FAHAMU SEHEMU NNE (4)  APANDWAPO MWAMINI.

FAHAMU SEHEMU NNE (4)  APANDWAPO MWAMINI.

Shalom.

Sisi kama waamini tunafananishwa na mche, au zao Fulani linalopandwa. Kwamfano ukisoma

Zaburi 1:1-3 Inasema..

1 Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. 

2 Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.

3 NAYE ATAKUWA KAMA MTI ULIOPANDWA KANDOKANDO YA VIJITO VYA MAJI, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.

Hii ni kufunua kuwa mtu yeyote mwenye haki (Aliyeokoka), huwa anapandwa mahali Fulani rohoni.

Sasa ni vema kufahamu maeneo Mungu aliyoyaruhusu/ aliyoyakusudia sisi tupandwe, na hii ni muhimu kujua ili tuwe na amani, kwasababu wakristo wengi wanapoona kwanini baadhi ya mambo yapo hivi, huishia kurudi nyuma, au wengine kukata tamaa kabisa, au wengine kupoa, na wengine kulegea legea. Lakini kwa kufahamu haya, nguvu mpya itakuja ndani yako.

Hizi ni sehemu nne (4), Ambazo sisi kama waamini tunapandwa.

1) TUTAPANDWA PALIPO NA  MAGUGU

Mathayo 13:24  Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake;

25  lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.

26  Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu.

27  Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu?

28  Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye?

29  Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo.

30  Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.

Ukiendelea mbele mstari wa 36-43, utaona Yesu anatolea ufafanuzi, wa mstari huo akisema hizo mbegu njema ni wana wa Ufalme, na konde hilo ni ulimwengu, na magugu ni wana wa ibilisi. Hivyo vyote viwili vimeruhusiwa vimee katika shamba hilo hilo moja la Mungu. Vishiriki neema sawa sawa, lakini mwisho, ndio vitofautishwe.

Kufunua kuwa tumewekwa pamoja na waovu, kamwe hatutakaa tuwe sisi kama sisi tu duniani, na hivyo basi tuwe tayari kusongwa na shughuli zao mbaya, kuudhiwa nao wakati mwingine, tuwapo kazini, majumbani, mashuleni, na wakati mwingine hata makanisani, watakuwepo. Na kibaya zaidi tuwe tayari kuona wakibarikiwa kama sisi tu tubarikiwavyo, watapokea mema yote kama tu wewe, kwasababu mvua ileile inyweshayo kwako itawapata na wao.

 Lakini Bwana anataka nini?

Anataka tuwapo katika mazingira hayo ya watu waovu tusifikirie kujitenga, na kutafuta mahali petu wenyewe tuishi, Yesu alisema Baba siombi uwatoe ulimwenguni, bali uwalinde na Yule mwovu, Bwana atakata tuwapo katikati yao tuzae matunda ya haki, kama Danieli alivyokuwa Babeli kwa wapagani, kama Yusufu kwa Farao, kama Kristo kwa ulimwengu. Vivyo hivyo na wewe kwa mume/mke wako asiyeamini, kwa majirani zako wachawi, kwa wafanyakazi wenzako walevi. Angaza nuru yako usijifananishe na wao, wala usingoje siku utengwe nao, jambo hilo linaweza lisitokee. Hivyo weka mawazo yako mengi katika kuangaza Nuru kuliko kutengwa na waovu. Kwasababu ni mapenzi ya Mungu tuwepo miongoni mwao.

2) TUTAPANDWA KATIKATI YA MITI MINGINE MEMA.

Bwana Yesu alisema tena, mfano huu;

Luka 13:6  Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate.

7  Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu?

8  Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi;

9  nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.

Tafakari huo mfano, Mtu huyu alikuwa na shamba la mizabibu tu! Lakini akajisikia moyoni mwake apande na mti mmoja wa TINI katikati ya shamba lake. Matokeo yake ni kwamba ule mtini ukagoma kuzaa. Baadaye  akataka kuukata. Akitufananisha na sisi. Upo wakati utapandwa katikati ya jamii nyingine ya watu. Na Mungu atatarajia uzae matunda yaleyale ya wokovu wako uliopokea mwanzo. Je! Utafanya hivyo au utalala?

Hili ni jambo ambalo linawaathiri waamini wengi, pale panapohama na kwenda ugenini, mfano labda kasafiri kaenda mkoa mwingine, sasa kwasababu kule hakuna wapendwa wa namna yake, basi anaamua kuwa vuguvugu hamzalii Mungu matunda yoyote, kwasababu kule  hawapo wakristo. Mwingine amesafiri nje ya nchi. Mbali sana na watu wenye imani ya Kristo. Kwasababu yupo kule anasema mimi nipo peke yangu, siwezi kufanya lolote la Kristo. Ndugu usifikiri hivyo, Bwana anakutaka uzae matunda sawasawa, bila kuangalia ni wewe tu peke yako upo hapo. Kama ni kuwashuhudia wengine habari njema, wewe fanya. Timiza wajibu wako, usiangalie kundi au dhehebu, au jamii nyingine ya waamini waonaokuzunguka. Wewe timiza wajibu wako hivyo hivyo. Bwana akuone unazaa. Kwasababu kwa namna moja au nyingine hatuwezi kuyaepuka mazingira mapya, ambayo tutajikuta tupo sisi tu wenyewe. Tufanye nini? Kumbuka tu mtini ulio katikati ya mizeituni. Usiwe mlegevu.

