MWONGOZO WA MAOMBI YA ASUBUHI.

by Admin | 26 September 2023 08:46 am09

Watu wengi wanapofikia hatua ya kuomba, wanashindwa kuomba vizuri au  kudumu kwa muda mrefu, sio kwamba hawana nguvu za rohoni, hapana bali wakati mwingine ni kwasababu wanakosa mwongozo wa vitu vya kuombea. Hivyo tumeona tuutoe mwongozo huu mfupi ambao utakusaidia, unapoingia katika maombi yako ya asubuhi. Zingatia: Hii sio kanuni ya daima, Zipo nyakati Roho atakuongoza cha kuombea. Lakini hapa tunakupa mambo muhimu ambayo unapaswa uyajumuishe katika maombi yako ya asubuhi kila siku .

Kiwango cha chini kiwe ni Saa moja (1).

1. SHUKRANI:  Ombi la kwanza liwe ni shukrani, Kumbuka umeianza siku mpya, huna budi kutanguliza shukrani kwa Mungu wako, kwa ajili ya uzima, afya,familia,wokovu, chakula,amani n.k.

Wakolosai 3:15 “…..tena iweni watu wa shukrani”

2. MWONGOZO WA SIKU MPYA: Omba Bwana akutangulie katika siku yako mpya. Ukayatende yale yote aliyokusudia uyatende katika siku hiyo. Usitoke nje ya mpango wake. Ili siku Yako isiwe Bure Rohoni.

Mithali 16:3 “Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika”.

3. NENO LA MUNGU : Omba uwezo wa kulikumbuka na kuliishi Neno la Mungu katika siku yote mpya. Neno lake Lisidondoke moyoni mwako, Usisahau agizo lake hata moja.Uishi Kwa hilo

Zaburi 119:16 “Nitajifurahisha sana kwa amri zako, Sitalisahau neno lako”.

4. ULIMI WAKO: Katika siku yenye masumbufu na pilikapilika ya mambo mengi, Ni busara umwambie Bwana aweke mlinzi katika kinywa chako usijikwae kwa maneno mahali popote.

Zaburi 141:3 “Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu”

5. UTUKUFU WA MUNGU: Mwambie Mungu mambo yote uyafanyao ndani ya siku mpya yawe ni kwa utukufu wake. Na sio wa adui au mwanadamu.

1Wakorintho 10:31  “Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu”

6.WAKATI: Omba Mungu akusaidie kuukomboa wakati wako, siku yako isiwe na mapengo, usipite hivi hivi hujafanya jambo la msingi katika wokovu au maisha yako kwa ujumla.

Waefeso 5:15  “Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; 16  mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu”

7. INJILI YA KRISTO: Mwambie Bwana akupe ujasiri wa kuwashuhudia wengine injili, popote uwapo. Vilevile ombea injili ya Kristo ienee kwa nguvu siku hiyo ulimwenguni kote. Ombea pia watumishi wa Mungu wanaotenda kazi yake, wapewe nguvu ili waitimize huduma hiyo ya Bwana.

Matendo 4:31  “Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri”

8. NDUGU NA FAMILIA: Ipeleke familia yako/ ndugu zako kwa Kristo wakutane nao katika siku hiyo/ waokoke/ wadumu katika wokovu. Umepewa ndugu ili usimame Kwa ajili Yao.

Warumi 10:1  “Ndugu zangu, nitakayo sana moyoni mwangu, na dua yangu nimwombayo Mungu, ni kwa ajili yao, ili waokolewe”.

9. JAMII: Utakutana na watu mbalimbali, mazingira mbalimbali, Hivyo huna budi  uyaombee Amani, utulivu n.k. Ili uweze kuishi pia kwa amani, katika utumishi wako Kwa Bwana.

Yeremia 29:7 “Kautakieni amani mji ule, ambao nimewafanya mchukuliwe mateka, mkauombee kwa Bwana; kwa maana katika amani yake mji huo ninyi mtapata amani”.

10. ADUI: Mwambie Bwana akuepushe na Yule mwovu. Katika siku yako, mwovu asikujaribu katika imani, afya, kazi n.k

Mathayo 6:13  Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.]

Ukitumia walau dakika sita (6), kuombea kila kipengele. Utakuwa umekamilisha SAA MOJA (1), La maombi. Na ukijijengea utaratibu wa kufanya hivi kila siku asubuhi, utaona mabadiliko makubwa sana ya maisha yako ya kiroho na kimwili.

WoKovu bila maombi ni sawa na gari zuri lisilo na mafuta. HUFIKI POPOTE.

Bwana akubariki. Nikutakie maombi mema.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

LITURJIA NI NINI? NA JE IPO KIMAANDIKO?

Je ile nyota ya asubuhi inamwakilisha shetani au Bwana Yesu?

Nini maana ya Mhubiri 10:16, inaposema Ole wako, nchi, akiwa mfalme wako ni kijana?(

Sadaka ya Amani ilikuwaje?

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

IJUE FAIDA YA KUFUNGA PAMOJA NA WANYAMA WAKO.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/09/26/mwongozo-wa-maombi-ya-asubuhi/