UTENDAJI KAZI MWINGINE WA ROHO MTAKATIFU USIOUFAHAMU.

UTENDAJI KAZI MWINGINE WA ROHO MTAKATIFU USIOUFAHAMU.

Ulishawahi kujiuliza ni kwanini Roho Mtakatifu alicheleweshwa kushuka juu ya mitume ikawachukua muda mrefu  kidogo, Na hata baada ya Yesu kufufuka tunaona iliwapasa tena kungojea kwa muda wa siku 50? Ulishawahi kujiuliza ni kwanini? Sio kwamba walikuwa hawastahili kupokea Roho Mtakatifu tangu zamani, hapana lakini ndio tabia ya Roho Mtakatifu aliyojiwekea, na anafanya hivyo kwasababu zake maalumu.

Hawi mwepesi sana kushuka juu ya mtu kwa haraka kwasababu anajua akishashuka huwa hashuki kwa kipimo au nusunusu, au kuchunguza chunguza. Na ndio maana Bwana Yesu alisubiri kwanza, wanafunzi wake wakamilishwe katika madarasa yake, ili kusudi kwamba watakaposhukiwa na Roho kile kilicho ndani yao kitendeke kwa ufasaha ziadi kama kilivyokusudiwa.

Roho Mtakatifu anafananishwa na MVUA,  Na kama tunavyojua mvua sikuzote ikishuka huwa haichagui hapa kuna ngano au magugu, au mboga, au bangi, au mbigili kazi yake ni kwenda kustawisha tu, hiyo ndio kazi yake. Hivyo ni wajibu wa mwenye shamba kuhakikisha kitu alichokipanda shambani kwake ni chenye manufaa, ahakikishe shamba lake amelipalilia vya kutosha, kwamba hakuna mbegu za magugu chini ya ardhi,vinginevyo itakuwa ni kwa hasara yake mwenyewe pale mvua itakaponyesha na kustawisha magugu badala ya chakula.

Na ndivyo Roho Mtakatifu alivyo, anaposhuka juu ya mtu au kanisa, huwa anakuza au kukiwezesha kile ambacho kimeshapandwa ndani yake. Na ndio maana anaitwa msaidizi, Sasa Kama ulitubu dhambi zako, ukawa unaishi maisha matakatifu, ukawa unabidii katika kumtafuta Mungu, basi Roho akija juu yako, anaikuza hiyo mbegu iliyopo ndani yako, kuwezesha kumjua Mungu zaidi na kuishi hayo maisha kwa viwango vingine vya juu sana.

Na ndio hapo atakuongezea vipawa na karama ili kuhakikisha unafikia pale ambapo umepakusudia na Mungu ufike na hata zaidi. Lakini pale atakaposhuka juu yako, na bado haujajiweka tayari kwa Mungu, kinyume chake, ni mzinzi, au unayo mambo yako ya kidunia, na bado unasema ni  mkristo, atakuja kweli na akija hatakufanya uwe mtakatifu bali atakufanya uwe mwovu zaidi. Hapo ndipo wengi wetu hatujui. Tendo hili katika biblia sehemu nyingine imeitwa “nguvu ya upotevu” itokayo kwa Mungu.. Soma 2Wathesalonike 2:10-12

Utajiuliza ni wapi tena jambo  hilo tena italipata katika biblia,  Embu vitafakari  hivi vifungu, hususani hivyo vilivyo katika herufi kubwa.

Waebrania 6.4 “Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu,

5 na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo,

6 wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri.

7 MAANA NCHI INAYOINYWA MVUA INAYOINYESHEA MARA KWA MARA, NA KUZAA MBOGA ZENYE MANUFAA KWA HAO AMBAO KWA AJILI YAO YALIMWA, HUSHIRIKI BARAKA ZITOKAZO KWA MUNGU;

8 BALI IKITOA MIIBA NA MAGUGU HUKATALIWA NA KUWA KARIBU NA LAANA; AMBAYO MWISHO WAKE NI KUTEKETEZWA”.

Embu jiulize upo katika kanisa muda mrefu, unasema umeokoka, unasali, unafanya ushirika, unaimba kwaya n.k. lakini bado una maisha ya dhambi ya siri siri unayoyajua wewe.. Unatazamia nini pale Roho Mtakatifu atakaposhuka juu yako au juu ya kanisa, upaliliwe kitu gani?

