KAMA TUNATAKA KUWA ASKARI WA BWANA, NI LAZIMA TUJUE VIGEZO.

KAMA TUNATAKA KUWA ASKARI WA BWANA, NI LAZIMA TUJUE VIGEZO.

Shalom mpendwa, Karibu katika kuyatafakari maneno ya uzima..

Tunaijua Habari ya Gideoni na wanajeshi wake 300, lakini ni vizuri tukajikumbusha tena, naamini lipo jambo jipya tutajifunza leo ndani yake..Tusome..

Waamuzi 7:4 “Bwana akamwambia Gideoni; Hata sasa watu hawa ni wengi mno; uwalete chini majini, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako; kisha itakuwa ya kwamba yule nitakayekuambia, Huyu atakwenda pamoja nawe, ndiye atakayekwenda pamoja nawe; na mtu yule nitakayekuambia, Huyu hatakwenda pamoja nawe, basi mtu huyo hatakwenda.

5 Basi akawaleta watu chini majini. Bwana akamwambia Gideoni, Kila mtu atakayeyaramba maji kwa ulimi wake, kama vile arambavyo mbwa, huyo utamweka kando; kadhalika kila mtu apigaye magoti kunywa.

6 Na hesabu ya hao waliokunywa kwa kuramba-ramba, wakipeleka mkono kinywani, ilikuwa watu mia tatu; bali watu wengine wote walipiga magoti kunywa maji.

7 Bwana akamwambia Gideoni, Kwa watu hawa mia tatu walioyaramba maji nitawaokoa, nami nitawatia Wamidiani katika mikono yako; lakini watu hawa wote wengine na waende zao, kila mtu mahali pake”.

Amen.

Ukitazama hapo, utaona lile kundi la kwanza walipofika tu majini jambo la kwanza walipiga magoti, jambo ambalo wale wengine hawakulifanya…

Pili walikutanisha midomo yao na yale maji ya mto moja kwa moja.Kwasababu walikuwa na kiu sana, hivyo njia pekee walioina kuwa itaondoa kiu yao kwa haraka ni kwa kupelekea midomo moja kwa moja majini, ili wanywe kwa haraka haraka bila bugdha yoyote.

Tofauti na wale wenzao, ambao walikuwa kwanza wanayakusanya maji kwenye mikono yao, kisha wanayalamba kidogo kidogo, kisha tena wanachota na kulamba hivyo hivyo, kidogo kidogo hadi walipokata kiu yao..

Walikuwa wanahakikisha kwanza kile wanachokinywa kabla ya kukinywa, bila kujali kuwa yatakuwa yanakaa kidogo tu kwenye mikono yao, na kuvuja vuja..Bila kujali kujitesa kuchota chota kila mara.

Pia walikataa kupiga magoti kuelekea maji, bali waliinama tu, au walichuchumaa, na hiyo ikawapa wigo mzuri wa kuona hatari iliyo mbele yao, kiasi kwamba hata adui angetokea mbele yao wangeweza kuacha wanachokifanya na kupigana nao, tofauti na wale wengine..

Vivyo hivyo, hata sisi, ni kweli tupo ulimwenguni, na wakati mwingine itatupasa tuchume vya ulimwenguni kidogo, lakini tukijisahau kuwa tupo mapambanoni na adui yetu shetani yupo mbele yetu, tukayapigia magoti mambo ya ulimwengu huu.. yaani kufanya mambo ya ulimwengu huu kuwa ndio kila kitu kwetu.Tujue kuwa hatufai kwa ufalme wa mbinguni.

Sio kila kinachokuja mbele yetu, ni cha kukipaparikia kwa moyo wote, sio kila fursa ni kutoka kwa Mungu vingine ni mitego ya adui,..Unapaswa uchague kazi, unapaswa uchague marafiki, unapaswa uchague mazingira ya kuishi..Sio kila kazi ilimradi tu inakupa pesa ni ya kuifanya..Unapaswa uipitishe kwanza kwenye mikono yako ya rohoni, uangalie je! Hii kazi ni salama, haitaniletea athari yoyote katika wokovu wangu huko mbeleni? Je hii kazi ni kulingana na Neno?..

