by Admin | 31 January 2022 08:46 pm01
Imekuwa changamoto kubwa kwa mtu anayeokoka mara ya kwanza, au kwa yule mtu ambaye anahitaji kumwabudu Mungu katika njia sahihi, kutambua kanisa sahihi la kumfanya yeye amwabudu Mungu wake katika Roho na kweli.
Hiyo ni kutokana na kuzuka kwa imani nyingi potofu, na watu wenye nia mbaya, ambao lengo lao ni kuwapoteza watu na sio kuwaokoa.
Hivyo wewe kama mkristo huna budi kuwa mchunguzi sana, na Mungu pia ameruhusu tuwe watu wa namna hiyo sawasawa na (1Timotheo 4:1 )..kwasababu hizi ni zama za uovu.
Lakini pamoja na kwamba kuna makanisa na imani nyingi za uongo ulimwenguni, bado suluhisho sio kukaa nyumbani..kwasababu ni agizo la Bwana kwamba tusiache kukusanyika pamoja na wengine, kumwabudu yeye(Waebrania 10:25)..Na faida zake ni nyingi sana, tofauti na utakavyokwenda mwenyewe mwenyewe, wakati wote. Hata ukutanapo na jiwe katika chakula haikufanya wewe umwage chakula chote..utalitoa lile jiwe utaendelea kula..Vivyo hivyo na katika habari ya makanisa.
Lakini pia kumbuka kujiunga na kanisa sio tiketi ya wewe moja kwa moja kwenda mbinguni..lakini kanisa sahihi lina sehemu kubwa sana ya kukusaidia wewe kufika mbinguni.
Makanisa yanafananishwa na SHULE. Kwamfano mwanafunzi anayehitimu shule ya msingi..akienda sekondari, huwa anakutana na chaguzi nyingi sana za shule zikimwita..na kila shule inajinadi kuwa ina ufauluji mzuri, na mazingira mazuri ya kusomea..
Hivyo ni wajibu wa mwanafunzi mwenyewe kufanya uchunguzi wake mwenyewe je, ni kweli shule hiyo ina vigezo vya kumsaidia kufaulu? .Uchaguzi wa shule mbaya utamweka katika hatari kubwa sana ya kufeli haijalishi atakuwa na akili nyingi kiasi gani.
Lakini pamoja na kwamba shule itakuwa na ubora na ufauluji mzuri, bado bidii ya mwanafunzi mwenyewe binafsi inahitajika..
Hivyo vyote viwili vinasaidiana na vina umuhimu, na vinakwenda sambamba. Tengeneza picha mwanafunzi anayesema mimi siendi shule..nitatafuta tu namba yangu ya mtihani wa mwisho siku hiyo ikifika nikafanye.. nitakuwa najisomea peke yangu nyumbani kwa miaka yote hiyo.. Jiulize mwanafunzi kama huyo atafaulu kweli..lengo la shule kuwekwa ni kumsaidia mwanafunzi ufauluji wake, kwa kukutanishwa na waalimu wa kumsaidia na kumpa nidhamu ya usomaji bila kuvutwa na mambo mengine..
Halikadhalika ukristo na kanisa ni vitu vinavyokwenda sambamba, na ni wajibu wako kuchagua kanisa sahihi litakalokusaidia kufanikisha safari yako ya wokovu hapa duniani.
Mpaka hapo naamini umepata picha..hivyo vifuatavyo ni vigezo muhimu sana vya kuukusaidia kutambua kanisa sahihi ni lipi
1) YESU KRISTO ndio kiini cha imani hiyo.
Tunapouzungumzia ukristo, tunamzungumzia Yesu Kristo, kanisa lisilomfanya Kristo peke yake ndio msingi wa imani hiyo. Ni kanisa la uongo. Ukiona halimtaji Kristo kwa kila kitu..Kimbia hilo kanisa..ikiwa jina la nabii au kiongozi ndio linatamkwa na kupewa heshima kubwa kuliko Kristo..ondoka haraka sana hapo..
Vilevile ukiona Bwana Yesu analinganishwa na watakatifu wengine, kana kwamba na wenyewe ni wapatanishi wa dhambi zetu kama yeye..mfano wa Yosefu na Maria. Ondoka pia hapo, haijalishi litakuwa na wafuasi wengi au zuri kiasi gani.