3) TUNAPANDWA  JUU YA MITI MINGINE.

Tofauti na sehemu mbili za kwanza, ambazo ni katikati ya magugu, na katikati ya miti mingine. Lakini pia tunapandwa juu ya miti mingine. Hii ikiwa na maana, “tunapachikwa” juu ya mti uliokatwa. Wana wa Israeli, walifananishwa na mzeituni halisi, na sisi mataifa mizeituni mwitu. Hivyo wao walipoikataa neema, basi wakakatwa,tukapachikwa sisi, neema ikatufikia pia.

Warumi 11:17  Lakini iwapo matawi mengine yamekatwa, na wewe mzeituni mwitu ulipandikizwa kati yao, ukawa mshirika wa shina la mzeituni na unono wake,

18  usijisifu juu ya matawi yale; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe

Na hivyo hapa tulipo tumepachikwa juu ya shina lingine. Na hivyo yatupasa tuwe makini, na kuuchukulia wokovu wetu kwa kumaanisha  sana, kwasababu na sisi tusiposimaa tutakatwa. Mhubiri mmoja wa Injili wa kimataifa aliyejulikana kwa jina la Reignhard Bonnkey, mwanzoni mwa huduma yake, Mungu alimwambia nenda kanitumikie, yeye akawa anasua-sua, Mungu akamwambia neema hii niliyokupa alipewa mwingine akaikataa, na hivyo itaondoka kwako na kwenda kwa mwingine usipotii. Aliposikia vile alikubali kutii kwa moyo wote, akaenda kuhubiri injili. Kuonyesha kuwa sisi ni wa kupachikwa, sio shina. Tuipokee neema kwa kuogopa na kutetemeka (Wafilipi 2:12). Usiwe mkristo vuguvugu, tumia muda wako vema, mzalie Mungu matunda. Kwasababu ulipachikwa tu, kwa kosa la mwingine.

4) TUNAPANDWA KWENYE UDONGO ULIORUTUBISHWA SANA.

Fuatilia habari hii,

Marko 11:12  “Hata asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa.

13  Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini.

14  Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia”

Kama tunavyoifahamu hiyo habari asubuhi yake Bwana Yesu alipopita karibu na njia hiyo, ule mti ulionekana umekauka kabisa kabisa. Lakini swali la kujiuliza ni kwanini aulaani, wakati haukuwa msimu wake wa kutoa matunda? Mbona ni kama ameuonea tu?

Ukweli ni kwamba Yesu aliona mti ule kwa mazingira uliokuwepo ulistahili kuwa na matunda hata kabla ya msimu. Kwa namna gani, chukulia mfano wa mazao ambayo yanastawishwa  kwa kilimo cha kisasa, mfano “banda kitalu”(green house), kulingana na matunzo yake, huwa yanastawi kwa haraka na kuzaa ndani ya muda mfupi. Kwasababu yamerutubishwa sana, kwa madawa na mbolea na kuwekewa mazingira rafiki mbali na wadudu waharibifu, mfano wa kuku wa kisasa, ndani ya wiki 6 wamekomaa, lakini matunzo yao hayawezi kama ya wale kuku wa kienyeji ambao wanaachwa wakajitafutie.

Sasa fikiri kama muda wote huo unapita halafu hawazai/hawakui, wanafanana na wale wa kienyeje, ni nini watarajie? Kama sio kuondolewa.

Ndivyo ilivyo kwetu sisi, tunapookoka, muda huo huo tunapokea ROHO MTAKATIFU. Huyu ndiye anayetupa uwezo na nguvu, ya kumshuhudia, na kuzaa matunda ya haki. Hivyo hatuhitaji tena kusubiri mpaka miaka Fulani ipite kama watu wa zamani, ambao walikuwa bado hawajakaliwa na Roho. Bali wakati huo huo tunapookoka na sisi tunawafanya wengine kuwa wanafunzi.

Hatupaswi kujiona sisi ni wachanga kiroho, au watoto, Bwana atakuja ghafla akikosa matunda atatuondoa, na sisi tutabakia kudhani wakati ulikuwa bado.

Hivyo ndugu, fahamu kabisa tayari tumesharutubishwa, usingoje wakati Fulani ufike, hapo hapo fanya jambo kwa Bwana, waeleze wengine habari ya wokovu wamjue Mungu. Wataokoka, usihofu kiwango chako cha kujua maandiko, anayewashawishi watu ni Mungu na sio wewe. Hivyo hubiri kwa ujasiri na Mungu atakuwa na wewe.

Bwana akubariki.

Kwa kufahamu sehemu hizo kuu nne (4), itoshe kutukumbusha mwenendo wetu hapa duniani, uzidi kuwa katika uvumilivu, hofu, wajibu na bidii. Ili tusijikwae, au kufa moyo.

Maran Atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

UTENDAJI KAZI MWINGINE WA ROHO MTAKATIFU USIOUFAHAMU

SIRI YA KUASI KATIKA KANISA LA MUNGU.

JE! WEWE NI MBEGU HALISI YA KRISTO?

UFALME WA MUNGU HAUPATIKANI KIRAHISI.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments