo hadi maangamizi yalipofika, tuseme kama leo mwaka (2020) ndio majeshi yametokea Tanzania basi Kristo alitoa unabii huo mwaka 1987… Hivyo kazazi kile chote kilichoyasikia yale maneno kilikuwepo hadi huo wakati ulipofika.

Sasa waliokuwa wameyazingatia maneno ya Kristo kwa wakati ule,walishangaa kweli kuyaona majeshi ya Rumi yamekuja kuuzingira mji, mwaka 66AD, Lakini hawakuleta madhara yoyote bado, Mungu aliruhusu iwe hivyo ili kupisha nafasi ya watu kuutoroka mji ule, sasa wale walioyasikiliza maneno ya Kristo walipoona vile, mara moja waliokuwa na miradi yao na mashamba yao, na mabenki yao, waliyaacha na kuondoka, wengine waliokuwa na majumba nao pia waliyaacha, wengine waliokuwa na mipango ya kuutembelea Yerusalemu msimu huo, wakaahirisha mipango yao..wakawa tayari kupata hasara ya mambo yao yote lakini sio hasara ya roho zao.

Lakini kulikuwa na wengine ambao waliona maneno ya Kristo kama hadithi za kizee tu, wakaendelea kubaki ndani ya mji ule na kuendelea na shughuli zao, wakitumai warumi wataondoka siku moja na kuuacha mji..na wengine wakajifariji kwamba hakutakuwa na vita yoyote, Lakini siku ya siku ilipofika, mwaka 70AD maangamizi yaliyokuwa Yerusalemu wakati ule, hadi leo kwenye historia tunayasoma..watu waliuliwa kikatili, hakuna hata mmoja aliyenusurika kutoroka, wale waliobahatika kuwa hai, walichukuliwa kama watumwa kwenda kufanyishwa kazi katika migodi sikuzote za Maisha yao, wengine wakatawanywa dunia nzima, na hekalu la pili likabomolewa halikusalia tofali juu ya tofali..(kutimiza unabii Bwana aliousema miaka 33 iliyopita)

Habari ya Israeli ilifutikia pale katika historia, mji uliharibiwa na kuchomwa moto, mpaka hekalu lile likaondolewa Yerusalemu pale..walipelekewa mbali kiasi kwamba iliwagharimu karibu miaka 1900 kurudi katika nchi yao tena..

Sasa kwanini Bwana Yesu aliwapa tahadhari ile kwanza, mpaka akaifananisha na dhiki kuu?

Ni kwasababu alikuwa anaonyesha mfano wa yatakayokuja kutokea huko mbele katika dhiki kuu HALISI, wapo wanaodhani kuwa Dhiki kuu ina muhusu kila mkristo..Biblia haifundishi hivyo..yapo makundi mawili katika kanisa, wapo wale wanaoyaishi bega kwa bega maneno ya Kristo, na hao ndio Bwana atakaowafungulia mlango wa kuikwepa dhiki kwa tendo linaloitwa UNYAKUO. Lakini wapo ambao wanafananishwa na wale wanawali wapumbavu, ambao hao wanaishi Maisha ya kubahatisha bahatisha tu, hawajishughulishi na mambo ya ufalme wa mbinguni, wapo tu, wanaridhika na hali zao za kiroho haijalishi wanazidi kuwa baridi au vuguvugu. Habari za dhiki kuu na unyakuo kwao ni kama stori za kilokole tu, na wakisikia mahubiri ya Neno la Mungu yanayowaonya, wananung’unika wanahukumiwa..

Bwana alishatupa tahadhari akasema kabisa, KESHENI,

Marko 13:32 “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba.

33 Angalieni, kesheni, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo.

34 Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe.

35 Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jimbi, au asubuhi;

36 asije akawasili ghafula akawakuta mmelala.

37 Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni”.

Siku ya Unyakuo hakuna anayeijua, lakini majira ya huo wakati tumeshapewa, tumeambia tukiona matetemeko makubwa ya ardhi, tetesi za vita duniani, tukiona magonjwa makubwa ya mlipuko yakitokea duniani kama vile CORONA. Basi tujue wakati wa mavuno umefika.

Hivyo tusishangae, moja ya hizi siku, wakati wowote, watakatifu wametoweka..Jiulize wewe ambaye hujajiweka tayari utakuwa wapi wakati huo?. Wakati wenzako wapo mbinguni kwenye karamu ya mwana kondoo, wewe utakuwa hapa chini duniani katika dhiki kuu ya mpinga-kristo, na wala usidhani ni rahisi kupona ndugu, hilo jambo halipo ikiwa leo hii unashindwa kumkiri tu Kristo, kwa mwenendo wako, kwa kukataa kuvaa vimini, na kuweka make-up, na kuvaa suruali utawezaye kumkiri kwa kifo kilichopo mbele yako..Yaani kwa ufupi ukishajiona umeachwa wewe, hukustahili katika ufalme wa mbinguni..wala hakuna tumaini lolote tena kwako. Sahau hili jambo linaloitwa nafasi ya pili. Mlango huo utakuwa kwa wengine kabisa..

Huu si wakati wa kuzidi kutanga tanga na dunia hii inayokaribia kuisha, kwasababu dunia inakwenda kuisha hii..Ni wakati wa kuyashika na kuyatunza maneno ya Yesu Kristo, kama yalivyoandikwa katika kitabu chake, Biblia takatifu.

Ufunuo 1:3 “Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

INJILI YA KRISTO HAITANGAZWI KWA HATI MILIKI.

Je ni kweli huwezi kuijua karama yako mpaka uwekewe mikono na wazee?

HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?

MAPAMBANO DHIDI YA SHETANI.

MAMBO YA KWANZA YAMEKWISHA KUPITA!

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments