SIFA ZA MAMBA YULE MKUBWA WA AYUBU.

by Admin | 18 July 2024 08:46 pm07

Katika Ayubu 41, tuona Mungu akieleza kwa urefu sifa ya mnyama mamba.

Ametumia taswira ya mamba huyu tunayemwona, kumwelezea mamba wake wa  rohoni, ambaye hasaa Ayubu alionyeshwa habari zake kwa urefu kupitia sura hii.

Na ndio maana kuna sifa nyingine ukizisoma hapo, huwezi kuziona kwa mamba huyu tuliye naye sasa, lakini Mungu hupenda kutumia mifano halisi walau tupate taswira wa kile alichokimaanisha. Ndio maana akaweka sifa chache kwenye mambo wetu huyu ili tumwelewe.

Sasa katika sura hii, Mungu anaanza kwa kumwonyesha Ayubu jinsi anavyomtofautisha sana mnyama mamba na viumbe vingi mbalimbali vilivyopo duniani, kuanzia vya kwenye maji kama vile samaki, mpaka vile vile vya angani kama  vile ndege, hadi wanyama wa kufugwa kama ng’ombe na wale wa mwituni kama vile simba.. Hawa wote hakuna aliyelinganishwa naye.

Mungu anamwonyesha ukali  mwingi alionao, nguvu alizonazo, ugumu ulio katika ngozi yake, kiasi cha mkuki wowote kushindwa kupenya kwenye ngozi yake, zaidi sana ujasiri alioumbiwa. Kwa ufupi kulingana na habari hii hakuna mnyama aliyeweza kulinganishwa na huyu duniani kote.

Sasa embu soma hizi sifa, na mwishoni utamjua mamba huyo ni nani, na uzao wake ni upi. (Zingatia maneno yaliyoandikwa kwa herufi kubwa)

Ayubu 41

1 Je! Waweza wewe KUMVUA MAMBA KWA NDOANA? Au, kuufunga ulimi wake kwa kamba?  2 Je! Waweza kutia kamba puani mwake? Au kutoboa taya yake kwa kulabu?

3 JE! ATAKUSIHI SANA? Au, atakuambia maneno ya upole?  4 Je! Atafanya agano pamoja nawe, UMTWAE KUWA MTUMISHI WAKO milele?

5 Je! UTAMCHEZEA kama ndege? Au, kumfunga kwa ajili ya wasichana wako?  6 Je! Vikosi vya wavuvi watamfanyia biashara? WATAMGAWANYA kati ya wafanyao biashara?

7 Je! Waweza kuijaza ngozi yake na vyuma vyenye ncha, Au kichwa chake kwa vyusa?  8 Mwekee mkono wako; Vikumbuke vile vita, wala usifanye tena.

9 Tazama, kumtamani ni bure; Je! Hatambwaga chini huyo atakayemtazama?  10 HAPANA ALIYE MKALI HATA AKATHUBUTU KUMWAMSHA; Bali ni nani awezaye kusimama mbele yangu mimi?  11 Ni nani aliyetangulia kunipa hata nimlipe? Kila kilicho chini ya mbingu nzima ni changu.

12 Sitanyamaa kusema habari za via vyake, Wala nguvu zake kuu, wala umbo lake zuri.  13 Ni nani AWEZAYE KUMBAMBUA MAGAMBA YAKE? NI NANI ATAKAYEPENYA DIRII YAKE MARADUFU?  14 Ni nani awezaye kuifungua milango ya uso wake? Meno yake yatisha kandokando yake.

15 Magamba yake yenye nguvu ndiyo fahari yake, Yamefungamana pamoja kama kwa kufungwa kwa muhuri.  16 Jinsi yalivyoshikamana Hata upepo hauwezi kupita kati.  17 Yamefungamana pamoja; Yameshikamana, hata hayawezekani kutengwa.

