Yohana Mbatizaji alibatiza watu kwa jina gani?.

by Admin | 12 March 2022 08:46 am03

Tunasoma Matendo 2:38, kuwa watu walibatizwa kwa jina la YESU. Lakini biblia haijataja Yohana Mbatizaji alitumia jina gani kumbatizia Bwana Yesu, Pamoja na makutano waliomjia ili awabatize?.


Jibu: Yohana Mbatizaji hakutumia jina lolote katika Ubatizo. Ubatizo wake ulikuwa ni ubatizo wa Toba, ambapo baada ya watu kusikia mahubiri yake na kutubu, aliwazamisha kwenye maji mengi kwa ishara ya kuoshwa dhambi zao kwa maji. (Hakuna jina lolote lililohusika).

Lakini baada ya Bwana Yesu kuja, maandiko yanasema mambo yote tunayafanya kwa jina lake (Jina la Yesu).

Wakolosai 3:17 “Na kila mfanyalo, KWA NENO au KWA TENDO, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye”.

Umeona hapo?.. anasema lolote lifanyikalo kwa “Neno” au kwa “Tendo”.

Mfano wa mambo yafanyikayo kwa neno, ni kuomba, kutoa pepo, kubariki, kuimba, kutoa unabii n.k Hayo yote tunayafanya kwa jina la YESU. Ndio maana leo Pepo linatoka kwa jina la Yesu, vile vile tunapoomba tunatumia jina la YESU, n.k Mambo haya hapo kabla hayakuwepo, kwamba pepo linamtoka mtu kwa kutaja tu jina la mtu Fulani!.. Lakini yamekuja kuwezekana kwa mmoja tu, ambaye ni Bwana YESU, kwa jina lake tunafanya yote!.

Lakini sio hilo tu, bali maandiko yanasema pia, lolote tufanyalo kwa TENDO. Sasa mfano wa tendo, ndio huo Ubatizo!.) Kwamba tunazamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU. Yohana hakutumia jina la Yesu, ndio maana ubatizo wake ukakoma, lakini ubatizo wa jina la Yesu umedumu siku zote!! Na ndio unaoondoa dhambi!.

Matendo 19:1 “Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko;

2 akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia.

3 AKAWAULIZA, BASI MLIBATIZWA KWA UBATIZO GANI? WAKASEMA, KWA UBATIZO WA YOHANA.

4 Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu

5 WALIPOSIKIA HAYA WAKABATIZWA KWA JINA LA BWANA YESU.

6 Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.”.

Umeona hapo?. Watu hao walirekebisha ubatizo wao, wakabatizwa tena kwa jina la BWANA YESU

Na sisi leo hii hatuna budi kubatizwa kwa jina la Bwana Yesu ili tupate ondoleo la dhambi.

Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu”.

Ubatizo ni nguzo muhimu sana na ya awali katika Ukristo, (Kila Mtu aliyemwamini Yesu ni lazima abatizwe). Na kumbuka lengo kuu la ubatizo sio wewe kupewa jina jipya. Hilo sio lengo la ubatizo, lengo la ubatizo ni kuzikwa kwa utu wako wa kale, na kufufuka katika upya.

Swali ni Je!  umebatizwa inavyopaswa kwa kuzamishwa na kwa jina la Bwana Yesu? Kama bado unasubiri nini?..Fanya hima ubatizwe ili uitimize haki yote!.na kumbuka pia ubatizo sio wa kunyunyiziwa wala wa uchangani, bali ni maji mengi! Na wa utu uzima.

Hivyo kama ulibatizwa pia utotoni, huna budi kubatizwa tena sasa, baada ya kujitambua, kwasababu wakati ule hukuwa umeokoka!, hukuwa umetubu..lakini sasa umejitambu, hivyo huna budi kubatizwa.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?

Je! Bwana Yesu alibatiza akiwa hapa duniani?

UMUHIMU WA KUBATIZWA.

UFUNUO: Mlango wa 1

Watu wajikatao ni watu wa namna gani? (Wafilipi3:1).

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/03/12/yohana-mbatizaji-alibatiza-watu-kwa-jina-gani/