UVUMILIVU NA MIKAKATI YA ABSALOMU, INA FUNZO NYUMA YAKE.

UVUMILIVU NA MIKAKATI YA ABSALOMU, INA FUNZO NYUMA YAKE.

Kati ya watoto ambao Daudi aliwapenda sana na wakati huo huo wakamsumbua sana, ni Absalomu. Absalomu alikuwa ni kijana mzuri wa umbo, na vilevile alikuwa ni kijana aliyetumia mbinu za kipekee sana katika kutimiza malengo yake.

Absalomu, alileta taharuki kuu mbili Israeli, Taharuki ya kwanza, ni ile ya kumuua ndugu yake, aliyeitwa Amnoni, mwana wa mfalme, na ya pili ni ile ya jaribio lake la kuupindua ufalme wa Baba yake (Daudi).

Kama wewe ni msomaji wa biblia, kitabu cha 2Samweli sura ile ya 13-19, utakutana na habari hizo, utakumbuka kuwa huyu Absalomu alikuwa ni dada yake wa tumbo moja aliyeitwa Tamari, lakini ikatokea siku moja ndugu yake wa mama mwingine aliyeitwa Amnoni, akamtamani, na mwisho wa siku akamwingilia kwa nguvu, bila kufuata utaratibu, hivyo akamletea aibu kubwa binti Yule, pamoja na ndugu yake. Sasa huyu Absalomu, ambaye ni kaka wa mama mmoja na Tamari,  alipopata habari akaudhika sana kwa kitendo kile, akamchukia Amnoni kupindukia.

Lakini tabia moja ya Absalomu,ilikuwa si ya kuchukua maamuzi ya muda huo huo, na ndio maana utasoma, hakuzungumza naye neno lolote lile liwe la heri au la shari, bali alitulia kimya tu. Sio kwamba moyoni alikuwa hawaki.

2Samweli 13:22 “Ila Absalomu hakusema na Amnoni wala kwa heri wala kwa shari; kwa maana Absalomu alimchukia Amnoni kwa kumtenza nguvu umbu lake Tamari”.

Akaanza chini chini kupanga mipango yake, ambayo ilikuja kutimia MIAKA MIWILI MBELE. Na mipango hiyo ilikuwa ni ya kumwangamiza ndugu yake.

Ukisoma utaona alianza kazi ya ukataji manyoya, na alipofanikiwa baada ya miaka miwili mizima akamwalika baba yake na ndugu zake waje washereheke pamoja naye, hivyo akatumia sasa fursa ile kumwomba baba yake yule ndugu yake aliyembaka dada yake, awepo, akakubali, na alipoenda, akamvizia saa amelewa, akatuma watumishi wake wamuue. Lengo lake likawa limetimia hapo hapo. Amnoni akafa. Kirahisi hivyo. Unaweza kujiuliza ni kwanini, Absalomu hakuchukua hatua za haraka tangu mwanzoni? Jibu ni kuwa ipo tabia ambayo Mungu anataka tujifunze kwa mtu huyu, jinsi alivyokuwa mtu wa mikakati.

Baadaye, baba yake alipopata taarifa akataka kumuua, lakini Absalomu akakimbilia taifa lingine akakaa huku muda wa miaka mitatu mizima.Sasa, kwa muda wako fuatilia kisa hicho katika biblia, lakini nataka tuone jinsi tabia yake ile ile ya uvumilivu na malengo ilivyomletea mafanikio mengine makubwa mbeleni.

Ukisoma biblia utaona, ulifika wakati akarudi Israeli, na kwenda kuonana na baba yake, Lakii  akiwa kama mgeni alidhamiria ndani ya moyo kuwa mfalme wa Israeli. Kama ilivyo kawaida yake alijua njia pekee sio kuanza kukurupuka na kuleta mapinduzi kwa haraka hapana, hatafanikiwa bali, alijua uvumilivu na bidii, ni nguzo muhimu sana za kutimiza malengo yake.

Hivyo akaanza mikakati yake, biblia inatuambia, akawa anaamka kila siku asubuhi sana na mapema, labda saa 10 alfajiri, anakwenda kusimama, karibu la lango la kuelekea kwa mfalme, ili kukutana na watu wenye shida zao,ambao wanahitaji kutatuliwa. Alipokutana nao, kila mmoja kabla ya kufika kwa mfalme alimbusu, akajinyenyekeza kwake, akamsikiliza shida zake, akamjibu  kwa upole, ikawa kila mtu aliyetoka pale alimpenda sana, na mwisho akawa anawaambia, maneno ya uongo, kuwa hakuna mtu anayewajili, kama wakimfanya yeye kuwa mfalme awatafanyia mema mengi..

2Samweli 15:1 “Ikawa baada ya hayo, Absalomu akajiwekea tayari gari na farasi, na watu hamsini wa kupiga mbio mbele yake.

2 Tena Absalomu huondoka asubuhi na mapema, na kusimama kando ya njia ya lango; kisha ikawa, mtu ye yote aliyekuwa na neno, lililokuwa halina budi kufika kwa mfalme ili kuhukumiwa, Absalomu humwita mtu huyo kwake, na kumwuliza, Wewe u mtu wa mji gani? Naye akasema, Mtumwa wako ni mtu wa kabila fulani ya Israeli.

3 Naye Absalomu humwambia, Tazama, maneno yako ni mema yenye haki; lakini hapana mtu aliyeagizwa na mfalme kukusikiliza.

4 Tena Absalomu husema, Laiti mimi ningewekwa kuwa mwamuzi katika nchi hii, ili kila mtu mwenye neno au daawa aje kwangu, nimpatie haki yake!

5 Tena ikawa hapo alipokaribia mtu ye yote kumsujudia, hunyosha mkono wake, na kumshika, na kumbusu.

6 Hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Israeli wote, waliomwendea mfalme ili wapate hukumu; na hivyo Absalomu akawadanganya watu wa Israeli.

7 Hata ikawa mwisho wa miaka minne, Absalomu akamwambia mfalme Tafadhali uniache niende nikaondoe nadhiri yangu, niliyomwekea Bwana huko Hebroni”.

Aliendelea hivyo kwa muda wa MIAKA MINEE (4), Mfululizo, akiamka asubuhi, kwa ajili ya kukutana na shida zao hao watu.. Ndipo watu wote, wakamtambua, wakampenda sana, kwa unyenyekevu wake, na kujali kwake, wakamsikiliza hata kwa uongo wake, Absalomu akafanikiwa kujikusanyia wimbi kubwa la watu waliompenda..akapata nguvu, huku baba yake hajui chochote.

Ndipo siku ya siku ilipofika, ghafla, Daudi akasikia mtoto wake Absalomu,  amekusanya majeshi ya watu, yanataka kuja kumpindua. Daudi kuona vile ikampasa akimbilie msituni kuokoa maisha yake. Na kama sio Bwana alikuwa upande wake, ule ufalme ulikuwa ni wa Absalomu. Kwasababu watu wengi sana waliandamana naye. Na vita vilivyopiganwa Israeli kipindi hicho vilikuwa ni vikubwa sana, hatuna nafasi ya kueleza habari yote, lakini kwa muda wako soma kwenye biblia utajionea.

Mpaka wakati ambapo Absalomu anakufa, Mfalme Daudi alikuwa ameshapata somo kubwa sana.

Ni nini tunajifunza?

Kumbuka hadithi zote tunazozisoma katika agano lake, zimebeba funzo kubwa kwetu, haijalishi ni za mtu mwovu au mwema. Leo sisi kama watoto wa Mungu, tumekuwa watu wa kutazamia mapinduzi ya wakati huo huo. Tunataka yote tunayoyatazamia yatokee ndani ya usiku mmoja. Kumbe hiyo siyo kanuni, ili tuteke, wakati mwingine tunahitaji uvumilivu na bidii. Itakupasa uhubiri injili kila siku kwa muda wa miaka kadhaa, bila kuona chochote, ndipo baadaye sana uanze kuvuna matunda ya kusumbuka kwako.

Itakugharimu ufanye mazoezi mengi sana ya kuimba, utunge nyimbo nyingi tu, ndipo baada ya kipindi fulani pengine  miaka kadhaa, Bwana ndio azifanye nyimbo zako kuwa Baraka kwa watu wengi.  Kama unataka karama ya uponyaji itende kazi ndani yako, itakugharimu uwe mvumilivu wa kuchukuliana na matatizo ya watu wengi, kuwaombea kwa bidii, hata kama hutaona lolote katika siku za kwanza kwanza, itakubidi uendelee hivyo hivyo, hata kwa miaka kadhaa pengine, lakini mwisho wake Bwana atakujalia kipawa hicho kwa viwango vingine. Uvumilivu na bidii, inapaswa iwe sehemu ya maisha yetu.

Absalomu, hakuwa mtu wa papo kwa papo, lakini uvumilivu wake na mikakati yake ilimsaidia sana baadaye, kuitikisa Israeli.  Hivyo usikate tamaa, unapoona chochote unachomfanyia Mungu sasa, hakizai kama vile unavyotazamia.. Kamwe usife moyo, kinyume chake ongeza bidii. Na wakati utafika utaona matunda ya taabu zako.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

UKIOKOKA, JIANDAE KUPITISHWA USIPOPATAZAMIA.

Nini maana ya siku moja kwa Bwana ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja? (2Petro 3:8)

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 3

USIMLAANI KIZIWI, WALA USITIE KWAZO MBELE YA KIPOFU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments