WALA TUSIACHE KUKUSANYIKA PAMOJA

by Admin | 31 March 2022 08:46 pm03

Waebrania 10:25 “WALA TUSIACHE KUKUSANYIKA PAMOJA, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia”.

Kukusanyika kunakozungumziwa hapo, ni kukusanyika na wapendwa wengine kanisani.

Mbinu ya kwanza shetani anayoitumia kuwaangusha watu, ni kuwatoa katika kundi!..(kuwatenga na kundi), atanyanyua kisa tu , ambacho kitamfanya huyo mtu akereke na aache kwenda kanisani. Na yule mtu kwa kudhani kuwa “kujitenga na wenzake, ndio atakuwa salama, kumbe ndio kajimaliza”.

Vifuatavyo ni visa vichache ambavyo shetani anawahubiria watu, lengo ni kuwatoa ndani ya kundi.

 1. IBADA INACHUKUA MUDA MREFU.

Ukishaanza kuona au kusikia hii sauti ndani yako inayokuambia kuwa “ibada ndefu sana”..basi jua ni shetani anakuhubiria kutaka kukutoa katika kundi, kwasababu anaona kuna hasara unataka kumletea katika ufalme wake.

Siku zote fahamu kuwa siku ya Bwana, ni amri kuwa yote iwe takatifu.. Ni heri ukose ibada za katikati ya wiki, lakini ya Siku ya Jumapili, siku hiyo ifanye takatifu yote kwa Bwana!..ukijiwekea hilo akilini, hutababaishwa na masauti ya shetani yanayokuambia ibada ni ndefu sana.

 2. KUSIKIA HABARI ZA WATU WENGINE.

Wengi shetani anawatoa katika makusanyiko, kuwasikilizisha kwanza habari mbaya za watu wengine wanaoshiriki nao katika kusanyiko hilo, au viongozi wa kanisa hilo. Mara watasikia mshirika Fulani kagombana na mwingine, au Mchungaji haelewani na mtu Fulani, au kafanya hiki au kile..

Na kwasababu hiyo basi wanaamua kuacha kwenda kanisani, kukusanyika kama ilivyokuwa kawaida yao, na kuishia kukaa tu nyumbani…wakidhani kuwa nyumbani ndio wapo salama, pasipo kujua kuwa ni shetani ndio kawatoa kule.

Siku zote fahamu kuwa hakuna mahali patakosa kasoro…kasoro kila mahali zipo, na zitaendelea kuwepo, hivyo kazi mojawapo ya wewe kukuweka pale ni ili uwe sababu ya kuziondoa hizo, kwa kuomba na kuonya, na sio kwa kukimbia na kuacha…

 3. KUKWAZWA NA MTU/BAADHI YA WATU KATIKA KANISA.

Hii ni sababu nyingine shetani anayoitumia kuwatenga watu wengi na kundi!.. utaona mtu kaaambiwa au kafanyiwa jambo moja tu, ambalo ameliona kuwa sio zuri! Lakini utaona hilo hilo analitumia kama sababu ya kutokanyaga tena kanisani.. Lakini akila wali na kukuta kipande kidogo cha jiwe, hamwagi chakula chote!. Lakini kwa Mungu anakuwa ni mtu wa kususa vitu vidogo..

Kumbuka ijapokuwa tunaitwa wakristo, bado hatutakosa kasoro kabisa, mchungaji hawezi kuwa mkamilifu saa zote, muumini mwanzako hawezi kuwa Malaika.. hivyo viwango unavyovitaka uvione hutaviona katika kanisa lolote lile duniani, unachopaswa kufanya ni kuwa mvumilivu, na kuendelea kudumu pale ukiomba na kupambana kurekebisha hizo kasoro..ili hatimaye zipotee kabisa ndani ya kanisa na si kuondoka..

Ukiondoka na kuamua kubaki nyumbani tu!, jua ni shetani ndio kakutoa katika kundi, kwasababu ameona utakuja kumsumbua huko mbeleni.

 4. HOFU YA MATOLEO.

Ni kweli kuwa katika siku hizi za mwisho, watatokea watu wa kupenda fedha hata katika madhabahu za Bwana, lakini usiitumie hiyo kama sababu ya wewe kuacha kwenda kanisani..

