UFANYE WEMA WAKO KATIKA MAARIFA.

UFANYE WEMA WAKO KATIKA MAARIFA.

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, Karibu tujifunze biblia..

2Petro 1:5 “Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, NA KATIKA WEMA WENU MAARIFA”

Wema usiokuwa na Maarifa bado haujakamilika.. Ni kweli unaweza kufanya Wema na nia yako ikawa ni njema, lakini wema huo usipoufanya katika maarifa, huenda ukakuletea madhara hata wewe mwenyewe uliofanya huo wema.

Hebu tuangalie mtu mmoja katika biblia ambaye aliufanya wema wake katika maarifa yote, na huyo si mwingine zaidi ya Yule Msamaria-mwema.

Hebu tusome habari yake na kisha tutafakari…

Luka 10: 30 “ Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa.

31  Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando.

32  Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando.

33  Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia,

34  akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza.

35  Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa”

Tunaona Msamaria huyu alipopita njiani na kukuta mtu kalala kando, hakukurupuka  na kumpeleka nyumbani kwake, akalale na watoto wake au ndugu zake.. Badala yake alimchukua na kumpeleka katika nyumba ya kulala wageni (yaani Guest-house), na akiwa huko huenda aliendelea na hatua nyingine za kuripoti habari yake katika vyombo vilivyohusika, ili kama ikiwezekana apate msaada zaidi wa kuwapata watu wa nyumbani kwake.

Sasa kwanini hakumpeleka nyumbani kwake moja kwa moja?, si kwasababu hakuwa na huo uwezo, au labda ni mbali.. La! Bali ni kwasababu alitumia maarifa katika Wema wake, kwasababu Yule mtu alikuwa hamjui, hivyo kumchukua na kumpeleka nyumbani moja kwa moja, ingeweza kuwa hatari kwasababu huenda akafa, na matatizo yakawa kwa Yule aliyemsaidia, au huenda si mtu mzuri wakati wa kulala usiku akapata nafuu na kuamka na kumdhuru Yule aliyemsaidia.

Hivyo suluhisho la akili na hekima si kumpeleka nyumbani, bali katika nyumba ya kulala wageni.

Hali kadhalika na sisi tunapaswa tufanye wema wetu katika MAARIFA.. Si kila anayehitaji msaada basi ni wa kumpatia kile anachokihitaji yeye, bali tunapaswa tupime namna ya kumsaidia katika maarifa..

1 . Mtu  usiyemjua akikuomba fedha ya hitaji Fulani, ni vizuri usimpe hiyo fedha bali ukamnunulia hilo hitaji lake na kumpatia.

2. Ukimkuta mtu usiyemjua yupo katika hali ya kuhitaji msaada wa kimalazi.. usimchukue moja kwa moja na kumpeleka kwako, jitahidi umtafutie mahali pa kulala hususani kama gesti, angalau kwa siku moja, huku unaendelea kufuatilia taarifa zake na kuziripoti, na ukishajiridhisha vya kutosha ndipo umwamishie kwako.

3. Mtu usiyemjua akikuomba nguo, kama una uwezo basi mnunulie yake mpya, lakini usiitoe ile ya mwilini mwako na kumpatia, kwasababu shetani anaweza kuitumia hiyo kama mlango wa kukuletea matatizo maishani mwako. Lakini kama mtu unamjua au umejiridhisha kabisa kuwa ni mhitaji asiye na tashwishi basi waweza kumpa moja kwa moja nguo inayotoka moja kwa moja.

4. Mtu usiyemjua akikuomba Lift ya gari, au pikipiki, au baiskeli..kama una uwezo mlipie nauli apande katika chombo kingine, kwasababu humjui mtu huyo ni nani, na hivyo ni rahisi kutumiwa na adui kuleta dhara lolote lile.

5. Mtu usiyemjua akikuomba chakula kutoka katika sahani yako, usimpe kile chakula, badala yake mnunulie cha kwake binafsi, (sio uchoyo kufanya hivyo, bali ni hekima) kwasababu shetani anaweza kumtumia kama chombo cha kukuletea matatizo, kwasababu unaweza kumpa na kumbe kile chakula hakiendani na mwili wake, hivyo kikamletea madhara au hata kifo, jambo ambalo linaweza kutafsirika kwamba umemwekea sumu au dhara lolote, na kukuingiza wewe matatizoni pasipo sababu yoyote, hivyo ni lazima katika WEMA wako uweke na maarifa. (Kumbuka usiache kutenda wema, bali utende katika maarifa).

Na mambo mengine yote mema unayoyafanya kwa Mtu au watu, hakikisha unayafanya katika maarifa yote, ndivyo biblia inavyotufundisha.

2Petro 1:5 “Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, NA KATIKA WEMA WENU MAARIFA

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

AINA SABA (7) ZA UNAFIKI, AMBAZO UNAPASWA UJIEPUSHE NAZO.

Je! Wana wenu huwatoa kwa nani? maana yake ni nini?

Tofauti kati ya Hekima, ufahamu na maarifa, ni ipi?

Nuru yetu inapaswa iangaze au isiangaze kulingana na Mathayo 5:16 na Mathayo 6:1?

MAWE YALIYOKWISHA KUCHONGWA MACHIMBONI.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments