by Admin | 8 November 2022 08:46 pm11
Swali: Katika Ufunuo 22:16, tunasoma ile nyota inamwakilisha Bwana Yesu, lakini tukirudi katika Isaya 14:12, tunasoma ile nyota inamwakilisha shetani, hapa imekaaje?
Jibu: Tusome..
Ufunuo 22:16 “Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi”.
Tusome tena..
Isaya 14:12 “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa”
Kwa haraka ni rahisi kufikiri au kutafsiri kuwa hiyo ni nyota ile ile moja inayozungumziwa hapo, lakini ki uhalisia sio nyota moja bali ni nyota mbili tofauti, isipokuwa zote ni nyota za asubuhi.
Sasa tofauti ya nyota hizi mbili ni ipi?.
1.MAJIRA
Nyota inayotajwa katika Ufunuo 22:16 ambayo inamwakilisha Bwana Yesu inatajwa kama Nyota ya asubuhi, lakini ile ya Isaya 14:22 ambayo inamwakilisha shetani inatajwa kama ni nyota ya alfajiri. SASA ALFAJIRI na ASUBUHI, ni majira mawili tofauti.
Alfajiri ni mapema zaidi kuliko asubuhi, alfajiri inaanza saa 10 usiku mpaka saa 12 na asubuhi inaanza saa 12 mpaka saa Tano na dakika 59.
Sasa hapo biblia inaposema shetani ni nyota ya alfajiri maana yake ni kuwa nyota hiyo inaonekana alfajiri tu wakati wa giza na kukisha pambazuka inapotea lakini hiyo nyingine ambayo inamwakilisha Bwana Yesu ni Nyota ya asubuhi maana yake ni kuwa wakati kunapopambazuka na ile nyota ya alfajiri inapopotea kutokana na mwanga wa jua, hii nyota ya asubuhi bado itakuwa inaendelea kuangaza..
Sasa kama wewe ni mtu wa kupenda kuchunguza anga, utakuwa umegundua kuwa kunakuwepo na nyota moja asubuhi ambayo wakati nyota nyingine zimeshapotea yenyewe bado inaangaza.. Sasa nyota hiyo ndiyo inayomwakilisha Bwana Yesu, na ndio nyota ya asubuhi.
Na sifa nyingine ya hii nyota ya asubuhi, huwa pia ndio ile ile ya jioni, wakati ambapo nyota nyingine bado hazijatokeza kutokana na mwanga wa jua, hii ya asubuhi ndio inakuwa ya kwanza kutokeza..hiyo ikifunua tabia nyingine ya Bwana Yesu kuwa yeye ndiye MWANZO na MWISHO. (Alfa na Omega, Ufunuo 22:13).
Sasa kwa mapana na marefu kuhusu hii nyota ya asubuhi, na tabia zake kwa undani unaweza kufungua hapa >>> NYOTA YA ASUBUHI
Sababu hii ya majira itatupeleka moja kwa moja kuelewa tofauti nyingine inayofuata ya nyota hizi mbili.
2. MNG’AO
Nyota inayotajwa katika Ufunuo 22:16, ambayo inamwakilisha Bwana Yesu Kristo inatajwa kama ni nyota yenye KUNG’AA Lakini inayozungumziwa katika Isaya 14:12 haitajwi kama inang’aa, ni kama nyota nyingine tu ambazo zinaangaza usiku…lakini ya asubuhi haing’ai..maana yake kukisha pambazuka basi yenyewe inaisha nguvu, lakini nyota ya Bwana Yesu inang’aa katika giza na vile vile katika Nuru. Na hata mchana kwasababu ya ukamilifu wa Mkuu wa uzima Yesu.
Mithali 4:18 “Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing’aayo, Ikizidi kung’aa hata mchana mkamilifu.
Je umemtumainia Yesu aliye Nuru ya kweli, ambayo wakati wa mchana atakuwa nawe na wakati wa usiku utamwona?.
Shetani ni nyota inayoangaza kwa nuru ya uongo ndio maana haitajwi kama ni nyota ing’aayo (Soma 2Wakorintho 11:14), na inayopotosha, na inayoangusha wengi kama maandiko yanavyosema hapo katika Isaya 14:12.
Hivyo Kama bado hujampokea Yesu mpokee leo, na unampokea kwa kuamini kuwa yeye ni Bwana na alikuja kufa kwaajili ya dhambi zako na kukiri kwa kinywa chako, na kuungama dhambi zako zote kwa kumaanisha kutorudia tena kuzifanya.
Na baada ya hapo kutafuta ubatizo sahihi ambao ni kwa jina la Bwana Yesu Kristo na kwa maji mengi (Matendo 2:38),
Na baada ya hapo Roho Mtakatifu atakuongoza na kukutia katika kweli yote ya maandiko.
Maran atha!.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Miungu wasio na kikao pamoja na wenye mwili.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/11/08/je-ile-nyota-ya-asubuhi-inamwakilisha-shetani-au-bwana-yesu/
Copyright ©2025 unless otherwise noted.