MIMI NA WEWE TU KAZI YA MUNGU.

by Admin | 17 July 2024 08:46 pm07

Waefeso 2:10

MAANA TU KAZI YAKE, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.

Nakusalimu katika jina la mwokozi wetu Yesu Kristo, karibu tujifunze maneno ya uzima.

Mimi na wewe kama vile maandiko yanavyosema hapo, ni  “kazi ya Mungu”..Hivyo ni lazima kujua kama ni  kazi ya Mungu basi ni lazima pia tumekusudiwa kutimiza jukumu fulani hapa duniani.

Kwamfano unapoona gari, unasema lile ni kazi ya mtu sio mbuzi.. Na kama ni kazi yake, basi kuna wajibu fulani nyuma yake ambao liliumbiwa lifanye. Na wajibu wenyewe ni kumsafirisha mtu au vitu kwa haraka na wepesi.

unapoona nyumba, tunasema ni kazi ya mtu,  imejengwa kuwa makao ya kupumzika, haijajengwa tu, bila kusudi lolote duniani.

hata unapoona kiota, ile ni kazi ya ndege kakijenga sio kiwe tu pale kama takataka, bali aishi ndani yake.

Vivyo hivyo na sisi ni kazi ya Mungu tuliumbwa kutimiza kusudi fulani. Hivyo ni lazima ujue, na kusudi lenyewe ni KUTENDA MATENDO MEMA.

Sisi ni vyombo mahususi, Mungu alivyovikusudia kudhihirisha matendo mema, ambayo aliyaumba tangu mwanzo yatendwe, hakuna chombo chochote chenye uwezo wa kufanya hivyo isipokuwa mwanadamu.

Waefeso 2:10

MAANA TU KAZI YAKE, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.

Sasa wewe kama mtu usipojua wajibu wako hapa duniani, utakuwa hatarini kuangamizwa. Ni sawa na TV isiyoonyesha kitu, gari lisilotembea, pasi isiyotoa moto. ni wazi kuwa vitatupwa kama sio kuwekwa kwenye karakana.

Na wewe vivyo hivyo, fahamu kuwepo kwako duniani ni kutenda matendo mema. ndio kusudi lako

Sasa, si matendo mema, ilimradi matendo mema…hapana…yapo matendo mema, lakini yasiwe na nguvu mbele za Mungu, hayo ndio yale ambayo mataifa huyafanya..lakini matendo mema tunayoyazungumzia hapa ni yale yaliyo ndani ya YESU KRISTO. Ndio maana hapo anasema tuliumbwa katika Kristo Yesu, sio katika Adamu, au Ibrahimu, au nabii fulani bali Kristo Yesu..maana yake matendo ya Yesu, (au kwa namna nyingine tabia za Yesu) ambayo hakuna mwingine awezaye kuyatenda isipokuwa mtu huyo amezaliwa mara ya pili.

Hivyo leo tutatazama aina ya matendo hayo mema ambayo wewe kama mwana wa Mungu huna budi kuyadhirisha uwapo duniani.

  1. UPENDO

Upendo wa Kristo, sio kama upendo wa kiulimwengu, ule ambao, unawapenda wakupendao hapana..mbele za Mungu hapo bado hujafanya tendo la upendo, huo ni mwanzo tu.

bali ni ule wa kupenda wanaokuudhi, lakini sio kupenda tu, unafikia hatua ya kuwaombea, na unapofikia kilele chake unaweza hata kuutoa uhai wako kwa ajili yao.

Mathayo 5:43-48

[43]Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;

[44]lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,

[45]ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.

[46]Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?

[47]Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?

[48]Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Huu unaitwa upendo wa agape. Mimi na wewe lazima tufanye bidii tuudhihirishe. Ndio ulioumbiwa tangu mwanzo uuonyeshe kwa wengine. Epuka mafundisho ya piga adui zako, kumbuka wewe ni kazi ya Mungu, kuonyesha upendo.

  1.  UTAKATIFU

Yesu alisema haki yenu isipozidi ya waandishi na mafarisayo, hamtaingia kamwe katika  ufalme wa mbinguni.

Mathayo 5:20

[20]Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.

