Je ni kweli hakuna aliyepaa mbinguni zaidi ya Mwana wa Adamu? (Yohana 3:13)

by Admin | 26 April 2023 08:46 am04

Je ni kweli Yesu peke yake ndiye aliyepaa mbinguni, na Eliya hakupaa wala Henoko? Kulingana na Yohana 3:13?

Jibu: Tusome,

Yohana 3:13 “Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu”

Mstari huu lengo lake si kutoa taarifa za waliopaa mbinguni au ambao hawajapaa!, tukiusoma kwa lengo hilo basi ni rahisi kuchanganyikiwa, na kuona biblia inajichanganya…

Mfano mtu anaweza kusikika akitoa kauli hii “hakuna mtu aliyewahi kuja kwangu kunitazama, isipokuwa mtoto wangu tu”.. Kauli hiyo mtu asipojua kwanini imezungumzwa vile, anaweza kutafsiri kuwa “hakuna mtu yeyote aliyewahi kufika nyumbani kwake huyo ndugu, iwe mgeni au mwenyeji, isipokuwa mtoto wake tu…..maana yake anaishi tu peke yake peke yake, au nyumba yake ipo mafichoni mahali ambapo watu hawawezi kufika, au pengine amefunga mlango kwa wageni hivyo hakuna mtu yeyote anayeweza kumtembelea”…

Lakini kumbe hakumaanisha hivyo, yule aliyemsikia hakuanza kusikiliza mwanzo wa maneno yake bali alichukua kipande cha mwisho cha maneno yake… lakini kumbe maneno yake hasa yalianza hivi….. “Tangu nilipoanza kuugua, mpaka nilipopona hakuna mtu aliyewahi kuja kwangu kunitazama isipokuwa mtoto wangu tu “

Na kauli ya Bwana Yesu, aliposema hakuna aliyepaa juu ila aliyeshuka, ina mantiki hiyo hiyo…

Sasa Ili tuelewe vizuri, tuanzie kusoma mstari ule wa 12.

Yohana 3:12 “Ikiwa nimewaambia mambo ya duniani, wala hamsadiki, mtasadiki wapi niwaambiapo mambo ya mbinguni?

13  Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu”

Hapa tunaona ni Bwana Yesu anampa Nikodemu taarifa kuwa “yeye pekee ndio mwenye taarifa za mbinguni, yaani siri za ufalme wa mbinguni”  asizozijua mtu mwingine yeyote.

Na kwanini siri hizo anazo yeye tu peke yake?, na si mwingine yeyote?..Kwasababu ni yeye tu pekee ndiye aliyetokea mbinguni, wengine wote asili yao ni hapa duniani, hivyo hawawezi kujua mambo ya mbinguni wala siri za ndani za mbinguni, kwasababu hawakutokea huko. Lakini Yesu asili yake sio duniani..yeye alikuwepo mbinguni kabla hajazaliwa na Mariamu.

Nabii Eliya alipaa mbinguni lakini hakutokea mbinguni, hivyo hawezi kuyajua ya mbinguni, kwasababu asili yake ni duniani,  yeye  alizaliwa hapa  duniani kama wanadamu wengine wote, mbinguni alienda kama tu sehemu ya mwaliko.. Kama sisi tutakavyoalikwa siku ile ya mwisho ya parapanda.. Tutaenda kama wageni waalikwa, lakini Kristo si mgeni mwalikwa bali Mwalikaji/naye ni mwenyeji.

Ni sawa na Mtoto wa mfalme wa Taifa fulani, aje aishi Tanzania na baada ya muda arejee nchini mwake, halafu kuna kijana mwingine raia wa Tanzania, mzaliwa wa Tanzania apewe mwaliko wa kwenda kuishi Huko kwenye huo ufalme, kipindi chote cha maisha yake.. Je huyu kijana aliyealikwa anaweza kuwa sawa na yule kijana aliye mwana wa Mfalme?.. Au watakuwa na uelewa sawa kuhusiana na mambo ya huo ufalme?.

Jibu ni la! Ni wazi kuwa Huyu kijana wa Mfalme atakuwa  anajua siri nyingi za Taifa lake, kuliko huyu kijana aliyealikwa, kwasababu ni mzaliwa wa kule, na zaidi sana ni mwana wa mfalme, lakini huyu aliyealikwa hatajua sana mambo ya ufalme ule, kwasababu yeye ni kama mwalikwa tu.

Ni hivyo hivyo kwa Eliya na Henoko.. Hao ni waalikwa tu mbinguni, lakini hawakuwa wenyeji wa kule,

Lakini Yesu ni Mwalika, na tena ni mfalme.. hivyo Kristo pekee ndiye ajuaye mambo yote ya  mbinguni, siri zote za Ufalme wa mbinguni, kwasababu yeye ni mwana wa Mfalme na pia asili yake ni kwenye huo ufalme.

Ndio maana sasa biblia inasema hapo… “Ikiwa nimewaambia mambo ya duniani, wala hamsadiki, mtasadiki wapi niwaambiapo mambo ya mbinguni? Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu”.

Maana yake hakuna mtu aliepaa mbinguni kwenda kuzichukua siri na kutujuza sisi, isipokuwa Yule aliyeshuka kutoka kule, ambaye ni Yesu Kristo mwenyewe, Mwana wa Adamu.

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Kwanini Yesu Kristo ni mwana wa Adamu?

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

MJUE SANA YESU KRISTO.

Ni kweli hakuna mtu aliyewahi kuuona uso wa Mungu Zaidi ya Bwana Yesu?

Uishi kwa furaha pamoja na mke umpendaye, siku zote

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/04/26/je-ni-kweli-hakuna-aliyepaa-mbinguni-zaidi-ya-mwana-wa-adamu-yohana-313/