Roho Mtakatifu anaposhuka ndani ya kanisa lake kulinyeshea mvua, halafu anakukuta, wewe ni gugu umepandwa ndani yake, ujue kuwa mvua hiyo itaistawisha gugu, lizidi kustawi zaidi ili siku ya kuteketezwa na kutupwa motoni likapate adhabu iliyokubwa zaidi. Ili kutimiza andiko hili;

Mathayo 13:24 “Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake;

25 lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.

26 Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu.

27 Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu?

28 Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye?

29 Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo.

30 Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu”.

Kumbuka kilichomfanya mfalme Sauli ashukiwe na Roho mbaya kutoka kwa Mungu, ni tabia yake ya wivu na ile ya kudharau maagizo ya Mungu, hivyo ile Roho njema ya Mungu iliposhuka juu yake na kukutana na tabia yake mbaya, ndio ikamfanya awe mbaya, kutaka kumwangamiza Daudi. Lakini kama angekuwa ni mtiifu kwa Mungu na mwenye upendo, Roho ya Mungu ingekutana na tabia hiyo njema na kumfanya kuwa mfalme Hodari zaidi na mshupavu kama alivyokuwa hapo mwanzoni. Hiyo ndio sababu kwanini biblia ilikuwa inasema “Roho mbaya kutoka kwa Mungu” ilikuwa inamjia Sauli..Hizi ndio sababu.(1Samweli 16:14-23)

Hata sasa, tunapaswa tujiangalie sana mienendo yetu katika kanisa, wapo watu baada ya kukaa kanisani   ndio wamezidi kuwa wabaya zaidi, wanafanya mambo ambayo hata watu wa kidunia hawafanyi, kama ulikuwa huji sababu ndio hii. Sasa usidhani mtu kama huyo alianza tu kuwa mbaya, hapana, bali alidharau maagizo ya Mungu, akawa anafanya mambo yasiyofaa kidogo kidogo hivyo hivyo, na mwisho wa siku akajikuta anayafanya kwa nguvu zaidi,..Hajui kuwa tayari kashapotea milele, Na biblia inasema mtu akishafikia hatua hiyo, hawezi kufanywa upya tena atubu, anasubiria kwenda tu katika ziwa la moto. Kwahiyo tujitathimini ni mbegu za aina gani zipo ndani yetu. Ili tuwe na amani pale Roho anaposhuka juu yetu, kutuwezesha zaidi.

Tukipanda mbegu njema katika utakatifu, Roho Mtakatifu atatufanya kuwa watakatifu zaidi, tukipanda katika imani,atatuongezea imani zaidi, tukipanda katika upendo vivyo hivyo, katika kulitafakari Neno lake, atatuongezea mafunuo mengi zaidi n.k. Huo ndio uzuri wa Roho Mtakatifu, ndio maana anaitwa msaidizi.

Yohana 16:13 Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.

Hivyo katika hili eneo tunapaswa tuwe makini sana, hata Bwana Yesu alituonya hivyo. Ni heri ukafanya mizaha katika mambo ya kidunia, lakini sio ndani ya kanisa la Kristo. Kwasababu huko ndani Roho Mtakatifu yupo kuwezesha watu, kwahiyo angalie zisije zikawa ndio dhambi zako zinawezeshwa huko.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOWAFUNULIA WATU MAANDIKO.

NI KWA NAMNA GANI ROHO HUTUTAMANI KIASI CHA KUONA WIVU?

Mungu anaposema “nitaliweka jina langu” ana maana gani?

MTEGO HUTEGWA BURE, MBELE YA MACHO YA NDEGE YE YOTE.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Mch Samwel S.M
Mch Samwel S.M
2 years ago

Bwana Yesu asifiwe.Mungu awabariki sana watumishi katika kuhakikisha Neno la Mungu lina wafikia watu.
Binafsi nimepata kujifunza Mengi katika tovuti hii na mengine yamenisaidia hata katika huduma ambayo naifanya,nimepata ufafanuzi wa mambo mbalimbali hasa maswali tata ya Biblia.
Usomae ukurasa huu soma kwa lengo la kujifunza na kukua kiroho.
Barikiwa.
Pastor Samwel (JRM)