by Admin | 9 November 2021 08:46 am11
Shalom, Jina la Bwana wetu, Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu.
Katika ulimwengu wa sasa, ukitaja mama wa kambo, au baba wa kambo, tayari picha ya kwanza inayotengenezeka kwenye vichwa vya wengi ni MATESO.
Lakini leo napenda tujifunze kitu kingine tofauti na hicho, ili tusije tukajikuta tunazuia baraka zetu pasipo sisi kujua.
Jambo la kwanza la kufahamu kabla hatujaingia kwenye kiini cha somo ni kwamba, popote pale unapojikuta upo, au umezaliwa, na kulelewa..jua Mungu kakuweka hapo kwa kusudi maalumu, ambalo ni la baraka.
Sasa turudi kwenye swali letu!. Je! Ni laana au mkosi, kuzaliwa au kulelewa na mama wa kambo au baba wa kambo?.
Tutalijibu swali hili, kwa kujifunza juu ya maisha mmoja katika biblia, na huyo si mwingine zaidi ya Bwana Yesu, Mkuu wa uzima..
Maandiko yanasema “tujifunze kwake”..Maana yake tumtazame yeye, tuyaangalie maisha yake, na tupate masomo (Mathayo 11:29).
Na leo tutapata somo lingine kutoka katika maisha yake.
Sasa wengi wetu hatujui kuwa Bwana wetu Yesu, alilelewa na Baba wa kambo katika mwili (Ni lugha ngumu kidogo hii, lakini ndivyo ilivyo).
Yusufu hakuwa Baba kamili wa Bwana Yesu. Mimba aliyoipata Mariamu haikumhusisha baba, ilikuwa ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu (soma Mathayo 1:18).
Baba wa Bwana Yesu, alikuwa ni Roho Mtakatifu.
Hivyo ni sahihi kabisa kusema, Yusufu alikuwa ni baba wa kambo wa Bwana Yesu.
Lakini ulishawahi kujiuliza ni kwanini Mungu aruhusu aishi na baba wa kambo?, kwani alishindwa kumfungulia Mariamu mlango, aishi mwenyewe tu na mtoto Yesu?.. Mungu angeweza kufanya hivyo, kwani yeye ni mweza wa kila kitu.
Angeweza kufungua mlango wa mali nyingi, kipindi Bwana Yesu anazaliwa na kumfanya Mariamu aishi maisha ya kifahari peke yake na mtoto Yesu, na pia angeweza kuzuia Yusufu asipose Mariamu kabisa..
Lakini hakufanya hivyo bali kinyume chake, baada tu ya Mariamu kuposwa ndipo mimba inaonekana..Na baada ya Yesu kuzaliwa, akaanza kubebwa na baba huyo huyo wa kambo, na hata wakati wa kazi ya ufundi, alifanya kazi ya baba huyo huyo wa kambo!.
Bwana aliruhusu maisha yake yawe hayo, ili kutufundisha na sisi kuwa si laana kuishi hayo maisha.
Sasa kulikuwa kuna nini kwa Yusufu, mpaka mkuu wa Uzima, Yesu Kristo apitie pale?
Yusufu alikuwa ni maskini kweli, hakuwa tajiri, lakini alikuwa amebeba ahadi ya kifalme, kumbuka Mungu alimwahidi Daudi, kwamba kupitia uzao wake atatokea Mfalme. Na Yusufu alikuwa ni wa Uzao wa Daudi.
Hivyo ili Bwana Yesu awe mfalme kupitia ahadi hiyo ya Daudi, ilikuwa hana budi azaliwe katika Hema ya Yusufu..angezaliwa pengine popote, ahadi hiyo ya Mungu isingetimia.
Mpaka hapo utakuwa umeanza kuona hata wewe ni kwasababu gani… umelelewa na huyo baba wa kambo Au mama wa kambo.
Haijalishi anakutesa kiasi gani, au ni maskini kiasi gani, lipo kusudi kwanini upo hapo, au umelelewa hapo, kuna baraka ambazo huwezi kuziona kwa macho!..
