Nakusalimu katika jina kuu sana la Bwana wetu Yesu Kristo, utukufu na heshima vina yeye milele na milele.AMEN. Nakukaribisha katika kuyatafakari maneno ya Mungu, na leo tutaona vile uaminifu unavyomshawishi Mungu, kukupa neema Zaidi ya unachokiomba.
Tumekuwa na maombi mengi sana mbele za Mungu, wakati mwingine tunatamani Mungu atutumie kama Fulani katika biblia, Lakini tusipojua kanuni za Ki-Mungu, kamwe hatutakaa tuvipate, haijalishi tutakuwa ni waombaji au wafungaji wazuri namna gani mbele za Mungu.
Mungu kumfanya Musa, kuwa Mchungaji wa taifa la Israeli, haikuwa ni kwasababu ni mwisraeli tu au anaomba sana. Hapana, ni kwasababu ya maamuzi aliyoyafanya zamani, ambayo yalimponza hata kuwa vile kama alivyokuwa kwa miaka 40. Musa aliona kustarehe katika jumba la kifalme, si kitu, moyo wake ukaanza kuugua juu ya ndugu zake waebrania aliokuwa anaona wanateswa, hivyo siku moja alipoona mmojawapo anaonewa na Mmisri, alikuwa radhi kumtetea ndugu yake, mpaka kumuua yule mmisri, kuonyesha kuwa aliwapenda waebrania kwelikweli, Hata siku ya pili yake, alipoona hao hao waebrania wanagombana, hakuwaacha hivi hivi tu, bali alikwenda kutafuta namna ya kuwapatanisha ili wawe na umoja. Lakini yule aliyemtapeli mwenzake, akamwambia unataka kuniua kama ulivyomuua yule mmisri jana.
Musa angeweza kukana hayo mashtaka hata kwa rushwa kwasababu alikuwa na uwezo huo.. Lakini kinyume chake, akawa tayari, kukubali mashutumu, kwamba yeye ndiye aliyefanya vile, akakimbia akaenda zake jangwani, huku moyo wake ukiugua tu kwa ajili ya ndugu zake. Utaona japokuwa hakujua njia sahihi ya kuwaokoa ndugu zake, lakini alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake, kufanya awezacho.(Matendo 7:22-40)
Huyo ndio mtu ambaye baada ya miaka 40, Mungu anamtokea katika kijiti cha moto, akimwambia, nakutuma uenda Misri ukawaokoe watu wangu kwa mkono mkuu. Ndipo Mungu akamtumia kwa uwezo mkubwa namna ile, kwasababu aliona uaminifu wake, katika kile alichokitamani.
Matendo 7:35 “Musa huyo waliyemkataa, wakisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu na mwamuzi? Ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mkuu na mkombozi, kwa mkono wa yule malaika aliyemtokea katika kile kijiti. 36 Huyo ndiye aliyewatoa, akifanya ajabu na ishara katika nchi ya Misri, na katika bahari ya Shamu, na katika jangwa muda wa miaka arobaini”.
Matendo 7:35 “Musa huyo waliyemkataa, wakisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu na mwamuzi? Ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mkuu na mkombozi, kwa mkono wa yule malaika aliyemtokea katika kile kijiti.
36 Huyo ndiye aliyewatoa, akifanya ajabu na ishara katika nchi ya Misri, na katika bahari ya Shamu, na katika jangwa muda wa miaka arobaini”.
Ukitamani kuwa mchungaji, onyesha tabia hizo tangu sasa kabla hujawa mchungaji wa kanisa la Kristo, ili Bwana ashawishwe, kukupa huduma hiyo, je, unalipenda kundi la Mungu, je unalithamini? , je upo tayari kuwalisha watu chakula cha kiroho, na kusimama nao katika shida zao, bila kuruhusu ibilisi awameze?
Hilo ni jambo la muhimu sana, kulifanya sasa ndugu..
Daudi kabla hajafanywa na Mungu kuwa mchungaji wa Israeli, aliwahi kuwa mchungaji wa kondoo na mbuzi, lakini alipoona adui wanataka kuja kulishambulia kundi, hakuliacha na kukimbia, bali aliweza kupambana na simba, Pamoja na dubu na kuwashinda, akiwa na fimbo tu. Mungu akamuona kuwa huyu anafaa hata kwa watu wangu Israeli kwasababu anathamini, kundi analoliongoza, hata kuwa tayari kuyahatarisha Maisha yake, kwa ajili ya hili..(1Samweli 17:34-36)
Umeona, Bwana Yesu alisema..
Luka 16:10 “Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia”.
Je ni sisi tuitwao wachungaji/Waalimu, wainjilisti, tunazo tabia hizi?
Wapo watu wengine wanasema, Bwana naomba unipe mali nyingi kama Sulemani, ili nizitumie kuisogeza injili yako mbele. Kumbuka, kabla Mungu hajakupa, atahitaji kwanza, aone ulichonacho unakitoaje? Umebarikiwa laki moja, Je!, ulishawahi kuwa radhi kutoa vyote, au sehemu kubwa ya mali zako kwa Mungu mara nyingi, hata kuwa tayari kulala njaa, au kukosa mahitaji yako, kwa Mungu?
Ikiwa hivyo hufanyi, unaishia tu kuomba, jua kuwa utajiri huo unaouhitaji, kamwe hutaweza kuupata.
Mtume Paulo, alilijua hilo, ndio maana akawa mwaminifu sana katika kumtumikia Mungu, katika udogo, ndipo Mungu akamfanya kuwa mtume na Mwalimu wa mataifa.
1Timotheo 1:12 “Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake;”
Hivyo ndugu, chochote, ukitamanicho kwa Mungu, waweza kukupata, lakini, anza sasa, kujitoa kwa hicho, kuwa tayari kuiponza roho yako, hata wakati mwingine kupoteza kila kitu, kwa ajili ya utumishi huo, na hakika yake utakipata kwa Mungu.
Uaminifu wako sasa ni mtaji wa ukitakacho kesho.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp: Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group
Mada Nyinginezo:
JE UNATAMANI KUMJUA MUNGU, NA HUJUI PA KUANZIA?
THAWABU YA UAMINIFU.
Gongo na Fimbo ni nini?
Unyenyekevu ni nini?
NIFANYE NINI ILI NIPENDWE NA MUNGU?
Je! Shetani anao uwezo wa kuumba, kama Mungu?
Rudi nyumbani
Print this post
Amina..ubarikwe