SIRI YA KUASI KATIKA KANISA LA MUNGU.

SIRI YA KUASI KATIKA KANISA LA MUNGU.

Yapo mambo umeshawahi kujiuliza ni kwanini, hayaishi kutokea kila kukicha katikati ya kanisa la Mungu hususani kwa watu wanaosema wao ni watumishi wa Mungu. Utaona leo kunatokea vituko hivi kesho vile, leo mmoja ananaswa kwenye jambo hili baya, kesho lile, sasa mambo kama hayo ukiyaona usianze kuunyooshea ukristo wote kidole au watumishi wote vidole, badala yake uogope kwasababu mlengwa ni wewe na usipojua sababu ya hayo mambo kuzidi kukithiri sana hususani katika kipindi hichi cha mwisho , utajikuta umetumbukia katika shimo ambalo hutajua ni lini umeingia humo..

Embu fuatilia mazungumzo haya dada huyu aliyonitumia kisha tutaendelea..

“mimi (…..) napenda kuuliza Hivi ni sahihi kwa mtumishi unayetumiwa na Mungu kufanya vituko kwa makusudi kwa kujinadi kwamba utatubu? Hii inanipa shida nafsini maana sielewi

Kwani kuna jambo kwa huyu mtumishi ambaye ndo aliyekua akinifundisha mambo ya kumjua Mungu kwa aliyoyafanya nilikata tamaa nikawa naenda tu kanisani lakini sina imani hata na wachungaji tena. nahisi nao watakua hivyo hivyo japokua natamani sana nikae kwenye mstari lakini nikikumbuka matukio mabaya nasikilizia tu neno ibadani lakini hayakai kabisa, nahitaji msaada zaidi kimaombi peke yangu siwezi mtumishi.

Kwanza huyu mtumishi ni mchafu kwenye mitandao pia ni mzinzi sana yani mno sasa kwa mimi ambaye ni mchanga kiroho nashindwa kuelewa ukimuonya ndio hayo anakujibu usimnyoshee kidole mtumishi wa Mungu utapata ukoma kamuulize Miriamu kilimpata nini.

nilimuuliza inakuaje unajua kabisa uzinzi ni dhambi au matusi ni dhambi alafu unafanya kwa makusudi?

akajibu hakuna mchungaji ambaye hajawai kuanguka na bado wanaendelea kuanguka, ndo nikamwambia kwahiyo wewe unawaiga hao? Mungu sio mjomba wako akasema Mungu ni wa rehema kila wakati, mtu anafanya dhambi anatubu anaendelea mbele nikasema naenda kumwambia mchungaji wako na askofu wako akasema ole wangu nikamharibie kule maana wana mwamini sana na hawajui mwenendo wake upoje na yupo kanisa moja la TAG mahali fulani hivi kule (……..).

natamani sana wachungaji wake wamjue tabia zake asiendelee kuchafua kanisa ndio sielewi nifanyeje.

Yananipa shida moyoni.” Naomba msaada.

***mwisho***

Watu wengi wanashindwa kuendelea mbele na Mungu wao kwa kuwatazama watu wa namna hii, Na hicho ndicho shetani anachotafuta kwako hata wewe usomaye ujumbe huu. ni kweli wanakatisha tamaa, na sio tu kukatisha tamaa bali pia wanawakosesha watu wengi waliowachanga kiimani jambo ambalo Bwana YESU anasema “Ingewafaa zaidi kwa watu wa namna hiyo jiwe la kusagiwa lifungiwe shingoni mwao, wakatupwe baharini kuliko kuwakosesha wadogo hao”.. wadogo wanaozungumziwa hapo ni watu wadogo katika imani (wachanga)/ wanyenyekevu…

Lakini je suluhisho ni nini?..Ni kuwanyoshea watumishi wote wahubirio injili vidole?..Hapana tukifanya hivyo tutajikuta tunapoteza hata vile vizuri Mungu alivyokusudia tuvipate katika Mwili wake [ambalo ndio kanisa lake]. Lakini uzuri ni kwamba Jambo kama hilo Bwana alishakwisha kuliona na kulitolea ufafanuzi uliobora zaidi embu tusome hapa kwa pamoja:

Mathayo 13:24 “Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake;

25 lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.

26 Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu.

27 Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu?

28 Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye?

29 Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo.

30 Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.”

Tukizidi kusoma tunaona Bwana akitoa tafsiri yake kama ifuatavyo: 

“Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu;

38 lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu;

39 yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika.

40 Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia.

41 Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi,

42 na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

 

Ndugu fahamu tu jambo moja Mungu ameruhusu kwa makusudi kabisa, watu wote waovu na wema wote wamee kwa wakati mmoja katika kanisa lake kwa kila kizazi, haijalishi ni wazinzi, au walevi, au washirikina wote, au waabudu sanamu, n.k. wote wameruhusiwa wawepo katikati ya watakatifu, wote waabudu pamoja kana kwamba wote wamekubaliwa na Mungu, karuhusu wote wapokee vipawa vya roho, wote watoe unabii, wote wahubiri, wote wafundishe, wote waponye magonjwa, wote watoe mapepo,. Na wala kusiwe na chochote cha kuwadhuru..Hiyo ni SIRI KUU..Biblia inaiita SIRI YA KUASI. Wote Wameruhusiwa pia kusimama madhahabuni kufundisha, hivyo hilo pia lisikupe shida,..

Magugu na ngano vyote vipokee mbolea ya ardhi na mvua kutoka kwa Mungu..Hivyo si ajabu hata kuwaona wanaombea hata wafu wanafufuka lakini Mungu hawatumbui. 

