Je ni kweli huwezi kuijua karama yako mpaka uwekewe mikono na wazee?

Je ni kweli huwezi kuijua karama yako mpaka uwekewe mikono na wazee?

SWALI: 1Timotheo 4:14 “Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na kwa kuwekewa mikono ya wazee.”.. Je ni kweli huwezi kuijua au kuitumia karama yako mpaka uwekewe mikono na wazee?


JIBU: Kwanza ni muhimu kufahamu wazee wanaozungumziwa hapo ni wakina nani?..wazee wanaozungumziwa hapo sio wazee wa ukoo, wala wazee wa vijiji, bali wazee wa Imani ambao ni viongozi wakongwe kiimani katika Kanisa…Na hawa wanaweza kuwa Wachungaji, Maaskofu au Mashemasi..ambao wamekaa muda mrefu wakitumika katika kazi ya Mungu. Wengi wa hawa Bwana anakuwa amewafundisha kipekee na kuwapitisha katika mambo mengi, hivyo wanakuwa wamekirimiwa hekima zaidi ya wengi katika ufahamu wa Neno..Kama vile Sulemani, alivyoandika hekima zile na kuwaita wale aliowaandikia “wanangu”

Mithali 3: 11 “Mwanangu, usidharau kuadhibiwa na Bwana, Wala usione ni taabu kurudiwa naye.

12 Kwa kuwa Bwana ampendaye humrudi, Kama vile baba mwanawe ampendezaye”.

Ni kama vile Mtume Paulo alivyowaita wanawe, wale aliowageuza na kumgeukia Kristo.

2Timotheo 2:1 “Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa ajili ya ahadi ya uzima ulio katika Kristo Yesu; kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu”.

Sasa hili kundi katika kanisa ndio linaloitwa wazee wa kanisa. Lakini pamoja na hayo, sio wote ni watumishi wa kweli wa Mungu, wapo pia wazee ambao ni mapando ya shetani..biblia imesema tutawatambua kwa matunda yao.

Sasa tukirudi kwenye swali, Je ni lazima kuwekewa mikono na wazee hawa ili karama au huduma ijidhihirishe?, na kwamba pasipo kuwekewa mikono na wazee hawa huwezi kuifahamu karama yako au huwezi kuifanya kazi ya Mungu?

Jibu rahisi la swali hili ni HAPANA!..Mikono ya wazee haiumbi karama ndani ya mtu, wala haidhihirishi karama ndani ya mtu…bali ina bariki karama ambayo tayari ipo ndani ya mtu.

Wengi wasiouelewa mstari huu, wanafikiri mpaka wazifahamu karama zao ni lazima kwanza wawekewe mikono na wazee…jambo ambalo sio sahihi kibiblia.

Katika biblia Agano jipya, tunamsoma mtu anayeitwa Paulo na Barnaba…hawa baada ya watu wote kuijua karama ambayo Mungu kaiweka ndani yao, yaani karama ya kitume…Ndipo wazee wa kanisa wakawawekewa mikono kwa uongozo wa Roho Mtakatifu, kama kuibariki huduma/ karama ambayo tayari ipo ndani yao..na hawakuwawekea kwanza mikono ndipo wakawa mitume..Hapana…Paulo alikuwa mtume tayari na alikuwa ameshapokea maagizo ya utume wake kutoka kwa Bwana Yesu mwenyewe, tangu alipokuwa anaeleke Dameski…hivyo kilichokuwa kimesalia ni watu tu kuibariki huduma hiyo, na hata kama watu wasingeibariki bado Mungu angeendelea kuibariki tu, isipokuwa kuombeana kule kunazidi kuongeza neema ya Mungu juu ya huduma ya mtu, hivyo kuna umuhimu pia mkubwa sana…Tusome,

Matendo 13:2 “Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.

3 Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao”.

Umeona hapo?..Neno linasema “Nitengeeni Paulo na Barnaba kwa kazi ile niliyowaitia” maana yake..tayari walikuwa wameshapewa huduma/kazi na Mungu..na sio kwamba walipokea huduma au karama ile siku ile ya kuwekewa mikono au baada ya kuwekewa mikono.

Hali kadhalika hata sasa, mtu aliyeokoka anapewa huduma na Mungu mwenyewe na si mwanadamu…hakuna mantiki yoyote kwenda kutafuta kupokea karama yako kutoka kwa mtumishi au mchungaji au mwanadamu yoyote Yule..Mungu aliyekuita atakufunulia wewe mwenyewe wito aliokuitia….na baada ya kukufunulia, wewe mwenyewe utaujua na watu wote wa kanisa watauona wito wako…na wakishaona kwamba Fulani anawito kweli katika eneo Fulani, labda anahubiri Neno kwa bidii na kwa moyo, anaombea watu kwa bidii, anaimba kimaandiko kwa bidii, anafariji watu kwa bidii, anahudumia watu hivi au vile kwa bidii n.k..Hapo sasa ndipo wazee wanakusanyika pamoja kwa uongozo wa Roho Mtakatifu na kuweka mikono juu ya mtu huyo…Na lengo la kufanya vile ni kuibariki ile kazi Mungu aliyoianzisha ndani yake, kumbariki kwamba Bwana azidi kuichochea karama ile iliyomo ndani yake kwa bidii sana hilo tu na si kumpa ile karama..Na tendo hilo lina nguvu sana katika Roho.

Lakini sio tu, mtu hajaokoka, au hajui lolote, wala hatumiki popote na anakwenda kutafuta kuwekewa mikono ili aipate karama..kama leo hii utaona manabii wa uongo wanawaita watu na kuwashika na kuwaambia nimekupa karama ya kinabii, kuanzia leo utaona maono, au nimekupa karama ya kiualimu kuanzia leo utafundisha, au nimekupa karama ya kiutume, au ya uimbaji…hapo hutaambulia chochote zaidi ya maroho ya Yule adui. Vipawa na karama anayetoa ni mmoja tu! naye ni BWANA YESU! MKUU WA UZIMA. Huyo pekee ndio biblia inasema alipopaa mbinguni aliteka mateka akawapa wanadamu vipawa (Waefeso 4:8)…hivyo hakuna mwadamu wala mwinjilisti, wala mwalimu wala Padre, wala nabii wala papa mwenye uwezo wa kumpa mtu karama au kipawa.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

KUMBUKA, VIVUKO VYA YORDANI VINAKUNGOJA MBELENI.

NI WAPI MAHALI SAHIHI PA KULIPA ZAKA?

NA MTU MMOJA AKAVUTA UPINDE KWA KUBAHATISHA, AKAMPIGA MFALME

BIBLIA INATUASA TUFANYE NINI KATIKA ZAMA HIZI ZA UOVU?

DANIELI:Mlango wa 5

HATUA ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA KUTUONGOZA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Devis Julius administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Yustina J. Kagito
Yustina J. Kagito
3 years ago

Asante sana ujumbe huu nimeupata kwa muda sahihi kabisa.
Mbarikiwa kiwe sana.