by Admin | 13 July 2022 08:46 am07
Mwana-haramu, au mwana wa haramu ni mtu aliyezaliwa nje ya Ndo Takatifu.
Zamani katika jamii ya Israeli, Mungu aliwakataza wana wa Israeli, wasioane na watu wa mataifa. (Kumbukumbu 7:2-3). Wala wasioane ndugu kwa ndugu..
Walawi 18:5 “Kwa ajili ya hayo mtazishika amri zangu na hukumu zangu; ambazo mtu akizitumia ataishi kwa hizo; mimi ndimi Bwana.
6 Mtu ye yote aliye wa kwenu ASIMKARIBIE MWENZIWE ALIYE WA JAMAA YAKE YA KARIBU ili kumfunua utupu; mimi ndimi Bwana”.
Vile vile Bwana aliwakataza watu wasiingie kwa wake wa Jirani zao (Kumbukumbu 5:21, Kutoka 20:17).
Kwahiyo mtoto yeyote aliyepatikana kwa mojawapo ya hizo njia tatu, yaani kwa njia ya kukutana ndugu kwa ndugu, au kuoana mtu wa Israeli na mtu wa mataifa, au kwa kuzaa na mke wa Jirani yako au ambaye hamjaoana, mfano wa Yuda katika Mwanzo 38:24. Mtoto huyo aliyezaliwa aliitwa MWANA-HARAMU, Au MWANA WA HARAMU.
Na Mwana haramu, enzi za agano la kale hakuruhusiwa kuingia katika MKUTANO WA BWANA MILELE, na hata kizazi chake chote..
Kumbukumbu 23:2 “Mwana wa haramu asiingie katika mkutano wa Bwana; hata kizazi cha kumi asiingie aliye wake katika mkutano wa Bwana”.
Lakini swali ni je! Mpaka sasa, wana wa Haramu,(yaani waliozaliwa nje ya ndoa, kimwili) hawakubaliwi na Bwana?
Jibu ni la!, katika Agano la kale, si tu wana haramu waliokuwa wanatengwa, bali hata walemavu na watu wenye ukoma, hawakuruhusiwa kuingia katika mkutaniko wa Bwana. Na Bwana aliruhusu vile, ili kufundisha Uana haramu wa kiroho jinsi ulivyo mbaya, ambao utakuja kufunuliwa mbeleni(katika Agano jipya). Ambao huo utatufanya sisi tusikubalike mbele za Mungu, milele!!.
Mwana wa Haramu kibiblia ni mtu ambaye Hajazaliwa mara ya Pili.
Je umewahi kujiuliza ni kwanini “Wokovu” unafananishwa na “kuzaliwa mara ya pili”.. jiulize kwanini biblia haijatumia neno “kutengenezwa upya” lakini imetumia neno “kuzaliwa mara ya pili”.. Tafsiri yake ni kwamba “hali tuliyopo” sasa ni “u-haramu”… hivyo tunapozaliwa upya, ili ule uharamu unaondoka, na kuwa wana HALALI!!.. Na hivyo tunakuwa na uwezo wa kushiriki baraka zote za Mungu kwasababu tumefanyika kuwa Watoto wa Mungu halali.
Wana wa Haramu, (ambao hawajazaliwa mara ya pili), wanafananishwa na mbegu zinazoharibika.. maana yake!, hazina uzima wa milele, lakini wana halali (yaani wale waliozaliwa mara ya pili), wanafananishwa na mbegu zidumuzo.
1Petro 1:23 “Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele”.
Na tabia ya mtoto halali, (asiye haramu), huwa baba yake anamfunza, ikiwemo pia kumwadhibu pale anapokosea..
Mtume Paulo aliliandika hilo kwa uweza wa roho na kusema…
Waebrania 12.5 “tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye;
6 Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye.
7 Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye?
8 Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo MMEKUWA WANA WA HARAMU NINYI, WALA SI WANA WA HALALI.
9 Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi?
10 Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake.
11 Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani”.
Je umezaliwa mara ya pili?
Maana ya kuzaliwa mara ya pili, ni Kutubu kwa kumaanisha kuacha dhambi, na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi (Kwa jina la Yesu) na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu. (Matendo 2:38).
Yohana 3:3 “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, MTU ASIPOZALIWA MARA YA PILI, HAWEZI KUUONA UFALME WA MUNGU.
4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?
5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.
6 Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.
7 Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili”.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
AMEFANYIKA BORA KUPITA MALAIKA!
TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!
KWANINI YESU NI ADAMU WA PILI?
Hema ya kukutania ni nini, na ilikuwaje?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/07/13/mwana-haramu-ni-nani-kibiblia-kumbukumbu-232/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.