by Admin | 22 September 2023 08:46 pm09
Maelezo ya Mithali 28:20
“Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele; Lakini afanyaye haraka kuwa tajiri hakosi ataadhibiwa”.
Mstari huo unatufundisha jinsi pupa (kutaka vya haraka), inavyokinzana na neno “Uaminifu”. Ikiwa na maana mtu ambaye anataka wingi kwa muda mfupi, ni lazima tu atatumia njia isiyo ya haki, ili avipate anavyovitaka. Kwamfano viongozi wa nchi au waajiriwa wenye tamaa ya mafanikio ya haraka, wanaotaka mwezi huo huo wajenge, au wawe na miradi mikubwa, mwisho wa siku huwa wanatumia njia za wizi, ili kufikia mafanikio yao. Hiyo ndio sababu inayowafanya wapoteze uaminifu katika kile walichokabidhiwa.
Na hatma ya hawa watu, ni kukutana tu na matatizo, aidha kufungwa, au kufukuzwa kazi, au kutozwa faini, n.k.. na kuangukia hasara tu sio faida.
Ndio maana ya hili Neno
Mithali 28:20 Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele; Lakini afanyaye haraka kuwa tajiri hakosi ataadhibiwa.
Kwasababu mafanikio na pupa, havipatani kabisa. Bali achumaye kidogo-kidogo ndiye atakayefanikiwa(Mithali 13:11)
Yusufu alirekodiwa kuwa ni mwaminifu katika kazi yake. Na hivyo, akabarikiwa na Bwana mpaka akapewa nafasi ya uwaziri-mkuu wa taifa kubwa la Misri (Mwanzo 39:1-6). Danieli alirekodiwa kuwa muaminifu na hivyo akadumu katika falme zote mbili zilizotawala dunia wakati ule, yaani Babeli pamoja na Umedi na Uajemi (Danieli 6:4).
Lakini pia Neno hili linatafsirika rohoni.
Katika kazi ya Bwana, palipo na UAMINIFU, basi mwishowe Mungu huwa anabariki utumishi wa mtu huyo. Alisema maneno haya;
Luka 16:10 “Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. 11 Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli? 12 Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?
Umeona? Lakini ukikosa uaminifu, ndio utataka utumie njia zisizompendeza Mungu ili uone matokeo unayoyatarajia haraka, ndio hapo utaona mhubiri anatumia njia za undanganyifu kutengeneza shuhuda za uongo, ili watu wajue kuwa anao-upako wajae kwenye kanisa lake. Mambo kama haya hatma yake ni , uangamivu. Wengine, wanahubiri injili ya kisiasa, au vichekesho, wengine wanapachika staili za kidunia madhabahuni na kwenye kwaya, hawahubiri tena kweli, wala hawakemei dhambi, wakihofia watu kukimbia makanisa yao. Wanapoteza uaminifu ili wapate watu wengi kanisani. Hii ni hatari kubwa!
Hawajui kuwa ndani ya uaminifu, zipo Baraka. Na Mungu anaona, Mungu atamnyanyua tu mtu huyo.
Hivyo tupende kusimamia kweli, turidhike na nafasi zetu, tupinge mambo ya giza, TUWE WAAMINIFU katika yote na hakika tutaona Baraka za Bwana.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group
Mada Nyinginezo:
UAMINIFU NI KIGEZO KIKUBWA CHA KUTUMIWA NA MUNGU.
USIZISHIRIKI DHAMBI ZA WATU WENGINE.
Maana ya Mithali 9:17 “Maji yaliyoibiwa ni matamu, Na mkate ulioliwa kwa siri hupendeza”
Vifungu vya biblia kuhusu Uongozi.
Nini maana ya Mithali 27:6 “Jeraha utiwazo na rafiki ni amini;
TABIA ZA NJIA YA MUNGU KWA MKRISTO
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/09/22/mithali-2820-mtu-mwaminifu-atakuwa-na-baraka-tele/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.