Kwasababu hata kama ukihimizwa kutoa, kama kweli na wewe unampenda Bwana huwezi kuchukia.. kwasababu unajua kabisa kwamba unamtolea Mungu, na si mwanadamu.. na hivyo thawabu zako zinazidi kuongezeka tu mbinguni.

Ukisikiliza hubiri la shetani linalokuambia usiende kanisani kwasababu utaambiwa utoe hela, afadhali ukae nyumbani tu!, jua kuwa upo katika hatari kubwa sana..

Kuna faida nyingi za kukusanyika Pamoja, lakini leo tutazitama faida 2 tu!

 1. UNAKUWA IMARA KATIKA IMANI.

Unaweza kusema nikiwa peke yangu, ninaweza kusimama… lakini nataka nikuambia..mtu anayelala hajui dakika aliyoingia usingizini, vile vile mtu aliye pekee yake siku za kwanza atajiona nafuu lakini ndivyo anavyozidi kupoa kidogo kidogo na mwisho kupotea kabisa..

Hebu soma maneno haya…

Mhubiri 4:9 “Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao.

10 KWA MAANA WAKIANGUKA, MMOJA WAO ATAMWINUA MWENZAKE; LAKINI OLE WAKE ALIYE PEKE YAKE AANGUKAPO, WALA HANA MWINGINE WA KUMWINUA!

11Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto?

12 Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi”.

Hivyo usiache kamwe kukusanyika Pamoja na wengine, kwasababu kuna vitu ambavyo ukiwa peke yako inakuwa ni ngumu kuvipata, mfano wa vitu hivyo ni Faraja, ari, motisha, hamasa,.. Na vile vile kuna vitu ambavyo ukiwa peke yako ni ngumu kuvifanya kikamilifu.. Mfano wa vitu hivyo ni maombi!.. ukiwa mwenyewe nyumbani ni ngumu kukesha kuomba.. lakini ukiwa kwenye mkesha mahali ambapo watu wote wanaomba.. ukitazama kushoto Jirani anaomba, ukitazama kulia mwingine anaomba ni lazima na wewe utapata nguvu ya kuomba.. lakini nyumbani peke yako ni ngumu.

Hiyo ni hekima ya kiMungu, hivyo usijione unayo hekima kuliko Mungu..

Ndio maana utaona ni kwanini Bwana Yesu alikuwa anawatuma wanafunzi wake kwenda kuhubiri, wawili wawili.. na si mmoja mmoja, ni kwasababu alikuwa anajua madhara ya mtu kwenda peke yake.

Marko 6:7 “Akawaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu”

 2. UNAPATA BARAKA.

Kuna baraka mara dufu, ukiwa katika kanisa kuliko ukiwa nyumbani

Zipo baraka ambazo Mungu anaziachia kwa Watoto wake kwa umoja.. na hizo zinaachiliwa kanisani…Na baraka hizo ni za kiroho na kimwili..

Mathayo 18:18 “Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.

19 Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni.

20 Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao”.

Hapo Bwana Yesu hajasema.. “akikusanyika mmoja nyumbani kwake, atakuwa katikati yake”..sasa sio kwamba “kila unapokuwa peke yako Bwana anakuwa hayupo nawe” ..yupo na wewe lakini, si kama utakavyokuwa na wengine. Kwasababu Bwana siku zote anahubiri umoja na anapendezwa na umoja.. Lakini ukijitenga Bwana hawezi kupendezwa na wewe.

Mithal 18:1 “Ajitengaye na wenzake hutafuta matakwa yake mwenyewe; Hushindana na kila shauri jema”.

Hivyo mkatae leo shetani, na anza kwenda kukusanyika na wengine, hiyo ni kwa faida yako wewe, kumbuka siku zote kuwa shetani anafananisha na simba atafutaye mawindo..na anawawinda watu walioanza safari ya wokovu watu kwa njia nyingi, na ya kwanza ndio hiyo.. ya kuwatenda na kundi.

1 Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze”.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

UTAWALA WA MIAKA 1000.

KUOTA NYOKA.

TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI.

NI KIPI KINAMZUIA MUNGU KUZUNGUMZA NA SISI?

Kwanini Mungu awachome watu kwenye ziwa la moto na hali yeye ndiye aliyewaumba?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/03/31/wala-tusiache-kukusanyika-pamoja/