WALIYATWAA MAVAZI YAKE, WAKAFANYA MAFUNGU MANNE,

WALIYATWAA MAVAZI YAKE, WAKAFANYA MAFUNGU MANNE,

Yohana 19:23 “Nao askari walipomsulibisha Yesu, waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu.

24 Basi wakaambiana, Tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani. Ili litimie andiko lile linenalo, Waligawanya nguo zangu, Na vazi langu wakalipigia kura. Basi ndivyo walivyofanya wale askari”.

Ulishawahi kujiuliza ni kwanini biblia haijakaa kimya kuhusiana na mavazi ya Yesu pale Goligotha, na jinsi yalivyopigiwa kura? Mpaka kufikia hatua ya kugawanywa katika mafungu manne (4) kwa wale askari wanne waliokuwa pale msalabani.? Na lile moja la 5 ambalo ni kanzu yake kupigiwa kura?. Haikuandikwa kutengeneza stori tu, kwamba Yesu alikuwa na mavazi matano, bali kulikuwa na maana nzito nyuma yake.

Hiyo ni kuonyesha kuwa hakubakiwa na nguo hata moja muda ule alipotundikwa  pale msalabani. Alisulibiwa akiwa uchi kabisa wa mnyama. Ni jambo ambalo haliwezekani kwamba nguo nyingine zipigiwe kura, na kugawanya, halafu nyingine abakiwe nazo kutundikiwa msalabani, Maandiko hayatuonyeshi hivyo. Kile tunachokiona kwenye misalaba ya kuchonga au kwenye muvi  kwamba Bwana Yesu alisulibiwa akiwa na kipande cha nguo cha kumsitiri, si kweli. Ukweli ni kwamba alisulibiwa akiwa uchi kabisa wa mnyama. Hata hivyo wakati ule wa Rumi wahalifu wote waliouliwa kwa kusulibiwa ilikuwa ni lazima wasulibiwe uchi, ili kwamba sio tu wafe kwa mateso bali pia wafe kwa aibu.

Je! ulishawahi kutafakari kwa utulivu kwanini Kristo aruhusu hayo yote yampitie, wakati alikuwa na uwezo kabisa wa kuyaepuka? Unadhani hakikuwa kitendo cha aibu kile? Kilikuwa ni kitendo kikubwa sana cha aibu, ambacho ninauhakika hata wewe ungekuwepo wakati ule usingedhubutu hata kumwangalia pale msalabani akiwa katika hali ile. Lakini yeye hakuona aibu, kuwekwa uchi, ilimradi tu mimi na wewe tu tuokoke. Huko ni kujitoa kulikopitiliza.

Hakunionea haya mimi, vilevile hakukuonea haya wewe, kinyume chake biblia inatuambia aliidharau aibu,

Waebrania 12:2 “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba NA KUIDHARAU AIBU, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu”.

Unaona, ukitafakari hilo vizuri, ndugu yangu, hutaona sababu ya wewe kumwonea aibu Bwana wako, katika dunia hii mbovu. Hutaona aibu kuitwa mshamba, kwa ajili yake, hutaona sababu  kuogopa kuitangaza injili yake.

Paulo alisema..

Warumi 1:16 “Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia”.

Alimwambia pia Timotheo maneno hayo hayo;

2Timotheo 1:8a “Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, ..;”

Huu si wakati wa kufikiria Fulani atanionaje, au marafiki watanichukuliaje, au majirani watanizungumziaje ikiwa nitampa Kristo Maisha yangu. Kumbuka Yesu hakukuonea haya wewe, aliposulibiwa uchi mbele ya kadamnasi, mbele ya maelfu wa watu waliokuwa pale Goligota, kwanini wewe umwonee haya yeye wakati hujafikia hata hatua ya kutembezwa uchi barabarani kwa ajili yake?.

Ukimkataa leo wakati utafika atakukataa na wewe.

Marko 8:38 “Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu”.

Tengeneza picha unasimama mbele ya mamilioni kwa mamilioni ya malaika, halafu Kristo anakuonea aibu mbele yao, utajisikiaje? Hali Fulani mbaya,

Hivyo chukua msalaba wako ujitwike umfate Kristo. Hizi ni siku za mwisho, yupo mlangoni kurudi. Kama bado hujatubu basi huu ndio wakati wako, mwamini yeye ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO, upate ondoleo la dhambi zako na yeye mwenyewe atakupa Roho wake Mtakatifu atakayekuongoza katika kweli yote.

Ikiwa utahitaji kuokoka, basi wasiliana nasi kwa namba hizi hapo chini, Nasi tutakusaidia katika hilo.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

VAZI KUU AMBALO MUNGU AMETUANDALIA KILA MMOJA WETU.

kwanini yule kijana aliitupa ile nguo ya kitani chini na kukimbia uchi?

Kutahayari ni nini katika biblia?(2Timotheo 2:15)

MARINDA KATIKA BIBLIA NI KITU GANI?

Nguo za magunia katika biblia ni zipi?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments