by Admin | 1 June 2021 08:46 am06
“Mahali pa juu” ni mahali palipoinuka ambapo watu walikwenda kutengeneza madhabahu na kutoa dhabihu zao.. Mahali hapo panaweza kuwa ni mlimani au mahali penye mwinuko. Ilikuwa ni heshima kwa Mungu kutengeneza madhabahu mahali palipoinuka, kuonyesha kuwa yeye ni juu ya yote.
Ibrahimu ni moja ya watu wa kwanza kutenengeneza madhabahu mahali pa juu.. Wakati anamtoa Isaka mwanawe, alipanda juu ya Moria, na kutengeneza madhabahu pale, sasa mahali pale alipojenga madhabahu ile ndio mfano wa “mahali pa juu”..
Ifuatayo ni baadhi ya mifano michache juu ya mahali pa juu…
1Samweli 9:11 “Hata walipokwea kwenda mjini, wakakutana na wasichana, wanatoka kwenda kuteka maji; wakawaambia, Je! Mwonaji yuko?
12 Nao wakawajibu, wakasema, Yuko; tazama, yuko huko mbele yako; fanyeni haraka sasa, maana hivi leo amekuja mjini; kwa sababu WATU WANA DHABIHU LEO KATIKA MAHALI PA JUU”
Na pia tunaona kabla Mfalme Sulemani kujenga hekalu lile juu ya mlima Moria, naye pia alikuwa anatoa dhabihuu katika mahali pa juu..
1Wafalme 3:2 “Ila watu walikuwa wakichinja dhabihu katika MAHALI PA JUU, kwa sababu haikuwapo nyumba iliyojengwa kwa jina la Bwana, hata siku zile.
3 Sulemani naye akampenda Bwana, akienda katika amri za Daudi babaye, ila hutoa dhabihu na kufukiza uvumba katika MAHALI PA JUU”
Mistari mingine inayozungumzia mahali pa juu ni pamoja 1Nyakati 16:39, 1Nyakati 21:29.
Lakini pamoja na hayo, walikuwepo pia watu waliotengeneza madhahabu katika mahali pa juu kwaajili ya miungu yao… popote walipopaona pameinuka walizitengeneza madhabahu hizo, na kuitolea dhabihu miungu hiyo, jambo ambalo lilikuwa ni chukizo kubwa sana kwa Bwana.
1Wafalme 14:22 “Basi Yuda wakafanya maovu machoni pa Bwana; wakamtia wivu, kwa makosa yao waliyoyakosa, kuliko yote waliyoyafanya baba zao.
23 Maana hao pia wakajijengea MAHALI PA JUU, na nguzo, na maashera, juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi”.
Unaweza pia kusoma 2Wafalme 16:4, 2Wafalme 17:9-11,29, utaona jambo hilo hilo..
Swali ni je! Mahali petu pa juu pa leo ni wapi?..mahali ambapo tunaweza kumtengenezea Mungu wetu madhahabu inayompa heshima yeye?.
Tusome,
Yohana 4:19 “Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii!
20 Baba zetu waliabudu katika MLIMA HUU, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.
21 Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu.
22 Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.
23 LAKINI SAA INAKUJA, NAYO SASA IPO, AMBAYO WAABUDUO HALISI WATAMWABUDU BABA KATIKA ROHO NA KWELI. KWA MAANA BABA AWATAFUTA WATU KAMA HAO WAMWABUDU
24 Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli”
Umeona mahali petu palipoinuka leo ni wapi?..Si milimani, wala si mahali penye miinuko, bali ni katika roho zetu. Huko ndiko madhabahu za Mungu aliye juu zinapotengenezwa.
Je ndani ya roho yako ipo madhabahu ya Mungu?..au ya miungu?..Haijalishi utakuwa unakwenda kanisani, au unatoa sadaka lakini kama mahali pa juu (yaani ndani ya roho yako), hakuna madhabahu ya Mungu, basi fahamu kuwa bado unaitumikia miungu migeni. Kama moyoni mwako kuna anasa, ulevi, wizi, uasherati, na mengineyo, bado wewe ni najisi mbele za Bwana.
Mathayo 15:19 “Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano”.
Bwana atusaidie tumjengee madhabahu bora katika roho zetu.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Swali: Kurushwa upesi kunakozungumziwa katika Danieli 9:21 ndio kupi?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/06/01/mahali-pa-juu-palikuwa-ni-wapi-kama-tunavyosoma-katika-biblia/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.