NI YESU YUPI UNATEMBEA NAYE?

by Admin | 28 January 2024 08:46 pm01

NI ALIYEFIFIA MAVAZI AU MWENYE MAVAZI MEUPE?

Yesu anajifunua kwa watu kulingana na jinsi mtu huyo anavyotembea naye. Wapo watu wanatembea na Bwana Yesu katika mng’ao wake wa ajabu. Lakini wapo wanaotembea naye katika hali ya kawaida sana. Utajiuliza kwa namna gani.

Wakati mwingi sana, Yesu alipokuwa na wanafunzi pamoja na makutano. Zaidi ya asilimia 98 ya maisha yake, alikuwa hana tofauti na watu wengine wowote. Kiasi kwamba akijichanganya kati ya watu 10, huwezi mtofautisha na yoyote, kimwonekano. Ndio maana wengi, walishindwa kumngundua, alipokuwa na watu soma (Yohana 18:7).

Lakini kuna wakati, alibadilika sura, mpaka mwonekano wake. Tutaona ni nini kilichomfanya awe vile jambo lililowafanya mitume wake kumchukulia kitofauti sana tangu ule wakati.

Marko 9:2  “Hata baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani, peke yao; akageuka sura yake mbele yao; 3  mavazi yake yakimeta-meta, meupe mno, jinsi asivyoweza dobi duniani kuyafanya meupe.

4  Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu. 5  Petro akajibu, akamwambia Yesu, Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. 6  Maana, hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa na hofu nyingi.

7  Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye. 8  Mara hiyo walipotazama huku na huku, hawakuona mtu pamoja nao ila Yesu peke yake.

9  Na walipokuwa wakishuka mlimani aliwakataza wasimweleze mtu waliyoyaona, hata Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu”.

Sababu iliyowafanya Petro, Yohana, na Yakobo, kumwona Bwana katika mwonekano ule. Ni mahali walipokwenda naye. Walikwenda naye mlimani “KUOMBA”. Maombi ndio yaliyopelekea, Yesu abadilike ghafla mbele yao na kuwa na ule utukufu wake wa asili.

Vivyo hivyo na sisi ili tumwone Kristo katika utukufu wake mkamilifu katika maisha yetu, Tupende maombi. Ukiwa mvivu katika kuomba, Yesu atakuwa ni wa kufifia maishani mwako. Hutafurahia uweza wake mtimilifu katika maisha yako, hutafurahia wokovu wako. Mfanye awe kama JUA kwako, ang’ae kweli kweli, mpe nafasi kwasababu yeye ndio Nuru ya ulimwengu. Penda maombi, kila siku omba, kutana naye hapo, hudhuria mikesha sana, omba kwa bidii, ondoa uvivu.

 Usipomruhusu Yesu akupangie maisha yako, kimaombi, shetani atakusaidia kuyapanga.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Tofauti kati ya maandiko na Neno ni ipi?

MAVAZI YA NDANI NA YA NJE.

FAIDA ZA MAOMBI.

USIYAACHE MAVAZI YAKO NA KWENDA UCHI!

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/01/28/ni-yesu-yupi-unatembea-naye/