by Admin | 25 April 2022 08:46 am04
SWALI: Je ni kweli, mpagani akioa au akiolewa na yule aliyeamini, na yeye pia anahesabiwa kuwa mkamilifu kulingana na mstari huu?
1Wakorintho 7:13 Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe.
14 Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi; bali sasa ni watakatifu
JIBU: Ifahamike kuwa hakuna mtu anayehesabiwa mkamilifu kwa ukamilifu wa mtu mwingine. Maandiko yapo wazi katika hilo; yanasema kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe, na kila mtu atatoa Habari zake mwenyewe siku ile, mbele za Mungu (Wagalatia 6:5, Warumi 14:12).
Lakini je! Mstari huo unamaanisha kwamba ikiwa umeolewa au kuoa mtu aliyeamini, hata kama wewe ni mtenda dhambi utahesabiwa mtakatifu kwa yeye?na ukifa utaenda mbinguni? Jibu ni hapana, ukisoma vifungu vya chini yake kidogo utaelewa vizuri..Tusome..
1Wakorintho 7:12 “Lakini watu wengine nawaambia mimi, wala si Bwana, ya kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke huyo anakubali kukaa naye asimwache.
13 Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe.
14 Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi; bali sasa ni watakatifu.
15 Lakini yule asiyeamini akiondoka, na aondoke. Hapo huyo ndugu mume au ndugu mke hafungiki. Lakini Mungu ametuita katika amani.
16 KWA MAANA WAJUAJE, WEWE MWANAMKE, KAMA UTAMWOKOA MUMEO? AU WAJUAJE, WEWE MWANAMUME, KAMA UTAMWOKOA MKEO”?
Paulo anamaanisha kwamba, ikiwa wewe umeamini, na mwezi wako hajaamini, hupaswi kumuacha na kwenda kuoa/kuolewa na mwingine. Bali unapaswa kuendelea kuishi naye ikiwa tu bado yupo radhi kuwa nawe. Kwasababu kwa kufanya hivyo ni rahisi yeye kuvutwa kwenye Imani yako, ikiwa ataona mwenendo wako mzuri,.. Na kwa matokeo hayo Paulo anasema ni nani ajuaje na yeye atashawishwa kuokoka kama wewe?
Na ni kweli ukisikiliza shuhuda za ndoa nyingi zilivyomrudia Mungu, utasikia moja inakuambia Baba aliokoka baada ya mkewe kuwa mcha Mungu, au mama alimrudia Mungu baada ya mumewe kuokoka. Umeona? Lakini hilo haimaanishi kuwa moja kwa moja ndio tayari na yeye kaokoka,kisa tu mwenzake kaokoka hata kama ataendelea kutenda dhambi, hapana.
Wanaweza wakakaa hivyo, na bado mmoja akaendelea kutokuamini hadi kifo na kuzimu akaenda. Lakini hiyo nayo hutokea mara chache, ikiwa kweli huyo mwenzi mwingine, anaishi Maisha ya haki, na ya kumpendeza Mungu, na ya kumwombea kwa bidii mwenzake.
Lakini pia ni lazima tufahamu kuwa biblia hairuhusu, mkristo kuoa/kuolewa na mtu asiyeamini. Mazingira yanayozungumziwa hapo, ni yale ambayo wokovu umemkuta tayari yupo kwenye ndoa ya namna hiyo. Leo hii kumekuwa na migogoro mingi ya kindoa, kwasababu ya maamuzi mabaya, yanayofanywa na wakristo, ambao hawazingatii maagizo ya Mungu yaliyosema tusifungwe nira Pamoja na wasioamini (2Wakorintho 6:14).
Ulinzi wa kwanza unapaswa uwe katika Imani yako, sio katika familia. Hivyo ikiwa bado hujaoa/ au hujaolewa, Imani ndio iwe ni kipimo cha kwanza cha kumtambua mwenzi sahihi. Lakini wewe ambaye tayari upo kwenye ndoa ya namna hiyo. Unalojukumu la kumvuta huyo mwenzi wako, kimatendo, kimaombi, na kimafundisho. Kwasababu huwezi jua kama atavutwa au la!.
Bwana akubariki
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 2: Upande wa wanawake)
Je! Ni halali kuoa/kuolewa na mtu ambaye tayari anao watoto?
Nini Tofauti kati ya uzinzi na uasherati ?
JE NI DHAMBI KUWA NA MAHUSIANO KABLA YA NDOA?
NJIA SAHIHI YA KUMPATA MWENZA WA MAISHA KIBIBLIA.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/04/25/kwa-maana-yule-mume-asiyeamini-hutakaswa-katika-mkewe/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.