Sasa ukishaiona haiikinzani na Neno la Mungu na haina madhara kiimani, ndipo unairamba tena kidogo kidogo, na sio kuikurupukia.. Kila tenda inayokuja inaipitisha kwenye maandiko kwanza, je ina sumu ya adui?..kama askari hawa walivyoipitisha maji mikononi kwanza kabla ya kuyanywa…Unaitazama je! Ina rushwa ndani yake?, je ina utapeli ndani yake n.k

Lakini kama hutajiuliza chochote wewe, kila fursa inayokuja mbele yetu, tunaipaparikia hutufai kuwa askari wa Mungu..haijalishi ni nzuri vipi, kwasababu huwezi jua baadaye itakufanya hata ule wakati wako uliokuwa unautumia kuomba unamezwa na shughuli hizo, au jumapili yako ulikuwa unakwenda ibadani sasa, inaingiliwa na kazi hizo, au mavazi yako uliyokuwa unavaa ya staha yanageuzwa na kuwa ya kikahaba.

Vile vile na marafiki pia, sio kila mtu unayekutana naye ni lazima awe Rafiki yako tu, unapaswa umpitishe kwanza kwenye mikono yako ya rohoni, kisha ukimwona anaendana na Imani yako, ndipo uanze kuunga naye urafiki, tena kidogo kidogo, mpaka utakapomthitisha kamili baada ya muda mrefu..Wengi leo wanawachunguza marafiki kama ni washirikina tu!..hicho ndicho wanachoweza kuchuguza..lakini hawawez kuchunguza huyu rafiki kama ni mlevi, au kama ni mtu wa rushwa, au mtu wa kutomjali Mungu..wengi hayo macho hawana, wana macho tu ya kuchunguza ushirikina.

Vilevile na mazingira, sio kila mazingira yanayokujia mbele yako ni ya kuishi au kukubaliana nayo..chunguza kwanza..Chunguza chochote kile kabla hujakifanya ukikilinganisha na wokovu wako, Je, ni salama?..kwasababu wokovu ni kitu cha kulinda na kukipigania kuliko kitu kingine chochote. Biblia inasema Imani tumekabidhiwa mara moja tu!

Kwasababu mitego ya adui ipo kila kona. Mungu aliona mbele ndio maana hakuwaruhusu wale wengine waende vitani, kwasababu alijua huko mbeleni, askari wataishiwa nguvu sana, watakuwa na kiu na njaa, lakini bado mapambano hayajaisha, Je watakuwa tayari kutotazama mambo ya mwilini wakaendelea na mapambano? (Soma Waamuzi 8:4). Ndio maana akawatenga wale 300 tu..waliovumilia kunywa maji kwa uangalifu na taratibu taratibu.

Na sisi pia tukitaka tuwe askari kamili wa Kristo, Bwana atusaidie tuyazingatie hayo….

Mungu akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Je Mtu anaweza kusema uongo, Na Mungu akambariki?

KILA MTU ATATOA HABARI ZAKE MWENYEWE.

BIBLIA INATUASA TUFANYE NINI KATIKA ZAMA HIZI ZA UOVU?

Je! habari ya Yusufu, inabeba ujumbe gani kwa agano jipya?

NINI NI KILICHOMFANYA IBRAHIMU AKUBALI KUMTOA MWANAWE SADAKA?

JE! KUBET NI DHAMBI?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
4 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Joseph Stephen Mwinuka
Joseph Stephen Mwinuka
3 years ago

Shalom!Mungu awabariki sana kwa kazi hii nzuri ya uinjilishaji.Naomba kutumiwa masomo haya

daudi j rogathe
daudi j rogathe
3 years ago

Mungu awabariki kwa kazi yenu nzuri