ANDALIZI LA MWISHO LA UJIO WA MPINGA KRISTO.

by Admin | 5 September 2023 08:46 am09

Je unajua kuwa roho ya mpinga-kristo imeshaanza kutenda kazi na inaendelea kutenda kazi hata sasa?

1 Yohana 4:3 “Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; NA SASA IMEKWISHA KUWAKO DUNIANI”.

Andalizi la mwisho la Mpinga Kristo kabla ya chapa yake kuanza kufanya kazi ni hili “MUNGU HAANGALII MWILI BALI ROHO”.

Roho ya Mpinga-kristo inawaandaa sasa watu na hiyo saikolojia, kwamba waamini Mungu haangalii mwili bali roho tu.

Na kwanini anafanya hivyo?.. ni ili iwe vyepesi kwake siku ile  kuwatia watu CHAPA mwilini (Usoni na mikononi)

Kwasababu asipowaandaa na hiyo saikolojia itakuwa kwake ni ngumu sana kuwashinikiza waipokee chapa katika vipaji vya nyuso na katika mwili siku zile baada ya unyakuo wa kanisa kupita.

Kwahiyo anaanza na saikolojia ndogo tu kwamba kuvaa hereni sio kosa, kutoboa pua sio kosa, kujichora tattoo na hina sio kosa na kupaka lipstick midomoni na wanja machoni sio dhambi.. ( kwamba Mungu hawezi kumhukumu mtu kwa vitu vinavyowekwa mwilini)

Ndugu usidanganyike,  je! Umewahi kujiuliza kwanini Mungu atawahukumu watu wote watakaoipokea  ile chapa ya mnyama  katika VIPAJI vya nyuso zao na katika MIKONO yao siku ile?..

Kama Mungu haangalii mwili kwanini chapa ya 666 itiwe katika mwili na Mungu awahukumu wale wote watakaoipokea chapa hiyo?, maana maandiko yanasema watu wote watakaoipokea chapa hiyo katika vipaji vya nyuso zao au katika mikono basi watahukumiwa katika lile ziwa la moto (Ufunuo 14:9-10).

Sasa kama tu alama ya kishetani katika kipaji cha uso au katika sehemu ya mkono, inaweza kuwa sababu ya mtu kukataliwa na Mungu milele!, vipi hizo tattoo unazochora mwilini, vipi hizo hina unazozipaka na  wanja unaoupaka machoni?, vipi hizo lipstick unazopaka mdomoni na rangi unazopaka kwenye kucha?… Vipi hizo hereni unazozining’iniza masikioni?.

Kama tu leo ni ngumu kuelewa kuwa kupaka wanja ni kosa kibiblia, utashawishikaje siku ile kuamini kuwa kuandikwa alama ya 666 kwenye kipaji cha uso wako ni kosa?..nataka nikuambie kuwa siku ile utaipokea tu chapa kama kawaida.  Kama tu leo kutoboa masikio na kuweka hereni na kutoboa pua na kuweka pini huoni shida, utaonaje shida siku ile utakapotobolewa  katika mkono wako na chipu kuwekwa mwilini mwako?.

Tafakari sana dada!!… tafakari sana kaka!! Tafakari sana Mama, tafakari sana Baba…Usiwe mwepesi kuiga mambo yanayoendelea na kuonekana ulimwenguni, hususani yanayofanywa na watu wengi!…(Mengi ya hayo yanaongozwa na roho ya mpinga kristo)…Ni kweli unajipenda, na ni vizuri kufanya hivyo, ni kweli unapenda uonekane vizuri na maridadi mbele za watu, ni vizuri pia kufanya hivyo lakini vipi na roho yako? Je itaendelea kubaki salama?.

Shetani amewafunga wengi macho siku hizi za mwisho wasiyaelewe maandiko! Na kuwaaminisha kuwa Mungu haangalii mwili bali anaangalia roho.

Dada usidanganyike! Kwasababu udanganyifu upo leo.. na utaendelea kuwepo mpaka wakati wa chapa ya mnyama.

Tupa hereni zote, kachome mawigi, ondoa pistick, na wanja machoni.

Bwana akubariki.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

UTENDAJI KAZI MWINGINE WA ROHO MTAKATIFU USIOUFAHAMU.

JE CHANJO YA KORONA NI ALAMA YA MNYAMA?

KUSAMBAA KWA ROHO YA MPINGA-KRISTO.

NIMEAZIMIA KUWAKUSANYA MATAIFA. NIPATE KUWAMWAGIA GHADHABU YANGU

MAUTI NA UZIMA HUWA KATIKA UWEZO WA ULIMI.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/09/05/andalizi-la-mwisho-la-ujio-wa-mpinga-kristo/