Mafarisayo walikuwa hawana Roho Mtakatifu, hivyo mambo yote waliyatimiza kwa nguvu lakini haikusaidia kuondoa tamaa za mwili. walikuwa hawazini lakini mioyo yao ilikuwa na tamaa. Lakini Yesu alitoa  mizizi ya uzinzi, ndani ya mtu kwa Roho wake mtakatifu anayempa.

Ndio maana kwanini unapaswa ujazwe Roho, lakini pia utembee kwa Roho Mtakatifu ili uweze kuushinda mwili, vinginevyo hutaweza kwa nguvu zao, utafanya kinafiki. Biblia inasema..

Wagalatia 5:16-17

[16]Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.

[17]Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.

Ni lazima ujifunze utii wa Neno la Mungu, kwa kujikana nafsi, na kumfuata Yesu, wakristo wengi hawajikani nafsi, wanakiri wokovu lakini gharama zake hawataki kuingia, wamesilibiwa kweli msalabani lakini hawataki kufa, hawataki kuvunjwa vunjwa miguu yao wafe,. Ukiingia kwa Kristo kubali kufa ili akuhuishe,  ndivyo utakavyoweza kuushinda ulimwengu, kubali kusema bye! bye! kwa ulimwengu. Utaona tu jinsi gani utakavyoweza kuishi maisha matakatifu bila shida yoyote. Roho Mtakatifu huwa anapata nguvu ya kumbadilisha mtu pale ambapo anakubali kujikana kweli nafsi. lakini kama hataki, Mungu kidogo, udunia kidogo, utaendelea kuwa vilevile tu kama mafarisayo na waandishi, ambao vikombe vyao havijasafishwa kwa ndani.

Wewe ni kazi ya Mungu umeumbwa uwe mtakatifu kama yeye alivyo mtakatifu. Kubali tu kuongozwa na Roho kwa kujikana nafsi.

1 Petro 1:16

[16]kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.

3) KUHUBIRI HABARI NJEMA.

Yesu alipokuja duniani, alitambua kuwa vinywa vyetu viliumbwa mahususi, kuwafundisha na kuwaekeza wengine njia iliyo sahihi. Ndio maana mapema tu, alianza kuhubiri na kufundisha katikati ya vijiji na miji, habari za ufalme..Huoni hayo ni matendo mema?

Warumi 10:15

[15]Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!

Halikadhalika hatuna budi kufahamu agizo la sisi kuhubiri, ndilo tuliloumbiwa na Mungu tangu mwanzo tulifanye..ndio agizo kuu. Jambo ambalo lipo kwa wakristo tu. Ni mpango ambao Mungu amekusudia kuutumia kuzungumza, kuponya, kufungua watu kupitia watu hao hao.

Sasa ikiwa wewe umeokoka halafu, huna habari ya kuwashuhudia wengine Injili, fahamu kuwa wewe, sio kazi ya Mungu, uliyeumbwa katika Kristo Yesu. Bali ni kazi ya mwingine.

Amka sasa, ondoa woga na uvivu wa kuwatangazia wengine Kristo, usiwe chombo kibovu, anza kuwatangazia wengine wokovu, uwezo huo upo ndani yako, kushuhudia hakuhitaji elimu yoyote ya biblia au vifungu elfu vya kwenye maandiko, ni kueleza ushuhuda wa maisha yako matendo makuu Kristo aliyokutendea, ushuhuda huo unatosha kumgeuza mwingine, kabla hujafikiria kutoa vifungu anzia kwanza hapo. Ndicho alichokifanya yule kichaa aliyetolewa pepo, Yesu alimwambia nenda kwenu kawashuhidie watu matendo makuu Mungu aliyokutendea, na  kwa kupitia ushuhuda wake taifa zima la Dekapoli likamwamini Kristo, mwanamke msamaria, kusikia tu habari zake zinafichuliwa akaenda kuwaleza watu, samaria yote ikaamini. Hakuna haja ya kuwa na hofu, anza sasa kuwashuhudia ndugu zako.

Wewe ni kazi ya Mungu, umeumbwa ili uhubiri.

4) IMANI

Vilevile Matendo ya imani, tuliumbiwa sisi tangu mwanzo tuyadhihirishe, na ndio maana hatumwoni Mungu kwa macho, tofauti na malaika, kwasababu tumetengenezwa kwa namna hii, haiwezekani wewe kumpendeza Mungu pasina imani.

Waebrania 11:6

[6]Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.

