HAKUONA MAHALI PA KUTUA KWA WAYO WA MGUU WAKE.

by Admin | 20 January 2023 08:46 am01

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze biblia, Neno La Mungu wetu.

Mwanzo 8:6 “Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya; 

7 akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huko na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi.

 8 Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi; 

9 bali YULE NJIWA HAKUONA MAHALI PA KUTUA KWA WAYO WA MGUU WAKE, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani”

Tunaona wakati wa Nuhu kutoka safinani… Aliwaachia ndege wawili ili kupima hali ya mazingira ya nje. Na ndege wa kwanza ambaye ni “KUNGURU” aliondoka lakini hakumrudia Nuhu.. lakini ndege wa pili ambaye ni “NJIWA” Alipoondoka na kukuta nje maji yamejaa kila mahali, alirudi safinani..

Sasa ni kwanini Njiwa arudi na kunguru asirudi?.

Siri ipo katika ile sura ya Saba, kuhusiana na wanyama Najisi na wasio Najisi.

Mwanzo 7:1 “Bwana akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki.

 2 Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, mume na mke; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mume na mke. 

3 Tena katika ndege wa angani saba saba, mume na mke; ili kuhifadhi hai mbegu juu ya uso wa nchi yote”

Sasa Kunguru yupo katika kundi la Ndege Najisi,

Walawi 11:13 “Kisha katika ndege hawa watakuwa ni machukizo kwenu; hawataliwa, ndio machukizo; tai, na furukombe, na kipungu;

14 na mwewe, na kozi kwa aina zake,

15 na kila kunguru kwa aina zake”

Na njiwa yupo katika kundi la ndege Safi (yaani wasio najisi) ndio maana alikuwa anatumika katika matoleo.

Sasa tabia ya ndege/wanyama najisi ni za tofauti na zile za wasio najisi. Wanyama najisi wanakula chochote na wanaweza kuishi popote.. lakini Wanyama/ndege wasio najisi wanachagua vitu vya kula, vile vile wanachagua mazingira ya kuishi, si kila mahali wanaweza kuishi.

Ndio maana tunaona huyu kunguru alipoachiwa, alienda kuzunguka zunguka huko nje, lakini njiwa aliona mazingira ya nje si salama, bado wakati wake, na hatimaye akarudi safinani.

Sasa wanyama najisi kiroho wanafananishwa na watu wa ulimwengu huu, walio mbali na MUNGU, na wanyama Safi (yaani wasio najisi) wanafananishwa na watu wa Mungu, waliookolewa kwa damu ya thamani ya YESU KRISTO, ambao hawajitii unajisi na mambo ya dunia.

Kama vile njiwa alivyozunguka huko na huko na kuona safinani ni mahali salama katika dunia iliyoharibika.. vile vile watu wa Mungu, kamwe hawawezi kuona hii dunia ipo salama, au ni mahali pa kustarehe kuliko safinani. Na safina ni BWANA YESU!.

Ukiona unaifurahia dunia iliyochafuka, dunia iliyojaa anasa, dunia iliyo mabaya basi katika roho wewe ni najisi.. Ukiona unaufurahia uasherati, ulevi, wizi unaoendelea duniani, na hata wewe mwenyewe kuwa mshirika wa hayo, basi fahamu kuwa unafanana na Yule kunguru! Na hivyo ni najisi mbele za Mungu kulingana na biblia.

Mathayo 15:18 “….vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi.

19  Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano;

20  hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi…”

Je! wewe ni miongoni mwa walio najisi au safi? Kama bado dhambi inatawala maisha yako basi upo hatarini hivyo suluhisho ni kumgeukia Yesu kwa kutubu na kumaanisha kuacha dhambi, na Yesu atakupokea na kukupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu, ambaye kupitia huyo atakutakasa kwa kukupa uwezo wa kufanya yale mema ambayo ulikuwa unashindwa kuyafanya kwa nguvu zako.

Kataa ukunguru!

Bwana akubariki

maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Kwanini Mungu aliwaita Adamu na Hawa jina moja?

JIHADHARI NA ROHO ZIDANGANYAZO.

Je mwanamke anaruhusiwa kupanda madhabahuni akiwa katika siku zake?

Mahali pa juu palikuwa ni wapi kama tunavyosoma katika biblia?

HUJAPEWA MBAWA ZA KUKIMBIA MATATIZO

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/01/20/hakuona-mahali-pa-kutua-kwa-wayo-wa-mguu-wake/