by Admin | 8 February 2024 08:46 am02
SWALI: Nini maana ya Mithali 20:11 inaposema;
Hata mtoto hujijulisha kwa matendo yake; Kwamba kazi yake ni safi, kwamba ni adili.
JIBU: Mwandishi anatuonyesha kuwa tabia ya mwanadamu yoyote, huwa haijifichi kufuatana na umri wake, kwamba yaweza kukaa ndani tu kipindi cha utotoni isionekane ikaja kudhihirika ghafla ukubwani. Hapana, anasema “Hata mtoto hujijulisha kwa matendo yake; Kwamba kazi yake ni safi, kwamba ni adili”.
Ikiwa na maana katika utoto ule ule unaweza kuuchunguza mwenendo wa mtoto, ukautambua. Na hiyo itakupa fursa ya kuurekebisha ukiwa ni mbaya, au kuuimarisha ukiwa ni mzuri, akiwa katika vipindi kile kile. Usione mwanao anayotabia ya udokozi, ukasema huyu ni mtoto tu, haelewi anachokifanya. Hapana unapaswa umrekebishe mapema, kwasababu hicho kitu kipo ndani yake, Ukiona mtoto anapenda kutazama biblia, anapenda kukaa kanisani, anapenda kusikiliza nyimbo za injili. Usiseme, huyu ni mtoto, ukampuuzia tu, kwa kuishia kusema ‘ubarikiwe mwanangu’ kinyume chake, mwendelezee mazingira hayo, kwasababu mwelekeo wa maisha yake, ni huko.
Ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo, tabia zake zilianza kuonekana tangu utotoni, wazazi wake walimstaajabia, kumwona katika umri ule mdogo, yupo hekaluni, amekaa na waalimu na wakuu wa dini akiwauliza maswali, Kinyume chake wazazi wake hawakumkemea, bali waliyaweka yote mioyoni mwao, na kukubali kuutambua mwelekeo wa mtoto wao.
Hii ni kufundisha nini?
Lipo funzo la rohoni, lakini pia la mwilini.
La mwilini ni kuwa yatupaswa tuwatazame watoto, bila kupuuzia kitendo chochote wanachokidhihirisha katika umri ule wa chini. Ikiwa ni chema tukipalilie, ikiwa ni kibaya, tukikemee, na kushughulika nacho kwelikweli kabla hakijaweka mizizi. Hivyo hakuna mzazi au mlezi anaweza kusema, huyu mwanangu kabadilika tu ghafla. Ukweli ni kwamba mabadiliko yalianza kuwepo tangu zamani, isipokuwa kwa namna moja au nyingine tulipuuzia, tulipoyaona ndani yao tukadhani ni tabia za utoto tu. Wazazi wanaowajenga wanao katika maadili na vipawa tangu utotoni, ukiwatazama watoto wao wanapokuwa watu wazima, huwa wanakuwa na ufanisi na ujuzi wa hali ya juu sana, zaidi ya wale ambao watajijengea wenyewe wanapokuwa watu wazima. Hivyo mzazi jali maisha ya kiroho ya mwanao.
Vilevile rohoni, wapo ambao ni wachanga kiroho. Ikiwa na maana katika kanisa ni wale ambao wameokoka hivi karibuni. Halikadhalika hawa nao utaweza kutambua karama zao, sio mpaka wawe wakomavu kiroho. Aliye Mwinjilisti, utaona anapenda kushuhudia, lakini pia anauwezo wa kuwavuta wengine kwa Bwana. Aliye mwalimu, utaona anapenda sana kujifunza, aliye nabii, utaona karama za maono, ndoto, huwa zinamjia mara kwa mara, hata kwa namna ambazo hazielewi elewi, mwimbaji atapenda wakati mwingi kujifunza kuimba hata kama hawezi. Hivyo, kila mmoja wetu, kitu ambacho Mungu amekiweka ndani yake, hujidhihirisha mapema sana pindi ameokoka. Sio mpaka awe amekomaa sana kiroho kama wengi wanavyodhani.
Pindi unapookoka, kipindi hicho hicho karama yako inaanza kufanya kazi, unapachopaswa tu, ni kujishughulisha na utumishi wa Bwana, ndivyo utakavyoruhusu mambo hayo kutokea kwa wepesi na urahisi zaidi?
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine
MZAZI, JALI MAISHA YA KIROHO YA MTOTO WAKO.
(TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!
Uasherati wa Kiroho maana yake nini?(Opens in a new browser tab)(Opens in a new browser tab)
MAANA WEWE, BWANA HUKUWAACHA WAKUTAFUTAO”.(Opens in a new browser tab)
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/02/08/mithali-2011-hata-mtoto-hujijulisha-kwa-matendo-yake/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.