Lakini imani yetu, haina budi kuzidi ile ya watu wa kidunia, ya kwetu huzaliwa na Neno la Mungu, nguvu ya Mungu iliyo katika msalaba wa Yesu.

tukiumwa tunaamini hakika, Yesu alishayachukua magonjwa yetu, huzuni zetu, umaskini, hatuna mashaka kwasababu Yesu alishayamaliza yote. Hatupaswi kuwa na hofu ya maisha, Yesu mwokozi wetu ameshayamaliza.

Kuwa mtu wa imani, liweke Neno la Mungu kwa wingi ndani yako. Mtegemee Kristo, amini kazi zake. Usiishi kwa kuona.

5) MAOMBI

Maombi ni mawasiliano. Sisi kama kazi yake anatazamia, tuwe watu wa kumtegemea kwa asilimia mia, maombi yapo ya aina mbalimbali, sifa ni moja ya maombi, ibada ni aina ya maombi,

Ndio maana Yesu alipokuja duniani, maombi yalikuwa ni sehemu ya maisha yake. Aliomba zaidi ya watu wa kidini, alikesha, akawataka na mitume wake wafanye vile, alisema ombeni nanyi mtapewa, ombeni bila kukoka, dumuni katika sala. (Mathayo 26:41, Wakolosai 4:2)

Wewe ni manukato ya Mungu, Mungu anataka kusikia harufu yako nzuri. Na harufu yenyewe ni Maombi yako.

Ufunuo 5:8  Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu

Vilevile fahamu maombi ni mahali ambapo unampa Mungu nafasi ya kukukarabati wewe kama chombo chake uweze kuzifanya kazi zake vyema. Vilevile Haiwezekani mwanadamu uliyeumbwa kwa mfano wa Kristo kwa wokovu uepuke maombi. Ukifa kimaombi, ni umekufa kiroho, huwezi kuzitenda kazi za Mungu.

6) UMOJA.

Jambo lingine ambalo Mungu anatazamia alione kwako, ni wewe kudhihirisha umoja wa Roho ndani ya mwili wa Kristo. (Waefeso 4:3)

Yesu alisema .

Yohana 17:11, 21

[11]Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. … [21]Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ILI ULIMWENGU UPATE KUSADIKI YA KWAMBA WEWE NDIWE ULIYENITUMA.

Lengo la kufikia umoja ni ili ulimwengu umwamini Kristo. Mahali ambapo tunashindwa kupaelewa sisi kama kazi ya Mungu ndio hapo, yaani kila mtu anataka awe kivyake, au wazo lake liwe bora, tukidhani ndio tuliombwa tuishi hivyo..

halitawezekana, endapo hutatambua nafasi zetu katika mwili wa Kristo ni ipi, kama Mungu hajakupa uongozi, kwanini ung’ang’anie nafasi hiyo?

kuwa katika utumishi wa chini, hakukufanyi karama yako kudidimia, Mungu alimtoa Daudi mazizini, vivyo hivyo yule aliyemkusudia atamwinua tu popote lakini sio kugombani au kumwonea wivu mwenzako awapo kwenye nafasi fulani, hivyo ili tuufikie umoja wa Roho ni kukubali kujishusha kwa kuongozwa, na kufundishwa, na kuridhika na ulichokirimiwa na Bwana.

Tukizangatia matendo hayo. Basi tutakuwa ni vyombo bora, vinavyostahili kutumika kwa kazi rasmi za Mungu ambazo bado hazijafuniliwa..Zitafunuliwa katika huo ulimwengu ujao, Huko ambako jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia.

Jiulize je! Wewe ni chombo kamilifu cha Kristo?

2 Timotheo 2:20-21

[20]Basi katika nyumba kubwa havimo vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali na vya mti, na vya udongo; vingine vina heshima, vingine havina.

[21]Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao, atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana, KIMETENGENEZWA KWA KILA KAZI ILIYO NJEMA.

Hayo ndio matendo yetu mema, yatokayo kwa Kristo Yesu, sio ulimwengu. Fanya bidii kuyatoa ndani yako.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

SI SHETANI BALI NI WEWE. (CHAGUA MEMA)

Ni kama machungwa katika vyano vya fedha.

“Vya Kaisari mpeni kaisari”  ni vipi hivyo tunavyopaswa tumpe?.

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/07/17/mimi-na-wewe-tu-kazi-ya-mungu/