SIKU YA HOFU YANGU NITAKUTUMAINI WEWE.

by Admin | 19 July 2021 08:46 pm07

Daudi alisema..

Zaburi 56:3 “Siku ya hofu yangu nitakutumaini Wewe;

4 Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake. Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwenye mwili atanitenda nini”?

Maadamu tupo hapa duniani, haijalishi tutakuwa ni watakatifu au mkamilifu kiasi gani, lakini maadamu tunaishi chini ya jua, zipo siku ngumu tutapishana nazo katika safari yetu ya imani. Hizo ni  nyakati zenye masumbufu sana, zenye kuvunjika moyo kusikokuwa kwa kawaida, zenye huzuni nyingi sana, zenye machozi na majonzi, Daudi alizitambua nyakati hizo na kuziita  “SIKU ZA HOFU YANGU”.

Na hizi zinatofautiana kati ya mtu na mtu, mwingine Siku ya hofu yake, ni vipindi cha Misiba.  Pengine amefiwa na mpendwa/wapendwa wake wa karibu sana kwa ghafla, labda kwa ajali mbaya, hichi kipindi huwa ni kigumu sana isivyoelezeka. Mfano wa watu kama hawa kwenye biblia alikuwa ni Ayubu, aliyefiwa na watoto wake wote 10 kwa mkupuo.

Mwingine,  siku ya hofu yake ni siku za kuwindwa na maadui ili auawe, mfano wa watu hawa ndiye kama Daudi mwenyewe aliyeandika habari hiyo. Yeye ilifikia wakati serikali nzima inamwinda, imwangamize. Embu jiweke wewe katika hiyo nafasi, maisha yako yote, unajificha mapangoni tu, kwasababu umesikia kuwa raisi na watumishi wake wote wa usalama wametumwa nchi nzima kukuwinda ili wakuue. Si jambo jepesi.

Mwingine siku ya hofu yake ni siku za  magonjwa. Amepatwa na ugonjwa wa ghafla ambao pengine hakuwahi kudhani kama ungemfikia mtu kama yeye, labda Ukimwi, au Kansa, au amepata ajali, na ikamletea ulemavu wa kudumu, kama vile kiharusi, au ukiwete, au kalazwa ICU, kwa kwa kipindi kirefu, huo wakati unakuwa ni mgumu sana kuchukulika,. Mfano wa mtu kama huyu ni Eprafodito ambaye alikuwa  ni mtume aliyetenda kazi pamoja na akina Paulo, yeye  ilifikia wakati hali yake ikawa mbaya sana karibu na kufa kwa kuugua.(Wafilipi 2:25-27)

Mwingine siku ya hofu yake ni siku ya kusalitiwa.  Aidha Kusalitiwa na ndugu yake katika imani, au kusalitiwa na wazazi kisa ameokoka, au kusalitiwa na mke/mume, au kusalitiwa na marafiki.  Kama vile Bwana Yesu alivyosalitiwa na Yuda. Huu pia si wakati mwepesi, hauchukuliki kirahisi. Jambo kama hili linaweza kumpelekea mtu mwingine hata kujinyonga, au kuleta madhara yoyote kwa wengine.

Mwingine siku ya hofu yake, ni siku za kukumbana na hasara. Kupoteza kila kitu, kupoteza mali zake alizozisumbukia, au fedha, au mashamba, au mifugo, kama vile Ayubu kiasi kwamba habakiwi na chochote. Madeni yamemsonga,  bado familia inamwangalia, akiangalia mikopo anapaswa arudishe,na asiporudisha nyumba inauzwa, jambo ambalo hakutegemea kabisa kama lingemtokea kwa haraka hivyo.  Hichi kipindi huwa ni kigumu pia, sio cha kuchukulika kiwepesi.

Na vipindi vingine vyote vya namna kama hiyo..

Sasa ukijikuta katika siku kama hizo, na wewe umekoka, usiwe na haraka kumkatia tamaa Mungu, usiwe mwepesi wa kukimbilia kwa wanadamu, vilevile usitoe maneno ya kukufuru, au kupeleka manung’uniko  yote kwa Mungu. Bali zidi kumtumaini yeye, kama Daudi alivyosema “Siku ya hofu yangu nitakutumaini Wewe”.. Kuwa mtulivu kama Ayubu, utakumbuka hata wakati ambapo mke wake anamshauri amkufuru Mungu afe lakini yeye alimkemea  na kumwambia asiwaze kipumbavu kama wengine wafanyavyo,  Na wewe pia mtazame Mungu peke yake, usiwe na maneno mengi kwake katika siku kama hizo, na kuanza kusema kwanini hivi, kwanini vile, mtazame Mungu tu ndugu. Zipo sababu nyingine zilizo juu ya upeo wa ufahamu wako usizozijua.

Siku kama hizo , kifungu hichi kiwe faraja yako wakati wote..

Yeremia 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho”.

Mtazame mtu kama Ayubu jinsi mwisho wake ulivyokuwa wa faraja, kwani yote aliyoyapoteza Mungu alikuja kumrudishia mara mbili, hata watoto nao Mungu alimpa wengine wazuri kushinda hata wale wa kwanza, na hata siku ile ya ufufuo bado Mungu atamkutanisha na wale watoto wake wa kwanza aliowapoteza.

Yakobo 5:11 “Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma”.

Daudi naye, japokuwa alilemewa na maadui zake (Sauli), lakini bado hakuacha kumtumainia Mungu, mwisho wa siku Mungu akamlinda, na kumuhifadhi hai, na kumstarehesha katika ufalme wake.

Nawe vivyo hivyo fahamu tu, mwisho wako utakuja kuwa mzuri endapo utaendelea tu hivyo hivyo kushikamana na Bwana. Kwasababu yeye ni mwingi wa rehema na huruma, kumbuka anajishughulisha sana na mambo yetu, Na zaidi ya yote alishayachukua masikitiko na fadhaa zetu zamani sana(Isaya 53:4).

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.

Waoga ambao hawataurithi uzima wa milele ni watu wa namna gani?(Ufunuo 21:8).

Mungu anaposema “nitaliweka jina langu” ana maana gani?

KUWA MAKINI NA MITANDAO, NI SHIMO REFU.

NAWE UTAGEUZWA KUWA MTU MWINGINE.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/07/19/siku-ya-hofu-yangu-nitakutumaini-wewe/