Yesu kuvishwa taji la miiba kichwani, kulifunua nini?

Yesu kuvishwa taji la miiba kichwani, kulifunua nini?

SWALI: Yesu kuvishwa taji la miiba kichwani alipokuwa anasulubiwa kulikuwa kuna funua nini rohoni?


JIBU: Kila tendo alilotendewa Yesu katika kipindi cha mateso yake lilikuwa lina ufunuo wake rohoni. Tunajua wale askari waliposikia kuwa yeye ni mfalme, muda ule ule walimvisha vazi la kifalme, kisha wakampa fimbo, na baada ya hapo wakasokota taji la miiba, wakamvisha kichwani, kisha wakaanza kumdhihaki, huku wakimpiga wakisema..  Salamu! Mfalme wa Wayahudi!

Yohana 19:2  “Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika vazi la zambarau. 3  Wakawa wakimwendea, wakisema, Salamu! Mfalme wa Wayahudi! Wakampiga makofi”

Tunajua lengo la wale maaskari kumvisha miiba ni kumfanya aumie zaidi, lakini upo ufunuo mkubwa rohoni, pengine kwanini asingevishwa la matambara mabovu, au taji la udongo, au la vyuma vyenye ncha kali, badala yake wakaona miiba.

Kibiblia, miiba, huwakilisha “mahali palipolaaniwa”.

Adamu alipoasi, Mungu alimwambia ardhi imelaaniwa kwa ajili yako, hivyo itatoa miiba na michongoma. Na matokeo yake ni kwamba italimwa kwa shida

Mwanzo 3:17 Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako;  18 michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni;

Ndio maana shamba ambalo  halipaliliwi  au halitunzwi, matokeo yake ni kuwa linatoa miiba.

Mithali 24:30 Nalipita karibu na shamba la mvivu, Na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili.  31 Kumbe! Lote pia limemea miiba; Uso wake ulifunikwa kwa viwawi; Na ukuta wake wa mawe umebomoka.  32 Ndipo nilipoangalia na kufikiri sana; Naliona, nikapata mafundisho.  33 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi! 34 Hivyo, umaskini wako huja kama mnyang’anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha

Na vivyo hivyo rohoni, mioyo yetu inafananishwa na mashamba. 

Ukisoma ule mfano wa mpanzi, utaona mbegu(Neno la Mungu), lilipopandwa, zipo ambazo ziliangukia kwenye miiba (yaani mahali ambapo hapajafyekwa na kupapaliwa), ndipo pale kwenye miiba, na mwishowe zikakua na kumea. Lakini zikasongwa na ile miiba hazikashindwa kuzaa.

Yesu akatoa tafsiri yake, akasema, miiba ile ni “anasa, udanganyifu wa mali, na shughuli za ulimwengu huu”.

Luka 8:14  “Na zilizoanguka penye miiba ni wale waliosikia, na katika kuenenda kwao husongwa na shughuli na mali, na anasa za maisha haya, wasiivishe lo lote”.

Sasa Yesu alipokuja kufa msalaba, alishughulika na jambo hilo kubwa, kubeba laana hiyo kubwa kwenye kichwa chake.

Akimaanisha kuwa ile nchi iliyolaaniwa (yaani mioyo wa mtu), kuanzia sasa ni mwisho. Imekwisha.

Miiba iliyokuwa inatoka mimi nimeichukua kichwani mwangu.

Moyo wa mtu kuanzia sasa, utaanza kuzaa matunda, na wala hautasongwa na anasa, wala udanganyifu wa mali, wala shughuli za ulimwengu huu, usiivishe chochote.

Hii ikiwa ni kweli kabisa.

Sisi tunaomwamini Yesu, moja kwa moja tunapewa UWEZO wa kufanyika watoto wa Mungu (Yohana 1:12), na matokeo ya uwezo huo ni kuwa,  nguvu ya kusongwa na ulimwengu inakuwa ndogo, kwasababu Roho Mtakatifu aliyemwagwa ndani yetu anatusaidia, Kuukataa ulimwengu, na kuishi maisha ya utauwa. Utakuwa ulimwenguni lakini, hutasongwa na mambo yake. Kwasababu utafundishwa pia “kiasi” na Roho Mtakatifu.

Hivyo uwezo huu utakuja ndani yako, pindi tu unapomgeukia Kristo kwa kumaanisha kabisa, ambapo panaanza na kwa KUTUBU kwanza dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kugeuka,na kumfuata Kristo tangu huo wakati, na kisha kubatizwa, na kupokea Roho wake. Lakini nje ya hapo, huwezi kwenda popote.

Je! Umempokea Yesu?

Pasipo yeye huwezi ndugu kuushinda ulimwengu kwa nguvu zako, haiwezekani hata kidogo, hata ufanyeje haiwezekani,miiba itakusonga tu, dunia itakulemea tu, Unahitaji nguvu zake, kwa Roho wake Mtakatifu. Ili kuzipata maanisha tu kumgeukia,  na kusudia kutembea naye moyoni mwako.

Utaushinda huu ulimwengu. Wala hakuna mwiba wowote utakaomea kwenye moyo wako. Kwasababu Kristo alishayakomesha yote. Je! upo tayari kuokoka leo? Basi fungua hapa kwa mwongozo wa kimaombi>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

SHAMBA HUWA HALIMTAMBUI WALA KUMSUBIRIA MKULIMA.

Marhamu ni nini? Na Manukato ni nini?

Je vazi alilovikwa Bwana Yesu lilikuwa la Zambarau au Jekundu?

Mbaruti ni mmea gani? (Mathayo 7:16)

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments