JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 4)

by Admin | 21 December 2021 08:46 pm12

Nakusalimu katika jina kuu sana  la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu katika kujifunza Neno la Bwana. Bado tupo katika mwendelezo wa thawabu mbalimbali za Mungu, na vigezo anavyovitumia kuzitoa. Hii sehemu ya 4.

4) Zipo thawabu kwa wanaowasadia  maskini na wasiojiweza.

Bwana Yesu alimwambia yule Farisayo Tajiri aliyemwalika katika karamu yake maneno haya;

Luka 14:12 “Akamwambia na yule aliyemwalika, Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo.

13 Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu,

14 nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki.

15 Basi aliposikia hayo mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye alimwambia, Heri yule atakayekula mkate katika ufalme wa Mungu”.

Ikiwa wewe ni mtakatifu Umeokoka, usisahau, kuwakumbuka watu wenye mahitaji, na wasiojiweza kwa kile Mungu alichokujalia, kwasababu kina thawabu yake kubwa mbinguni siku ile Bwana atakapowafufua wateule wake ili kuwapa thawabu.

Unapotoa msaada, au unapofanya sherehe, usiwaalike tu, watu wenye uwezo, bali tafuta na wengine wasio na kitu cha kukurudishia, tusiwaalike watu tu waliotuchangia, bali tuwaalike pia, na wasioweza kuchangia, kwasababu, tutakuwa tumejiwekea hazina nzuri mbinguni.. Mtume Paulo alikuwa na bidii kulifanya hilo, pale alipousiwa na mitume waliomtangalia. Alisema..

Wagalatia 2:9 “tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara;

10 ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami neno lilo hilo nalikuwa na bidii kulifanya”.

Unaona? Hivyo na sisi tuwaonapo maskini, na mayatima, na wenye mahitaji, basi tujue hapo ni mahali petu pa kujichumia thawabu zetu nyingi, tufanye bidi kuwasaidia. Kwasababu tukifika mbinguni, utajiri wetu, utapimwa kwa matendo kama haya, lakini kama kila tulichokuwa tunakipata, tunakula wenyewe, au na watu wenye uwezo kama sisi, tujue kuwa tunapunguza kiwango cha utajiri wetu mbinguni. Kutoa si mpaka tuwe na vingi, ukipata sh.100, inatosha, kuwaga 50, kwa maskini na nyingine ukatumia wewe.

Bwana atusaidie tulione hilo, tuanze sasa kuwakumbuka na watu wengine wenye uhitaji.

Bwana akubariki.

Usikose mwendelezo..

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/12/21/jinsi-mungu-atakavyotoa-thawabu-4/