Wakili ni nani kibiblia? Uwakili ni nini?

by Admin | 19 October 2023 08:46 pm10

Wakili kibiblia ni mtu aliyepewa usimamizi wa nyumba (Au kaya) ya mtu mwingine. Na usimamizi huo unajumuisha kuanzia kwenye ngazi ya kifamilia, mpaka mali alizonazo bwana wake.

Uwakili tunaona tangu enzi za agano la kale, kwamfano, Eliezeri alikuwa ni wakili wa Ibrahimu. Na tunaona yeye ndio alikuwa mwangalizi wa mali zake, lakini pia ndiye aliyehusika kwenda kumtafutia Isaka, mke katika ukoo wa baba zake Ibrahimu (Mwanzo 15:2, Mwanzo 24).

Lakini pia tunamwona Yusufu, naye alikuwa ni wakili katika nyumba ya Potifa, aliachiwa vyote avisimamie, (Mwanzo 39:5-7).

Vilevile tukirudi kwenye agano jipya tunaona,  Bwana Yesu alitumia mifano ya mawakili, kuwawakilisha watumishi wake wanaofanya kazi ya kuhudumu/kulichunga kundi lake, kwamba kwa mifano ya wao na sisi tujifunze utumishi uliosahihi kwake.

Kwamfano Luka 12:40-48 Inasema;

“Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu.

41  Petro akamwambia, Bwana, mithali hiyo umetuambia sisi tu, au watu wote pia?

42  Bwana akasema, Ni nani, basi, aliye WAKILI mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake?

43  Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo.

44  Kweli nawaambia, atamweka juu ya vitu vyake vyote.

45  Lakini, mtumwa yule akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia kuja, akaanza kuwapiga wajoli wake, wanaume kwa wanawake, akila na kunywa na kulewa;

46  bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini.

47  Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana.

48  Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi”

Ikiwa wewe umepewa dhamana ya kulichunga/kulisimamia kundi, basi tambua kuwa Bwana anataka aone uaminifu wako wa kuwahudumia na kuwalinda watu wake aliokupa. Yesu alipomuuliza Petro Je! Wanipenda akasema ndio nakupenda!, Hapo hapo akamwambia chunga kondoo zangu, lisha kondoo wangu. Kuonyesha kuwa ikiwa wewe ni mtumishi na unasema unampenda Bwana, basi ujue upendo wako ni kuwachunga na kuwalisha kondoo wa Bwana.

Lakini pia uwakili sio tu kwa waliowatumishi wa Mungu, bali pia kwa kila mwaminio, aliyeokoka, amepewa uwakili wa kuifanyia kazi  kwa ile talanta aliyopewa.

Bwana Yesu alitumia mfano wa Yule mtu aliyesafiri, akawaita watumwa wake, akawawekea mali yake yote wafanyie biashara, Hivyo mmoja akapewa talanta 5, mwingine 2, mwingine 1. Kama tunavyoijua habari wale wawili wa kwanza wakafanikiwa kuzalisha, lakini Yule mmoja wa mwisho hakuifanyia chochote talanta yake, akaiacha mpaka aliporudi bwana wake. Matokeo yake ikawa ni kunyang’anywa na kutupwa katika giza la nje (Mathayo 25:14-30).

Hiyo ni kutufundisha kuwa hakuna hata mmoja wetu, ambaye hajapewa karama na Mungu, hivyo unapaswa ujiulize, je! Talanta yangu ninaitumiaje, Uwakili wangu ninautumiaje Je! Ni katika kuujenga ufalme wa Mungu, au katika mambo yangu mwenyewe.

Hivyo kwa hitimisho ni kuwa waliokoka wote ni mawakili wa Kristo. Na hivyo Bwana anataka aone wakihudumu katika nyumba yake kwa uaminifu wote. Na ndivyo mitume wa Bwana walivyojiona mbele za Mungu.

1Wakorintho 4:1  Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu.

2  Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu.

Vifungu vingine ambavyo utakutana na neno hili ni hivi; Luka 16:1-13, 1Wakorintho 9:17, Waefeso 3:2, Wakolosai 1:25.

Bwana akubariki.

Swali ni je! Umeokoka? Kama sio unasubiri nini? Mpokee sasa Bwana Yesu ili akupe uzima wa milele bure. Kumbuka hizi ni siku za mwisho, Yesu yu mlangoni kurudi , akikukuta hujaitendea kazi talanta yako utamjibu nini, Na umeshaisikia injili?

Ikiwa upo tayari leo kumpokea Bwana, akusamehe dhambi zako, basi fungua hapa kwa mwongozo huo wa sala ya toba >>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mada Nyinginezo:

ANGALIA JINSI USIKIAVYO:

Mtakatifu ni Nani?

Talanta ni nini katika biblia (Mathayo 25:14-30)

Tirshatha ni nini? (Ezra 2:63)

Beelzebuli ni nani? (Mathayo 12:24).

Mierebi ni Nini kwenye biblia? (Isaya 15:7)

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/10/19/wakili-ni-nani-kibiblia-uwakili-ni-nini/