Kutoka 21:10 ina maana gani?.

by Admin | 29 August 2023 08:46 am08

Jibu: Tuanze kusoma  kuanzia mstari wa 7..

Kutoka 21:7 “Mtu akimwuza binti yake awe kijakazi, hatatoka yeye kama watumwa wa kiume watokavyo. 

8 Kwamba bwana wake hakupendezewa naye, akiwa amemposa, ndipo atakubali akombolewe; hana amri yeye kumwuza aende kwa watu wageni maana amemtenda kwa udanganyifu. 

9 Kwamba amposa mwanawe, atamtendea kama desturi zipasazo binti zake. 

10 Kwamba ajitwalia mke mwingine, chakula chake huyo, na nguo zake, na ngono yake, hatampunguzia.  11 Kwamba hamfanyii mambo haya matatu, ndipo atatoka aende bure, pasipo kutolewa mali”.

Jibu: Kwa desturi za kiyahudi mtumwa wa kiume au wa kike anapaswa amtumikie bwana wake kwa muda wa miaka 6 tu, ukifika mwaka wa 7 anakuwa yupo huru kuondoka.,

Kumbukumbu 15:12 “Ikiwa nduguyo, mume wa Kiebrania, au mwanamke wa Kiebrania, akiuzwa kwako, naye amekutumikia miaka sita; basi mwaka wa saba mwache huru aondoke kwako.

 13 Nawe utakapomwacha huru aondoke kwako, usimwache aende zake mikono mitupu”

Ikiwa mtumwa wa kiume aliingia na mke wake basi utakapofika mwaka wa 7 ataondoka na mke wake huyo, (Kutoka 21:1-3) lakini kama aliingia bila mke na akaozwa mke kutoka katika familia ya bwana wake, basi utakapofika mwaka wa 7 atatoka yeye kama yeye, lakini mke na watoto watabaki kwa baba wa mke wake, hana amri ya kuondoka nao, lakini kama hataki kumwacha mke wake na watoto wake basi atamtumikie bwana wake huyo daima kwa agano la kutobolewa sikio kwa uma.

Kutoka 21:5 “Lakini huyo mtumwa akisema waziwazi, Mimi nampenda bwana wangu, na mke wangu na watoto wangu; sitaki mimi kutoka niwe huru; 

6 ndipo hapo huyo bwana wake atamleta mbele ya Mungu na kumleta mlangoni, au penye mwimo wa mlango; na bwana wake ATALITOBOA SIKIO LAKE KWA UMA; ndipo atamtumikia sikuzote”.

Hivyo ishara ya kutobolewa sikio ilikuwa ni ishara ya mtumwa kukataa uhuru wake.

Lakini kwa upande wa mtumwa wa kike (yaani kijakazi) ilikuwa ni tofauti kidogo. Kama kijakazi aliingia bila kuolewa na baadaye kijana wa bwana wake akampenda na kumwoa, kama mke wa kwanza basi famila ya kijana inapaswa kumfanya kama binti yao.

Lakini kama ameolewa kama mke wa pili, na bado ni kijakazi, na bwana wake hamtaki tena awe mke wake au suria wake, basi utakapofika mwaka wa 7, wakati wa maachilio, yeye hatamwachilia kama mabinti wengine wajakazi wanaoachiwa huru, bali kinyume chake ataachiliwa kwa gharama (maana yake atakombolewa).

Hivyo yule baba wa mtoto wa kiume aliyemwoa huyo binti, atamwuza kwa mojawapo wa ndugu aliye karibu, na si kwa mgeni (yaani mtu kutoka taifa lingine tofauti na Israeli), na asipopatikana wa kumnunua ndipo yule kijana ataendelea kuishi naye huku akimtimizia haki yote ya ndoa, ikiwemo CHAKULA, MAVAZI NA HAKI YA NDOA (Ngono).

Vitu hivyo vitatu ni sheria avitimize, si kwasababu hamtaki tena na kakosa mtu wa kumnunua basi aanze kumnyanyasa kwa kumnyima chakula chake na mavazi pamoja na haki ya ndoa ambayo imenenenwa na mtume Paulo kwa uongozo wa Roho katika 1Wakorintho 7:5. Na ikitokea kashindwa kumtimizia hayo mambo matatu basi atamwacha aende zake huru, bila gharama zozote za kumkomboa.

Kutoka 21: 10 “Kwamba ajitwalia mke mwingine, chakula chake huyo, na nguo zake, na ngono yake, hatampunguzia. 

11 Kwamba hamfanyii mambo haya matatu, ndipo atatoka aende bure, pasipo kutolewa mali”.

Mambo gani tunajifunza?

1.Kutoboa masikio si ishara nzuri.

Asili ya kutoboa sikio na kuweka hereni haikuwa nzuri, watu waliotobolewa masikio enzi za zamani ni watu waliokataa uhuru wao, hali kadhalika roho hiyo hiyo inatembea mpaka leo, kibiblia mwanamke au mwanaume hapaswi kutoboa masiko yake. Huenda ulitobolewa enzi hujaokoka, sasa umeshaokoka usiweke hereni baki katika uhalisia wako.

Wengi wanaosumbuliwa na nguvu za giza ni kutokana na vitu wanavyoviweka katika miili yao, na hawajui kuwa hivyo ndio vyanzo vya roho zinazowasumbua.

2. Ni lazima kutimiza haki ya Ndoa

Mtu aliyeoa au aliyeolewa ni sharti amtimizie mwenzie haki zote za ndoa ikiwemo upendo, na ukaribu wakati wowote unapohitajika. Maandiko yanasema mume hana amri juu ya mwili wake kadhalika mke.

1Wakorintho 7:2  “Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe.

3  Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake.

4  Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe.

5  Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu”.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

EPUKA MUHURI WA SHETANI

USIMPE NGUVU SHETANI.

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU NDOA.

TUNAHESABIWA HAKI BURE KWA NJIA YA IMANI.

Tu uzao wake Ibrahimu, wala hatujawa watumwa wa mtu.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/08/29/kutoka-2110-ina-maana-gani/