Wakolosai 2:18-19
[18]Mtu asiwanyang’anye thawabu yenu, kwa kunyenyekea kwa mapenzi yake mwenyewe tu, na kuabudu malaika, akijitia katika maono yake na kujivuna bure, kwa akili zake za kimwili;
[19]wala hakishiki Kichwa, ambacho kwa yeye mwili wote ukiruzukiwa na kuungamanishwa kwa viungo na mishipa, hukua Kwa maongeo yatokayo kwa Mungu.
2) Pili, kanisa la kweli Linaamini Biblia Takatifu tu ndio mwongozo wake.
Ni lazima liamini Biblia yenye vitabu 66, na si zaidi wala pungufu..yapo madhehebu ambayo yameongeza vitabu vya Apokrifa katika biblia na kuifanya iwe na vitabu 73.
Ukiona dhehebu hili ondoka hapo, vitabu vyovyote nje ya vile vinavyojulikana yaani 66 havijaviviwa Roho Mtakatifu.
Ufunuo wa Yohana 22:18
[18]Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.
Halikadhalika yapo mengine yanaamini katika mapokeo, kama vile waaminivyo bibila takatifu hayo pia yakimbie ni upotevu na udanganyifu mwingi upo ndani yake.
Utapotezwa tu..
3) Tatu linafundisha mafundisho yanayolenga ufalme wa mbinguni.
Yohana mbatizaji alipoanza kuhubiri alisema tubu kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia..Bwana Yesu naye alihubiri kwa kusema tubuni kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia(Mathayo 3:2, 4:17)…mitume nao walihubiri na kufundisha vivyo hivyo.
Nasi pia tujue ukristo, ni habari za ufalme wa mbinguni na sio ufalme wa duniani..Ikiwa utakuwepo mahali unafundishwa na kushinikizwa tu juu ya mambo ya ulimwenguni wakati wote..yaani mali, na vitu vya ulimwenguni..hiyo ni ishara kuwa kanisa hilo ni la uongo..hivyo ondoka hapo.
Ndio zipo nyakati, hayo nayo yatafundishwa katika kanisa lakini sehemu yao iwe ndogo sana, yasiwe kiini cha mtu kuwepo kanisani kumwabudu Mungu. Kanisa ni habari za ulimwengu ujao.
4) Utakatifu na Upendo:
Huu nao ni msingi mwingine wa kanisa hai la Kristo, kufundishwa utakatifu na Upendo ambavyo vyote viwili ndio vinatajwa kama malango ya kumuona Mungu sawasawa na (Waebrania 12:14, na 1Yohana 4:7-8 ).
Kanisa ambalo, watu wake wanamwabudu Mungu watakavyo, wanawake na vijana wanavaa hohe hahe, wanaenda kanisani kama vile disco na hawaambiwi chochote, hawakemewi dhambi, hawaonywi..hilo sio kanisa hai.
5) Karama za Roho:
Alipo Roho Mtakatifu, atadhihirisha na uwepo wake pia, kama kanisa haliruhusu karama kama za uponyaji wa Roho, unabii, uinjilisti, lugha, maombi n.k. ni dalili kuwa hilo sio kanisa la Kristo.
Yapo ambayo yanaamini lakini hayahimizi, haya yanaweza yasiwe na shida..lakini yapo ambayo hayaamini kabisa kiasi kwamba lolote likitokea waweza fukuzwa kanisani..haya ndio uyakimbie, kabisa kwasababu yatakuua kiroho, ushindwe kumtumikia Mungu kwa karama aliyoiweka ndani yako.
1 Wakorintho 12:7-11
[7]Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.
[8]Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule;
[9]mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja;
[10]na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha;
[11]lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.
Hivyo kwa vigezo hivyo, naamini utakuwa umepata mwanga wa kujua kanisa la kweli ni lipi.
Hivyo chukulia kwa uzito suala hili, lipime kanisa lako, kwasababu wengi wameshafungwa katika kamba za makanisa ya uongo na bado wanaendelea nayo..Usiogope kutoka kwasababu atakayehukumiwa ni wewe sio hilo dhehebu.
Nikitakie uchaguzi mwema.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/01/31/je-ni-kanisa-lipi-sahihi-kumuabudia-mungu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.