USIYAACHE MAVAZI YAKO NA KWENDA UCHI!

USIYAACHE MAVAZI YAKO NA KWENDA UCHI!

Kuna mahali Bwana wetu Yesu alisema maneno haya..

Ufunuo 16:15 “ (Tazama, naja kama mwivi. HERI AKESHAYE, NA KUYATUNZA MAVAZI YAKE, ASIENDE UCHI HATA WATU WAKAIONE AIBU YAKE.)”

Umewahi kujiuliza ni kwanini, Bwana aseme heri akeshaye “na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi”?.

Katika hali ya kawaida mtu hawezi kutoka mahali na kwenda uchi labda awe na matatizo ya akili, lakini kwa mtu mwenye akili timamu, haiwezekani kutoka nje akiwa uchi na kutembea hivyo barabarani na watu kumwona..

Lakini Bwana alivyosema hayo, alikuwa na maana!. Kwamba inawezekana pia mtu kutoka nje akiwa uchi, na watu kuiona aibu yake. Endapo atakuwa yupo katika mazingira Fulani.. Hebu tusome kisa kimoja kwenye biblia kisha tuendelee mbele.

Marko 14:48 “Yesu akajibu, akawaambia, Je! Ni kama juu ya mnyang’anyi mmetoka wenye panga na marungu, kunitwaa mimi?

49  Kila siku nalikuwa mbele yenu hekaluni nikifundisha, msinikamate; lakini haya yamekuwa ili maandiko yapate kutimia.

50  ndipo wakamwacha, wakakimbia wote.

51  NA KIJANA MMOJA ALIMFUATA, AMEJITANDA MWILI WAKE NGUO YA KITANI; WAKAMKAMATA;

52  NAYE AKAIACHA ILE NGUO YA KITANI, AKAKIMBIA YU UCHI”.

Umeona mazingira kama hayo?.. Kijana alikuwa ni moja wa wanafunzi wa Yesu!,  Lakini alipoona hali imekuwa tete!!.. Anakwenda kufa na Bwana!.. na ameshakamatwa, lile vazi lake zuri la KITANI, aliliacha!, pale na kumkimbia Bwana, akakimbia uchi!.. na watu wakaiona aibu yake.

Jambo hilo hilo linaendelea katika roho leo hii.. Tunapoamua kuwa wanafunzi wa Yesu, tunakuwa tunavikwa na Bwana VAZI ZURI LA KITANI, Ambalo vazi hilo tafsiri yake ni “utakatifu”..tunalithibitisha hilo katika…

Ufunuo 19:8  “Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni MATENDO YA HAKI YA WATAKATIFU”.

Hivyo tunapoamua kumfuata Bwana, na kuwa wanafunzi wake ni lazima tujikane nafsi tubebe misalaba yetu, pamoja na mavazi yetu mazuri ya kitani. Tuwe tayari kufa tukiwa na Bwana. Lakini kama hatumtaki Bwana tufahamu kuwa hatuwezi kumkimbia bado tukiwa na yale yale mavazi yetu ya kitani(matendo ya haki).. ni lazima tuache mavazi yetu pale ndipo tukimbie uchi!, na watu wataiona aibu yetu.

Je! na wewe leo umeyaacha mavazi yako nyuma, na kukimbia uchi! Kwasababu tu umepitia mtikisiko kidogo kwenye imani yako??, kwasababu umetengwa na wazazi?, kwasababu umechukiwa na ndugu?, kwasababu boss wako hataki wewe usali,  hivyo na wewe umeamua kumwachia Bwana mavazi yako(yaani matendo yako ya haki) na kukimbia uchi (kurudia machafu ya ulimwengu)??.. Kumbuka tena Bwana anasema maneno haya…

Ufunuo 16:15 “(Tazama, naja kama mwivi. HERI AKESHAYE, NA KUYATUNZA MAVAZI YAKE, ASIENDE UCHI HATA WATU WAKAIONE AIBU YAKE.)”

Je unayatunza mavazi yako?.. Usimwachie Bwana mavazi yako na kukimbia uchi kwasababu ya majaribu.. Kabla ya kuamua kumfuata Bwana Yesu, kumbuka kujikana nafsi, ujue kuwa kuna majaribu utakutana nayo mbeleni, ambayo yanaweza hata kuhatarisha maisha yako, katika hayo hupaswi kuyavua mavazi yako, ili kuusalimisha mwili wako.

Marko 8:35  “Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha”.

Bwana atusaidie, na kutubariki.

ANAKUJA KAMA MWIVI!.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

KUOTA UPO UCHI.

VAZI KUU AMBALO MUNGU AMETUANDALIA KILA MMOJA WETU.

Kutahayari ni nini katika biblia?(2Timotheo 2:15)

WALIYATWAA MAVAZI YAKE, WAKAFANYA MAFUNGU MANNE,

JE! UNAYATUNZA MAVAZI YAKO?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments