by Admin | 27 February 2024 08:46 pm02
Si kila mtu anayesema “amemwamini” Yesu ni kweli, ameokoka, au amepokea msamaha wa dhambi zake. Ukweli ni kwamba kuupokea msamaha wa dhambi kwa kuiamini kazi aliyoimaliza Yesu Kristo pale msalabani ya ukombozi wa wanadamu si kugumu, Lakini haiji kwa kusema “naamini tu” halafu basi ndio uwe tayari umetiwa muhuri na Mungu kwamba ni wake milele.
Imani ya namna hiyo inatiwa imani ya” bure” (1Wakorintho 15:2).
Na sehemu nyingine inajulikana kama “imani ya wote” ambayo hata mashetani wanayo. Wanamwamini Yesu kuwa ni mwokozi, lakini pia wanaiamini vizuri sana kazi ya msalaba (Yakobo 2:19). Lakini je! Wamesamehewa dhambi zao?
Zipo injili zinazowafundisha watu, “kuamini tu” au “kukubali tu msamaha” inatosha. Hakuna la ziada baada ya hapo. Ndugu hizo sio sifa za mwaminio yoyote.
Neno “kuamini” kwa kigiriki ni PISTIS, lenye maana ya sio tu kuwa na ujasiri na Mungu wako kwa kile anachokupa au kukuelekeza,lakini pia kuwa ‘mwaminifu”.
Maana yake ni kuwa ili tuseme tumeamini ni lazima pia tuwe waaminifu kwa Yule tuliyemwamini.
Sasa mtu yeyote aliyemwamini Kristo. viashiria hivi vitatu(3) utaviona ndani yake
Yohana 10:2 Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo. 3 Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje. 4 Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake. 5 Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni…
27 Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. 28 Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. 29 Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu.
Umeona, ni kondoo tu, ndio hawawezi kupokonywa katika mikono ya mchungaji wake. Lakini mbuzi wanaweza, kwasababu hawategemei sana sauti ya mchungaji, wanaweza kujichunga wenyewe. Ukiona mtu anasema ameokoka, halafu, maisha yake ni kama ya mbuzi, ujue huyo si wa Kristo. Haisikii sauti ya Kristo ikimwelekeza aache maisha ya kiulimwengu, ajitofautishe na watu wa kidunia, . Ujue huyo bado hajapokea kweli msamaha wa dhambi, kwasababu hajaamini. Anapaswa ashuhudiwe mpaka aamini. Na aseme kuanzia leo, Kristo ndio kiongozi wa maisha yangu na sio dunia tena. Akubali TOBA ya kweli.
2. Atakuwa Ni kiumbe kipya.
Yesu alisema..
Yohana 1:12 Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.
13 waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu
Wenye sifa ya kwamba wamemwamini Yesu ni lazima pia wawe wamegeuzwa kuwa watoto wa Mungu, yaani wamezaliwa mara ya pili kwa mbegu isiyo ya kibinadamu, bali ya Mungu mwenyewe.
Na kama tunavyofahamu mtoto hubeba tabia za Baba. Vivyo hivyo mwaminio ni lazima moyoni mwake kuwake, tamaa za Baba yake. Maandiko yanasema Baba ni Mtakatifu, vivyo hivyo tamaa ya mwaminio huyo mpya itakuwa ni kupenda utakatifu, na kuutafuta huo kwa bidii.
Haiwezekani mtu aliyemwamini Yesu, awe na raha tena katika maisha ya kidunia ya dhambi. Au asipige hatua yoyote ya kuutafuta ukamilifu. Halafu tuseme ni mwaminio si kweli.
1Yohana 3:9 Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu
3) Atakuwa ni mwanafunzi
Mwaminio mpya amefananishwa na mwanafunzi, na mwanafunzi sikuzote huwa yupo tayari kujifunza, na kukua kiufahamu.
Matendo 2:41 Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. 42 Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali.
Hivyo mtu yoyote anayesema amemwamini Yesu, na hapendi fundisho, hapendi kuchungwa, hapendi kufuatiliwa maendeleo yake ya kiroho, anapinga ubatizo, na wakati mwingine kufanya ushirika, huyo mtu bado hajaamini.
Lakini akiwa na sifa zote hizo tatu, ni uthibitisho kuwa amemwamini Yesu, na hivyo kaupokea pia msamaha wa dhambi. Mtu wa namna hiyo wokovu kwake ni uhakika. Kwasababu Yesu ameumbika ndani yake. Kazi ya Mungu kamilifu imetimilika ndani ya mwanadamu.
Je! Na wewe Umepokea ondoleo la dhambi zako? Je! Ni mwanafunzi, ni kondoo, ni mwana wa Mungu?. Kama bado basi fahamu unamwihitaji Kristo, fungua moyo wako mkaribishe ndani yako akuokoe. Sasa, Maanisha tu tangu sasa kuwa na badiliko na yeye mwenyewe atakuokoa.
Bwana akubariki.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
NAMNA YA KUITAMBUA SAUTI YA MUNGU INAPOZUNGUMZA NA WEWE
LISHA KONDOO WANGU, LISHA WANA-KONDOO WANGU.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/02/27/viashiria-vya-mtu-aliyesamehewa-dhambi-zake/
Copyright ©2025 unless otherwise noted.