Kuzaliwa kwa Bwana kwenye lile zizi, chini ya Bwana Yusufu asiyekuwa na kitu, kulikuwa na maana kubwa.
Na wewe vile vile..tengeneza mambo yako vizuri sasahivi kwasaababu kuna baraka tele, mbele yako.
Ishi na Baba yako huyo vizuri, mheshimu, mbariki kwasababu ni Mungu ndiye aliyekuweka hapo, hujajiweka mwenyewe..na Mungu ndiye anayeijua mbele yetu..
Usianze kuharibu mambo kwa kunung’unika, unapopitia vikasoro vidogo vidogo, wewe tazama mbele, ongeza utii na heshima.
Kadhalika na kama wewe ni baba au ni mama na una watoto wa kambo, ishi nao vizuri, kwasababu nao pia wamebeba ahadi, ahadi hiyo isingeweza kukamilika pasipo wewe. Na mwisho utaona faida kubwa mbeleni.
Utasema vipi na mama wa kambo?
Musa alilelewa na Mama wa kambo, Binti Farao, hakujua atakuja kuwa nani..lakini maandiko yanasema, baadaye Mungu alikuja kumfanya Musa kuwa kama “mungu kwa Farao”.
Kutoka 7:1 “BWANA akamwambia Musa, Angalia, nimekufanya wewe kuwa kama Mungu kwa Farao; na huyo ndugu yako Haruni atakuwa nabii wako”.
Alienda kwa binti Farao, ili kupata jina hilo MUSA, Jina hilo alipewa na “mama wa Kambo”…hakupewa na mama yake mzazi, wala halikuwa jina la kiyahudi..
Na cha ajabu ni kwamba, Mungu hakumbadilisha jina Musa…aliendelea nalo hilo hilo, Sauli alibadilishwa na kuwa Paulo, Yakobo alibadilishwa na kuwa Israeli, lakini Musa amebakia kuwa Musa mpaka leo…kumbe wito wake ulikamilishwa pia na mama wa kambo.
Hivyo tunachoweza kujifunza ni kuwa macho ya kiroho kuona mbele na si hapa tu..katika nafasi uliyopo kama unaishi na baba au mama wa kambo, mheshimu kama Baba yako na kama mama yako, unapoona shetani ananyayuka na kujaribu kuharibu uhusiano wenu.. basi ni wakati wa wewe nyanyuka na kuongeza maombi…usiende kusikiliza simulizi za kishetani zinazosimuliwa huko na huko katika mitandao na katika vijiwe kuhusu ubaya wamama au wababa wa kambo, utajizolea elimu zitakazoharibu maisha yako..Biblia ndio kitabu chetu na mwongozo wetu.
Kama Bwana Yesu aliishi na Baba wa kambo, na kufanya naye kazi moja na bado akawa mfalme, ni kitu gani kitakachokuzuia wewe kufikia baraka zako, kupitia huyo mzazi au mlezi ambaye si wako?.
Kadhalika na kama wewe ni mzazi, au mlezi wa mtoto ambaye si wako, usimkatae mtoto wa kambo, kwasababu hujui ana ahadi gani kupitia wewe.. Na Mungu amekuchagua wewe, kwasababu na wewe pia unabaraka juu yake.
Hivyo kwa hitimisho ni kwamba hakuna laana yoyote kuishi au kulelewa na Baba au mama wa kambo. Vile vile hakuna laana yoyote au mkosi, kulea mtoto wa kambo.
Bwana akubariki.
Ikiwa bado hujamwamini Bwana Yesu, ni vyema ukakata shauri sasa kwasababu siku tunazoishi hizi ni siku za mwisho.
Na Bwana Yesu alisema.. “Itatufaidia nini tupate ulimwengu mzima halafu tupate hasara ya nafsi zetu”
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/11/09/je-ni-laana-kulelewa-na-baba-au-mama-wa-kambo/
Copyright ©2025 unless otherwise noted.