by Admin | 8 May 2024 08:46 pm05
Elewa maana ya mstari huu;
Mithali 10:12 Kuchukiana huondokesha fitina; Bali kupendana husitiri makosa yote.
Mstari huu unalenga kutufundisha sifa za kipekee sana za upendo. Ambazo zinazungumziwa pia sehemu mbalimbali.
Kwamfano hapo anasema kuchukiana hakuzai kingine zaidi ya fitina,( yaani uchongezi, na kudhuriana), lakini upendano husitiri MAKOSA YOTE. Anaposema yote. Ni kweli yote. Endapo upendo utatoka kwelikweli katika kilele chache. Hiyo ndio sifa ya ajabu ya upendo ambayo kitu kingine chochote chema hakiwezi kutoa, kwamfano imani, nguvu, mamlaka, uweza n.k. haviwezi kusitiri “makosa yote”. Ni upendo tu peke yake.
Neno hilo hilo pia limerudiwa katika agano jipya.
1Petro 4:8 Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi
Ndio maana Bwana Yesu alisema Torati yote imelalia hapo, katika kumpenda mwenzako kama nafsi yako, alisema vile unavyotaka wewe utendewe watendee wenzako. Utashangaa tu, wivu unayeyuka wenyewe, hasira inakufa, vinyongo vinaondoka, mashindano yanapotea, wizi, uzinzi unafutika, kwasababu umegundua kuwa mwenzako ni kama hiyo nafsi yako mwenyewe, kama vile wewe unavyopenda kufanikiwa vivyo hivyo usichukie kuona mwenzako amefanikiwa.
Lakini Jambo hili linaweza kutoka ndani yetu kwa njia tatu. Ya kwanza ni kujazwa Roho Mtakatifu. Kwasababu tunda mojawapo la Roho Mtakatifu ni upendo (Wagalatia 5:22). Hivyo unapokuwa mwombaji sana, hususani wa “masaa” sio dakika, unajazwa Roho Mtakatifu vema. Na matokeo yake ni kuwa urahisi wa kuudhihirisha upendo unakuja.
Lakini hilo peke yake halitoshi, unapaswa uambatanishe na usomaji wa Neno kila siku. Neno ni njia nyingine ya Roho Mtakatifu kukukumbusha, yale unayopaswa kufanya, kwamfano ukidhihirisha hasira ukisoma Neno utafunza uvumilivu, utajifunza unyenyekevu, kuachia, na madhara ya kutokusamehe. Hivyo litakufanya uweze kurejea kwenye mstari haraka pale unapokaribia kuteleza. Usipuuzie kusoma Neno kila siku.
Tatu, ni kutendea kazi. Lazima ujiwekee malengo. Kwasababu ukiwa mwombaji tu, na msomaji peke yake bado haitakusaidia sana , kama huna mikakati ya kukifanyia kazi. Ndio maana hapo anasema iweni na JUHUDI nyingi katika kupendana,.Juhudi ni lazima yaani unaanza kuchukua hatua ya kushindana na vipinga-upendo, na hapo hapo utaanza kuona, wepesi umekuja ndani yako,
Sisi kama watoto wa Mungu, tumeagizwa tukue kila siku kuufikia upendo wa ki-Mungu ndani yetu. Ndio ukomavu wetu na kilele cha imani yetu. Kwasababu hii ndio dawa ya dhambi zote.(2Petro 1:5-11)
Bwana atuongezee neema.
Shalom.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Kuhubiri injili kwa husuda na fitina ndio kupi?
UPENDO NI NINI NA JE! KUNA AINA NGAPI ZA UPENDO?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/05/08/maana-ya-mithali-1012-kuchukiana-huondokesha-fitina/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.