MIGAWANYO MINNE (4), YA HUDUMA YA YESU.

by Admin | 28 December 2022 08:46 am12

1.) DUNIANI (miaka 33 na nusu)

2) KUZIMU (Siku tatu)

3) MBINGUNI (Miaka elfu mbili na …)

4) DUNIANI TENA (Miaka 1000)

Ni vema tukaifahamu hii migawanyo kwa kina ili tujue huduma ya Bwana wetu Yesu sasa ni ipi kwa watu wake.

1.DUNIANI (miaka 33 na nusu):

 Bwana aliposhuka duniani, aliishi miaka thelathini na tatu na nusu, ndani ya miaka hii alikuwa na lengo la kuwafundisha na  kuwakomboa wanadamu wote kutoka katika laana ya dhambi na mauti. Na siku ile alipokwenda msalabani, ndipo akakamilisha kusudi hili. Ndio pale aliposema IMEKWISHA. Akiwa na maana  kuwa kuanzia huo wakati na kuendekea kila mwanadamu atakayemwamini yeye ni lazima aokolewe.

Kusudi lake la kwanza likawa limekwisha.

2) KUZIMU (Siku tatu):

Kusudi la pili lilikuwa ni kuzimu.  

Pindi tu alipokufa hakwenda mbinguni moja kwa moja bali alishuka kuzimu. Kuzimu ni mahali pa wafu. Hivyo zamani wafu wote waliokuwa wema na waovu, wote walikuwa wapo makaburini, isipokuwa waovu walitengwa mahali pao mbali na wema. Waovu walikuwa katika vifungo vya hukumu. Lakini wema walikuwa sehema salama. 

Sasa Bwana Yesu aliposhuka kuzimu, alifanya huduma kwa makundi yote mawili. Kwamfano lile Kundi la waovu alikwenda kulihubiria makosa yao, ni kwanini wamestahili hukumu, Soma..

1Petro 3:19 “ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri;

20 watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji”.

Maana yake ni kuwa hata sasa, ikiwa utakufa katika dhambi, ni moja kwa moja utakwenda huku wafu hawa walipo ambapo hapana raha, ndio Jehanamu yenyewe iliyopo chini ya dunia.

 Lakini  walio wema Bwana Yesu aliwachukua na kuwafungua kutoka katika vifungo vya kaburi, na kuwahamishia mahali pazuri sana  pajulikanapo kama peponi.

Mathayo 27:50 “Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.

51 Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;

52 makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala;”

Hivyo ikiwa wewe ni mtakatifu ukifa sasa, hutajiona ukishuka makaburini, bali utajiona ukichukuliwa juu, mbinguni. Lakini sio kule Kristo alipokwenda,(huko tutafika baadaye) bali katika mbingu ya katikati, ambayo hiyo utakaa huku ukisubiria ule ukombozi wa miili yetu, Siku ile ya Unyakuo. Ambapo kwa pamoja utaungana na watakatifu walio hai, na moja kwa moja kwenda mbinguni kule Kristo alipo kwenye karama ya mwana-kondoo. Hivyo hudumu hii ya Yesu iliishia pale siku ile alipofufuka.(1Wakorintho 15:51-55)

  1. 3) MBINGUNI (Miaka elfu mbili na …)

Hii ndio huduma ambayo mpaka sasa inaendelea ya mwokozi wetu. Alisema mwenyewe maneno haya..

Yohana 14:1 “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.

2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.

3 Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo”.

Mpaka anasema ninakwenda kuwaandalia makao, maana yake ni kuwa hapo kabla sisi hatukuwa na makao yoyote mbinguni. Hivyo makao haya ndio ile Yerusalemu mpya, ambayo itashuka kutoka kwa Mungu mbinguni, baada ya utawala wa miaka 1000 kuisha.

Haya ni makao ya milele, hivyo hatushangai ni kwanini hadi sasa Bwana anatuandalia. Bwana atusaidie tusiikose ile mbingu mpya na nchi mpya ambayo Yerusalemu mpya ipo ndani yake. Ni makao ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia. Huko tutamashangaa Mungu sana, kwa kipindi kisichokuwa na mwisho.

Huu ndio wakati wa ule utawala wa miaka elfu moja, ambao Kristo atakuja kutawala na watakatifu wake, hapa duniani, ndio kule kurudi kwa pili kwa Yesu Duniani, akiwa kama Mfalme wa wafalme, na Bwana wa Mabwana.  Ni wakati wa sabato ya watakatifu wote. Utajiuliza kulikuwa na umuhimu gani Mungu kuipitisha kwanza hii miaka 1000, na sio tuingie moja kwa moja kwenye Yerusalemu yake iliyo ndani ya mbingu mpya na nchi mpya?

Ni kwasababu Bwana anataka kuwahakikishia watu wake kuwa hakuna chochote walichokipoteza pindi walipokuwa wanataabika kwa ajili yake hapa duniani, pindi walipojikana, kwa kuacha kila kitu, na kudharauliwa,.hivyo ili kuwaonyesha hakuna walichokipoteza, atawarudishia hiyo miaka ya raha, na wenyewe watakuwa wafalme na Mabwana duniani. Wakati huo dunia haitakuwa kama hii tena, bali itarejezwa hata zaidi ya Edeni, na amani itakuwepo duniani.(Soma Ufunuo 20:1-4). Watatawala pamojanna Kristo kwa amani na furaha isiyoelezeka.

Ndugu, tukiyaona haya, tunatambua sasa wakati tuliobakiwa nao ni mchache sana. Siku yoyote unyakuo utapitia, mlango wa neema utafungwa, dalili zote zimeshatimia Jiulize Je, umejiandaaje? Au umejiwekaje tayari kumpokea Bwana Yesu. Na hata kama hatarudi wakati wako. Ukifa leo hii, huko uendako utakuwa ni mgeni wa nani?

Yesu yupo mlangoni kurudi, tubu dhambi zako ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO, upate ondoleo la dhambi zako. Hizi ni siku za mwisho. Tunachokisubiri sasa ni unyakuo tu, dalili zote zimeshatimia.

Maran Atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 3)

Je mbinguni itakuwa ni kuimba tu wakati wote?.

KWANINI KUWE NA UTAWALA WA MIAKA 1000

MAUMIVU  NYUMA-YA-HUDUMA.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/12/28/migawanyo-minne-ya-huduma-ya-yesu/