KAMA MTUMISHI WA MUNGU, TAFUTA MAARIFA KWA BIDII.

by Admin | 9 March 2023 08:46 am03

Huu ni mfululizo wa Masomo maalumu kwa Watumishi wa Mungu (Wahubiri wa Injili, Wachungaji, Wainjilisti, Waalimu, Manabii na Waimbaji wote).

Hosea 4:6 “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako”.

Tunaona hapa Bwana anaanza  kama kwa kulaumu!.. sasa anamlaumu nani? Si wana wa Israeli bali anawalaumu  MAKUHANI wake! (Yaani watu waliowekwa kwa lengo la kuwafundisha wana wa Israeli njia ya kumcha Bwana)… ambao kwasasa wanafananishwa na (Wachungaji, Wainjilisti, Waalimu, Mitume, Manabii na wahubiri wote)

Watu hawa Bwana anawalaumu kwa kuwa “wameyakataa maarifa” (maana yake hawataki kujishughulisha kutafuta maarifa yatakayowasaidia wao pamoja na wengine), na hivyo kusababisha Israeli yote kukosa maarifa.. kwasababu laiti wakiyapata maarifa hayo ya kiMungu ya kutosha, basi wangeweza kuwafundisha Israeli nzima na hivyo Israeli yote ingeponyeka..

Lakini kinyume chake, Makuhani hawa hawayataki maarifa!, wanaridhika kukaa katika ujinga, hawataki kusoma maandiko,  na hivyo kusababisha Israeli yote kukosa maarifa na kuangamia, jambo ambalo ni DHAMBI KUBWA SANA MBELE ZA MUNGU!, Kwasababu wao ndio chanzo cha Israeli yote kukosa maarifa..

Na tunaona madhara yake ni nini… Bwana AKAWAKATAA wasiendelee kuwa makuhani, na akawakataa na WATOTO WAO pia.

Ni jambo baya sana, Bwana kukukataa kuwa KUHANI.. kwani unakuwa Umenyang’anywa Neema yote iliyokuwa juu yako.. utalazimisha kuendelea na Mungu, lakini yeye atakuwa yupo mbali na wewe kama ilivyokuwa kwa Sauli..

1Samweli 15:23 “Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme”

Hili ni jambo baya sana na linaloendelea sasa miongoni mwa watumishi.. Ni heri tukataliwe na wanadamu wote, lakini tusikataliwe na Mungu..

Kama mtumishi wa Mungu tafuta maarifa!!!… kwasababu utumishi wako unapimwa!.. Bwana anategemea kuona watu wake wanajaa maarifa ya kumjua yeye pindi wanapokuja katika kanisa unalohudumu, wanapokuja katika maskani unayo hudumu…. hataki kuona watu wake wanaangamizwa kwa kukosa maarifa, ili hali wewe (unayejiita mtumishi wa Mungu) ndiye ambaye ungepaswa uwape hayo maarifa.!

Bwana akiona watu wake wanaangamia kwa kukosa maarifa, usidhani wewe utabaki salama!.. Bwana atakukataa wewe na pia atawakataa watoto wako..

Usifurahie kuona watu walio chini yako, hawaelewi kanuni ya Imani, wanatanga tanga huku na kule kutafuta  maji, au mafuta au kuufananisha ukristo na uganga wa kienyeji…

Chukua jukumu la kujifunza biblia kwa kina ili ujae maarifa yatakayokusaidia wewe na ukawasaidie na watu wako!!!!!…soma, tafiti, chunguza maandiko kila siku, hakiki mambo yote, acha kutafuta umaarufu na sifa zisizokuwa na maaana kutoka kwa watu wako…. hiyo itathaminisha utumishi wako mbele za Mungu.. wape watu Maarifa ya kiMungu, hayo ndiyo yatakayowalinda wasije wakaangamia!… Kumbuka siku zote kuwa Bwana hataki watu wake waangamizwe kwa kuyakosa hayo!.

Kama unaona uvivu kutafuta maarifa na kuwapa watu hayo, acha hiyo kazi ya kuhubiri, sio wito wako!, nenda katafuta kazi nyingine, kafanye biashara na Mungu atakubariki huko!, lakini usiwaongoze watu katika njia ya upotevu, kwa kuwajaza elimu za mambo ya ulimwengu huu na elimu za kichawi badala ya kuwapa elimu na maarifa ya ufalme wa mbinguni.. utajitafutia laana badala ya Baraka!.

Bwana Yesu na atusaidie sana.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

TAFUTA KWA BIDII KUWA MTAKATIFU.

NJAA ILIYOPO SASA.

Je! Mungu anaupendeleo kwa wanaume zaidi ya wanawake?

UFANYE WEMA WAKO KATIKA MAARIFA.

Tofauti kati ya Hekima, ufahamu na maarifa, ni ipi?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/03/09/kama-mtumishi-wa-mungu-tafuta-maarifa-kwa-bidii/