Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake

by Admin | 13 September 2022 08:46 am09

SWALI: Biblia inaposema “Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake”, ina maana gani?

Isaya 53:5 “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona”.


JIBU: Ili kuelewa neno hilo, wazia mfano huu; Mtu mmoja ameshitakiwa na mahakama kwa kosa la uchafuzi wa mazingira, hivyo, akapewa adhabu ya kulipa faini ya sh. Milioni 5 ndani ya wiki 3, au jela miaka 3. Sasa ikatokea mtu huyu akawa hana cha kulipa,.. Unadhani atakuwa katika hali gani? Ni wazi kuwa atapoteza amani yote, hawezi kuwa katika furaha, hawezi kuwa katika raha wakati wote huo kwasababu anajua hukumu ya kifungo ipo mbele.. Ili amani yake irudi, hana budi apate kiwango hicho alipe. Lakini akatokea mtu, akasema mimi nitakuchukua adhabu hiyo nitamlipia deni lake. Bila shaka furaha na amani ya yule mdaiwa itarejea tena.

Hivyo tunaweza kusema, ili kuirejesha ile amani yake ya mwanzo, alikuwa hana budi kutumikia adhabu kwanza..

Sasa tukirudi katika huo mstari ..biblia inaposema;

Isaya 53:5 “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona”.

Huyo ni Bwana Yesu anayezungumziwa hapo, sasa anaposema, Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona”. Ni kwamba ili sisi kuipokea Amani yetu, tuliyoipoteza tangu kule edeni, ilitupasa kwanza tutumikie adhabu ya makosa.. Lakini ashukuruwe Kristo kwasababu alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, akapigwa na kuteswa ili sisi tupone. Adhabu ya amani yetu aliichukua yeye.

Na ndio maana Warumi 8:1 inasema; “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu”.

Ukiwa ndani yake, amani yako inarejeshwa bila kulipa gharama yoyote. Lakini inastaajabisha kuona bado wapo watu hawataki kulipiwa deni zao. Wakidhani kuwa wataweza kustahimili hukumu ya Mungu siku ile. Ndugu ikiwa upo nje ya Kristo huna tumaini lolote. Ukifa ni moja kwa moja jehanamu kwenye ziwa la moto. Adhabu yako ni Mauti katika lile ziwa la moto milele.

Hiyo ndio sababu kwanini unamuhitaji Yesu Kristo leo, kwasababu ukishakufa leo hakuna tumaini, wala huna matendo yoyote ya kumshawishi Mungu, afute dhambi zako. Wasubiri nini, usimgeukie Bwana Yesu akusafishe Maisha yako angali ukiwa hai? Tubu sasa mpokee yeye. Muda ni mchache.

Maran Atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

KAMA SI YESU, HABARI YETU INGEKUWA IMEISHA ZAMANI SANA.

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

Je Mungu ana njia ngapi za kuzungumza?

Sadaka ya Amani ilikuwaje?

Tofauti kati ya mbinguni, peponi, Kuzimu, Jehanamu, na Paradiso ni ipi?

Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/09/13/adhabu-ya-amani-yetu-ilikuwa-juu-yake/