Merikebu ya Iskanderia kwanini itajwe jina lake ‘Ndugu Pacha’?

by Admin | 9 March 2024 08:46 am03

SWALI: Je kulikuwa na umuhimu wowote wa ile merikebu ya Iskanderia  walioipanda Paulo na wafungwa wengine kutajwa jina lake ‘ndugu Pacha’,?

Matendo 28:11  Baada ya miezi mitatu tukasafiri katika merikebu ya Iskanderia iliyokuwa imekaa pale kisiwani wakati wa baridi; na alama yake ni Ndugu Pacha. 12  Tukafika Sirakusa, tukakaa siku tatu. 13  Kutoka huko tukazunguka tukafikia Regio; baada ya siku moja upepo wa kusi ukavuma, na siku ya pili tukawasili Puteoli. 14  Huko tukakuta ndugu, wakatusihi tukae nao siku saba; na hivi tukafika Rumi.


JIBU: Safari ya mtume Paulo kama mfungwa, kutoka Kaisaria kwenda Rumi kuhukumiwa, haikuwa rahisi, iligubikwa na misuko suko mikubwa ambayo ilihatarisha maisha yao ukisoma Matendo 27, utaona mtume Paulo alionywa na Roho Mtakatifu kuhusu hatari hiyo lakini alipomwambia akida na manahodha, walipuuzia agizo lake, kwasababu watu wale hawakuamini habari za “miungu kabisa”. Maandiko yanasema walipoona upepo wa kusi umevuma kidogo tu, unaoruhusu kusafiri, wakadhani itakuwa hivyo mbeleni.

Lakini tunaona walipofika katikati, ghafla ile bahari iliwachafukia sana, upepo wa nguvu ukavuma merikebu yao ikawa karibu na kuzama, baadaye ilivunjika kabisa, na wakaokoka kwa shida kwasababu Mungu alimuhakikishia Mtume Paulo kuwa hakuna hata mmoja wao atakayeangamia.

Walipookoka na kufika kisiwa kile kilichoitwa Melita, walikaa miezi mitatu pale, kuruhusu hali ya hewa kutulia, kabla ya kuondoka. Lakini tunaona walipotaka kuondoka, safari hii wale mabaharia pamoja na maakida, hawakuichukulia safari yao kirahisi rahisi, yaani hivi hivi tu bila uongozo wowote. Ndipo walipojifunza kuchagua merikebu yenye “ulinzi wa kiroho”. Wakaipata hiyo ya Iskanderia iliyokuwa na nembo ya “Ndugu Pacha” kwa mbele.

Ndugu Pacha ni miungu ya kipagani ya kiyunani, ukisoma tafsiri nyingine za biblia imewataja moja kwa moja miungu hiyo kama Castor na Pollux. Ni miungu ambayo waliamini inahusika na ulinzi wa  safari za majini. Hivyo kwa imani yao ya kipagani, wakachukua nembo yao kuonyesha tunaiabudu na kuiheshimu hii miungu, na kutaka iwaongoze  salama katika safari yao, hawategemei tena elimu zao na nadharia zao.

Sasa tukirudi kwenye swali, linalouliza, kulikuwa ni umuhimu gani, hiyo merikebu ya Iskanderia kutajwa hadi nembo yake ya ndugu Pacha. Sababu ndio hiyo, Sio kwamba biblia inatufundisha, na sisi tukaweke miungu ya kipagani, kwenye vyombo vyetu vya usafiri kutuhakikishia ulinzi, hapana!

Bali inatufundisha Safari ya maisha hapa duniani. Kila mwanadamu anasafiri, lakini Je! Katika safari yako ni kitu gani kinakuongoza na kukulinda ili kukufikia ng’ambo yako salama?

Hakuna mwanadamu ambaye anaweza kujiongoza mwenyewe. Na ndio maana utaona hawa kwasababu hawakumjua Mungu wa kweli iliwabidi wakatafuta vinyago visivyoweza kuwasaidia kitu viwaongoze, na kama sio mtume Paulo kuwepo ndani ya Merikebu ile, safari yao ndio ingekuwa mbaya mara mbili zaidi. Hawakujua tu waliongozwa na Kristo Yesu pasipo wao kujua kwa neema tu!. Kwasababu watumishi wa Mungu walikuwa ndani.

Na sisi, hapa tulipo, fahamu kuwa maisha yako, bila KRISTO ni mauti mbele. Shetani hakuwazii mema, wala akili zako mwenyewe hazikusaidii ndugu, hiyo elimu ni kazi bure, huo uzoefu na ujuzi ulionao ni bure rafiki. Unamuhitaji Kristo, yeye ndio awe nembo  ya maisha yako. Mwamini leo akupe msamaha wa dhambi, mwamini leo akuokoe, safari yako iwe salama hapa duniani. Ukifa leo katika hali hiyo, fahamu ni jehanamu moja kwa moja. Umesikia injili ikihubiriwa mara ngapi, kwamba Yesu ni mwokozi lakini unapuuzia? Walio kuzimu wanatamani hata dakika moja, watubu hawawezi kwasababu kule hakuna maisha ya kuishi. Lakini wewe unaishi.

Usikiapo maneno haya, ugeuze moyo wako, umruhusu Kristo leo akuokoe, ikiwa upo tayari kumgeukia Bwana Yesu , na unatamani upate mwongozo wa kimaombi kwa ajili ya wokovu wako. Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo mwisho wa makala hii, bure.

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

NA UPEPO WA KUSI ULIPOANZA KUVUMA KIDOGO,

MAJARIBU MATANO (5) YA MKRISTO.

Kalafati ni nini? (Ezekieli 27:9)

KWANINI DANI ALIKAA KATIKA MERIKEBU.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/03/09/merikebu-ya-iskanderia-ndugu-pacha/