Je! Kuota unakabwa, mara kwa mara ni ishara ya nini?

by Admin | 27 February 2024 08:46 pm02

SWALI: Mimi kila nikilala, huwa kuna kitu kinanikaba koo, nakosa pumzi, kinanikandamiza naona kama nakwenda kufa au wakati mwingine ninaganda muda mrefu siwezi kusogea. Hata nikijaribu kukemea, natumia kushindana sana, baadaye kinaniachia, Je hili ni jinamizi?. Jambo hili limekuwa likijirudia mara kwa mara. Nimejaribu kufunga na kuomba zinaweza pita tu  siku kadhaa halafu kikajirudia tena. Naomba msaada nifanye nini?


JIBU: Hayo ni mashambulizi ya adui ndotoni. Tufahamu kuwa adui hashambulii tu katika mwili, lakini wakati mwingine pia katika ndoto. Wapo watu wanaosumbuliwa na shetani husasani katika maeneo ya ndoto.

Utakuta kila anapolala, ni mfululizo tu wa ndoto za kipepo, labda anafukuzwa-fukuzwa, au anazini-zini na mapepo hayo, au yupo makaburini, anafanya mambo ya kichawi, zaidi wengine zinakuwa ni mwendelezo, yaani pale alipoishia jana, leo anaendelea nazo sehemu ya pili, kila anapolala hana raha, kwasababu anajua vitisho ni vilevile anakwenda kukutana navyo. Wengine mpaka inazidi wanasikia sauti kabisa za mapepo, zikiwasemesha, au wanaona vitu vya ajabu vikipita mbele yao, na hiyo yote hutokea pindi tu wanapopitiwa na usingizi kidogo, haijalishi mchana au usiku. Kundi lingine ndio hili ambalo wanaona kama wananaswa, na kitu Fulani pumzi haitoki, wanaishia kutaabika. N.k.

Sasa, unapokutana na mojawapo ya shida, hizo au mashambulizi hayo ndotoni. Jambo la kwanza ‘hupaswi kuogopa’ Fahamu suluhisho ni moja tu nalo ni YESU KRISTO. Lakini wengi hawajui ni kwa namna gani.

Mambo haya matatu (3), yaelewe yatakusaidia..

1) Tumia jina la Yesu.

Unapojikuta kwenye mashambulizi hayo, usiwe tu bubu. Hakikisha unalitumia jina la YESU kukemea. Kuyadhibiti hayo mapepo na kazi zao. Kwasababu mamlaka hiyo umepewa.

Mathayo 10:19  Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.

Lakini ukiona unasumbuliwa na hizo ndoto, halafu unapambana mwenyewe mwenyewe, huna silaha yoyote mkononi mwako, jiandae kukugeuza wewe  kuwa ndio kijiwe chao. Vaa silaha za vita. Jina la Yesu ndio silaha yetu kuu, kutiisha nguvu zote za Yule mwovu.

2) Jiweke vema nafsini, kabla hujalala.

Penda kuwa mwombaji kabla hujalala, usilale tu bila kumkabidhi Bwana usiku wako. Lakini pia hakikisha moyoni mwako, huna makunyanzi ambayo shetani atapata sababu ya kukushitaki. Unajua ni kwanini biblia inasema maneno haya?

Waefeso 4:26  Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; 27  wala msimpe Ibilisi nafasi

Ni kwasababu shetani hupenda mipenyo kama hiyo, kwamfano moyoni mwako una vinyongo na wenzako, una hasira na jirani zao, mambo kama hayo, husababisha adui kukushambulia kwa njia yoyote nyakati za usiku. Hivyo ukabidhi moyo wako kwa Bwana.

3) Zidisha Imani.

Ikiwa mambo hayo mawili unayafanya, lakini bado unaona mashambulizi, yanaendelea. Basi tatizo kubwa kwako lipo kwenye IMANI.  Imani yako ni chache. Upo wakati mitume walipambana na mapepo wakashindwa kuyatoa. Baadaye wakamuuliza Bwana mbona sisi tulishindwa? Yesu akawaambia ni kwasababu ya upungufu wa imani yenu. Hata leo hii ukiona mkristo unasumbuliwa sana na vibwengo, na vipepo. Ujue pia imani yake bado haijawa imara.

Kwa namna gani?

Bado hujaamini vya kutosha nguvu iliyopo ndani ya JINA LA YESU. Na ushindi ulipoupata kupitia Kristo Yesu moyoni mwako. Unachopaswa kufanya ni kumwamini Yesu asilimia mia alimaliza yote msalabani, uwe jasiri, ondoa hofu, vipepo ni vinyago tu, havina chochote cha kukubabaisha wewe. Ukiona hiyo hali inakuja wewe kuwa  ujasiri na Imani yote, usiope kitu. Kemea. “Sema wewe pepo, mimi nimekombolewa na Yesu, huna uwezo wa kushindana na Roho Mtakatifu aliye ndani. Na sasa nisikilize, kuanzia sasa hili sio hekalu lako. Kwa mamlaka ya kifalme iliyo ndani ya jina la Yesu Kristo mwokozi wangu, nakuamuru toka na kwamwe usirudi hapa tena”.

Ukiwa na ujasiri unaotokana na imani ya Bwana unayemtumikia. Nakuambia pepo hilo litabadili uelekeo mara moja, hata likija kujaribu mara nyingine likakukuta na msimamo wako huo huo, hakuna hofu ndani yako. Ndio bye! bye! Halitakaa lirudi tena itakuwa ni historia.

Kumbuka Samsoni alipokutana na Yule Simba, yeye alimwona kama ni “mzinga” tu uliomletea asali. Hivyo akalirarua, na ndio maana baadaye akaja akakuta asali ndani yake akala akaondoka. Kwasababu alijua nguvu zilizo ndani yake, zinatuliza pepo na bahari, na milima  simbuse hichi kisimba-mbarara kinachonguruma hapa mbele yangu.

Na wewe vivyo hivyo, usiishi kinyonge-nyonge tu, unakubali kunyanyaswa nyanyaswa na hivyo vipepo ambavyo havina kitu kwako kama vile huna mtetezi hapa duniani.. KEMEA! KWA IMANI, na Ujasiri. KAZI ITAKUWA IMEISHA!. Wala usitafute maombezi.

Bwana akubariki

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine

IMANI “MAMA” NI IPI?

MAMBO (2) YATAKAYOKUTENGA NA IMANI SIKU HIZI ZA MWISHO.

KUOTA UPO MAKABURINI.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/02/27/kuota-unakabwa-mara-kwa-mara-ni-ishara-ya-nini/