18 Kwa kuchemua kwake mwanga humemetuka, Na macho yake yanafanana na makope ya alfajiri.  19 MIENGE IWAKAYO HUTOKA KINYWANI MWAKE, NA MACHECHE YA MOTO HURUKA NJE.  20 MOSHI HUTOKA KATIKA MIANZI YA PUA YAKE, Kama nyungu ikitokota, na manyasi yawakayo.

21 Pumzi zake huwasha makaa, Na miali ya moto hutoka kinywani mwake. 22 Katika shingo yake hukaa nguvu, Na utisho hucheza mbele yake.  23 Manofu ya nyama yake hushikamana; Yanakazana juu yake; hayawezi kuondolewa.

24 MOYO WAKE UNA IMARA KAMA JIWE; Naam, imara kama jiwe la chini la kusagia.  25 Anapojiinua, mashujaa huogopa; Kwa sababu ya woga wao huvunjwa moyo.  26 Mtu AKIMPIGA KWA UPANGA, HAUMWINGII; Wala fumo, wala mshale, wala mkuki wenye ncha.

27 Yeye huona chuma kuwa kama nyasi, Na shaba kama mti uliooza.  28 Mshale hauwezi kumkimbiza; Na mawe ya teo kwake hugeuka kuwa kama makapi.  29 Marungu huhesabiwa kama mabua; Naye hucheka mshindo wa mkuki ukitupwa.

30 Pande zake za chini ni kama vigae vikali; Hutandika malazi kama kuweka chombo cha kupuria nafaka juu ya matope.  31 Yeye huchemsha kilindi mfano wa nyungu; Hufanya bahari kuwa kama mafuta.

32 Hufanya mapito yake kung’aa nyuma yake Hata mtu angedhani kilindi kina mvi.  33 JUU YA NCHI HAPANA ALIYEFANANA NAYE, ALIYEUMBWA PASIPO OGA.  34 Yeye hutazama kila kitu kilicho juu; Ni mfalme juu ya wote wenye kiburi.

Mamba huyu si mwingine zaidi ya BWANA YESU KRISTO.!

Hakuna ufalme, au mwanadamu, au mamlaka iliyoweza au inayoweza kuutetemesha ufalme wa Kristo, zaidi dunia nzima humuhofu. Yeye sio samaki, yeye ni zaidi ya mamba.

Lakini pia anao uzao wake tofauti na uzao wa viumbe vingine. Na watoto wake watafanana na yeye, ndio wale waliomwamini. Ndio maana ukimpokea Kristo kwa kuzaliwa mara ya pili, unakuwa mtu mwingine kabisa duniani, kwasababu asili yake  inakaa ndani yako.

Ndugu, utaishi kinyonge hapa duniani, mapepo yatakusumbua, dunia itakusumbua kwasababu wewe ni dhaifu, na utaendelea kuwa dhaifu tu kama visamaki vingine vinavyovuliwa-vuliwa tu ovyo na ndoano. Lakini ukimpokea Kristo maishani mwako. Wewe ni mtu mwingine.Rohoni unaogopeka mno.

Embu leo tubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kuziacha, mwambie Yesu naufungua moyo wangu, ingia ndani yangu, na hakika ataingia, na kukusamehe dhambi zako zote, kama hakikisho la uzima wa milele . Atakufanya kiumbe kipya, hakikisha tu unamaanisha kusema kimatendo kuanzia leo YESU ni wangu, mimi ni wake. Hilo tu, kisha nenda ukabatizwe ikiwa hukubatizwa. Baada ya hapo asili yako itabadilishwa. Uwe mamba, umiliki na kutawala sio samaki.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Neno “Via” linamaanisha nini katika biblia?

KWANINI YESU KRISTO NI WA MUHIMU KWETU SASA?

Yesu kuvishwa taji la miiba kichwani, kulifunua nini?

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/07/18/yupo-mamba-mmoja-ni-tishio-duniani/