Je! Mfalme Abiya na Mfalme Asa walikuwa ni ndugu?

Je! Mfalme Abiya na Mfalme Asa walikuwa ni ndugu?

Katika 1Wafalme 15:2 na 1Wafalme 15:10 tunaona wote mama yao ni mmoja, ambaye ni Maaka, binti Absalomu. Lakini Mstari wa 8 unasema ni mtu na mwanawe.

Jibu: Tusome,

1Wafalme 15:1 “Mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, ABIYA alianza kutawala juu ya Yuda

2 Miaka mitatu akatawala huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa MAAKA, BINTI ABSALOMU…………..

8 Abiya akalala na baba zake, wakamzika mjini mwa Daudi. Akatawala Asa mwanawe mahali pake.

9 Mwaka wa ishirini wa Yeroboamu mfalme wa Israeli, ASA ALIANZA KUTAWALA JUU YA YUDA.

 10 Akatawala miaka arobaini na mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa MAAKA, BINTI ABSALOMU”

Ni muhimu kufahamu kuwa katika biblia, hakuna Neno “BABU” wala “BIBI”. Neno bibi katika biblia lilitumika tu kuwakilisha “Mwanamke mstahiki” kama vile bibi-arusi, au mwanamke mwenye hadhi Fulani (soma Esta1:18, Mwanzo 16:9) lakini sio “mama wa mama” kama leo hii tunavyolitumia, kwamba  wale waliowazaa mama zetu au baba zetu tunawaita “Bibi” au wale mababa waliowazaa baba zetu tunawaita “Babu”. Katika biblia hilo jambo halipo… Yule aliyemzaa baba anaitwa hivyo hivyo “Baba” na Yule aliyemzaa mama anaitwa hivyo hivyo “mama”..haijalishi ni vizazi vingapi vitapita, Yule babu wa babu wa babu, bado ataitwa baba tu!

Kwamfano utaona Mfalme Hezekia katika biblia ambaye alikuwa ni kutukuu cha 13 cha Mfalme Daudi, Lakini Mungu anamtaja kama Daudi ni baba yake na si babu yake. (soma 2Wafalme 20:5) unaweza kusoma pia,  2Nyakati 21:12, kutoka 3:15, Hesabu 32:8, kumbukumbu 1:8, Yoshua 24:2, Waamuzi 2:1, 1Samweli 12:6. N.k. Utaona jambo hilo hilo..

Kwahiyo tukirudi kwenye swali letu, ni kwamba huyu Maaka alikuwa ni mama wa Mfalme Abiya na ni bibi wa mfalme Asa, kwasababu Asa alikuwa ni mtoto wa Mfalme Abiya kama tunavyosoma hapo katika mstari wa 8.

1Wafalme 15:8 “Abiya akalala na baba zake, wakamzika mjini mwa Daudi. Akatawala Asa mwanawe mahali pake”

Kwahiyo biblia ingeweza kumtaja Maaka kama ni bibi wa Asa, badala ya mama lakini haina hilo neno bibi, halipo bali “mama” ndio maana unaona imewataja wote wawili (Abiya na Asa) kwamba mama yao ni mmoja, anayeitwa Maaka.  Na kama ukizidi kuendelea kusoma habari hiyo utaona, huyu Asa alipoingia tu katika ufalme alimtoa bibi yake huyo katika umalkia kwasababu alikuwa ni mwovu mbele za Bwana, kwa namna ya kawaida ni ngumu mtu kumtoa kwenye umalkia mama yake mzazi kwasababu huwa kunakuwa na uhusiano mkubwa sana wa tabia ya mtoto wa kiume na mama yake.

Sasa kwanini Biblia isitumie maneno “Babu” au “Bibi” na badala yake inatumia tu Baba au Mama, haijalishi ni vizazi vingapi vimepita?

Ni kwasababu Mungu anataka kutufundisha jambo Fulani la kiroho, kwamba na yeye mwenyewe si BABU yetu, bali ni BABA YETU haijalishi ni vizazi vingapi kabla yetu.

Kwa ufupi Mungu hana “wajukuu”. Huwezi kusema mimi ni mjukuu wa Mungu, sisi wote ni watoto wa Mungu, na Mungu wetu ni Baba yetu.. ndio maana kaondoa cheo cha “Ubabu” katika maandiko yake.

Mwanao utakayemzaa hatakuita wewe baba, na Mungu amwite Babu, bali atakuita wewe “baba” na Mungu atamwita “BABA” ya herufi kubwa!!. Kwasababu wewe ni kivuli tu! Cha Baba halisi aliye mbinguni.

Waefeso 3:14 “Kwa hiyo nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa”.

Maana yake ni kwamba kwa chochote kile unachokifanya anakuchukulia wewe kama mwanae, na baba yako wa kimwili anamchukulia kama mwanae..hivyo katika roho wewe na baba yako wa kimwili ni mtu na kaka yake, hana upendeleo!!. Ukifanya linalostahili makosa atakuadhibu kama mwanae, na si kama mjukuu na baba yako vile vile atamwadhibu kama mwanae.. Kadhalika mkifanya mambo mazuri wote anawapa thawabu kama wanae.

Lakini kumbuka si wote katika hii dunia, Mungu ni Baba yao… wengi bado hawajafanyika watoto wa Mungu, tofauti na inavyoaminika na wengi leo kwamba sisi wote ni watoto wa Mungu! La huo sio ukweli hata kidogo.. wengi ni watu tu walioumbwa na Mungu!, lakini si watoto wa Mungu. Biblia inasema ili tufanyike watoto wa Mungu ni lazima tupasi huu mtihani hapa chini…

Yohana 1:11  “Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea.

12  BALI WOTE WALIOMPOKEA ALIWAPA UWEZO WA KUFANYIKA WATOTO WA MUNGU, NDIO WALE WALIAMINIO JINA LAKE;

13  waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu”

Swali ni je!.. Umempokea?..ili upewe huo uwezo wa kufanyika mwana?..

Kama hujampokea fahamu kuwa bado wewe sio mtoto wa Mungu, huwezi kuwa mrithi wa ufalme wa mbinguni. Kwasababu katika hali ya kawaida watu hawawarithishi watu wasio watoto wao mali zao. Vivyo hivyo Mungu hawezi kuwarithisha wale wasio wanawe urithi wake.

Kama unatamani kwenda mbinguni na kuurithi uzima wa milele, leo hii mpokee Yesu maishani mwako, na dhamiria kuacha dhambi na katafute kubatizwa ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu (Matendo 2:38). Na baada ya hapo, Roho Mtakatifu atakayeingia ndani yako atakupa uwezo wa kufanyika mwana, na Mungu kwako atakuwa Baba.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

KWANINI UNAPASWA UWE BIBI ARUSI NYAKATI HIZI ZA MAJERUHI?

Kwa jina lake Ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa.

Mbari ni nini kibiblia?

HAKUNA MTU ANIONDOLEAYE, BALI MIMI NAUTOA MWENYEWE

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Prisca komba
Prisca komba
2 years ago

Asante mtumishi