Kwanini Bwana hataki kuwang’oa sasa?. Tukirudi kwenye ule mfano wa magugu na ngano tunaweza kuendelea kujifunza kitu, 

kwa mfano mbegu zozote wakati zikiwa changa ni ngumu sana kuzitofautisha zipi ni ngano na yapi ni magugu mpaka zitakapokomaa ndio utajua kiwepesi, kadhalika pia unaweza ukang’oa magugu yote kumbe hujui kuwa zipo mbegu nyingine za magugu zilikuwa zimefukiwa chini hazijamea vizuri, na ukajikuta umeziacha zile..Hivyo ili zote uzipate kiwepesi bila kubakisha hata moja itakupasa uwe mvumilivu kidogo ungoje kwanza kipindi fulani kipite zote zichipue, kubwa na ndogo. Ili sasa uzitoe zote kiwepesi na mara moja, kwasababu utakuwa una uwezo wa kuzitofautisha.

Na vivyo hivyo waovu na wema katika hatua za awali huwezi kuwatofautisha katika kanisa la Mungu, lakini kwa jinsi siku zinavyozidi kwenda mwisho wao utawaweka wazi wote..Ndipo hapo watakapokuja kukusanywa wote na kutupwa katika lile ziwa la moto. Siku ile ndio lile kundi la Bwana! Bwana! Hatukutoa unabii kwa jina lako?, hatukufufua wafu? Hatukufanya miujiza mikubwa n.k??..Litakapomfuata Bwana. Lakini Bwana atawakana dhahiri..na kuwaambia siwajui nyinyi tokeni kwangu nyinyi mtendao maovu.

Watu wa namna hiyo ni mahususi kabisa wamepandwa na shetani kuliharibu shamba la Mungu. Ni ule UZAO WA NYOKA wenyewe. Na wanajua kabisa mtu yeyote aliye muhubiri atapata hukumu iliyokubwa zaidi kuliko wengine endapo atayahalifu mapenzi ya Mungu lakini wao hata hawaogopi kufanya, wanaendelea tu!..Huo ni uzao wa nyoka. Wanageuza kazi ya Mungu kuwa biashara, huku hofu yoyote ndani yao kuwalipisha watu pesa ili wapate huduma ya kiroho. Ni washirika kanisani lakini bado wanakwenda kwa waganga wa kienyeji, na wengine ni wachawi.. Wanafanya mambo ya ajabu kwa siri huwezi kuwagundua, lakini siku ile watajulikana.

Wanafahamu kabisa hakuna mlevi yoyote atakaye urithi ufalme wa mbinguni lakini wanakunywa pombe, na wakati huo huo bado utawakuta katika vikundi vya maombi, utawakuta wanahubiri, utawakuta wana imba kwaya, utawakuta wanahudumu kanisani, utakuwa ni manabii, ni waalimu na ni wachungaji, lakini bado matusi wanazidi kutukana.. Wanafanya jina la Mungu linatukanwa, si ajabu kwasababu ndio utumishi shetani aliowaitia huo.

Ni UZAO WA NYOKA..kama Bwana alivyosema.. “Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehanum? Mathayo 23.33”……Ni Wana wa shetani waliopandwa mahususi na ibilisi kuliharibu shamba la Mungu.

Hivyo wewe unayesoma, usiache unyofu wako na usafi wako uliokuwa umeuanza kwa kuutazama tu uzao wa nyoka katika kanisa la Mungu na kutetereka . Usitishwe na wao kwasababu uzao huo haukuanzia siku za mitume tu hapana, bali chimbuko lake lilitokea tangu Edeni, pale tu Hawa alipokubali kudanganywa na nyoka na kula tunda, kisha baadaye akaenda kula na mume wake. na ndio maana ndani ya tumbo la Hawa kulionekana watoto wawili Kaini na Habili…Mmoja uzao wa Nyoka na mwingine Uzao wa Adamu, tunafahamu habari ilivyokuwa jinsi Kaini alivyokuwa mwovu kwa tabia zake, na ndivyo ilivyo katika kanisa la Kristo

Mtume Paulo aliandika haya kwa uweza wa Roho..

2Wakorintho 11: 2 “Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi.

3 Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo”.

Unaona, Sisi tuliposwa kwa Kristo [mfano dhahiri wa Adamu ]kama bikira safi lakini lile JOKA ibilisi akapanda mbegu zake chafu katika kanisa la Kristo ambalo linafananishwa na Hawa,. Na hivyo mpaka sasa kumetokea watoto wawili KAINI na HABILI..kwenye kanisa…Kaini ndio hawa wakristo-wa-uwongo.

Lakini mtume Paulo anatushauri tusiuache unyofu na usafi wa Kristo. Hivyo huu si wakati wa kulelemaa tu, kwa kufuata kila wimbi la mafundisho yanayokuja mbele yako. Bali ni wakati wa wewe binafsi kujitathimini, je! umesimama katika IMANI,? Je! Kristo akirudi leo utakwenda naye? Je! wewe binafsi upo katika utakatifu? Ambao biblia inasema pasipo huo hakuna mtu atakayemwona Mungu?(Waebrania 12:14) Je! unayashika maagizo yake?…Usisimame kwa niaba ya mwingine! Simama wewe kama wewe Kama ukijifunza kuenenda kwa utaratibu huo basi shetani hataweza kukunasa hata akija na wimbi kubwa kiasi gani la watumishi wake wa uongo, au mafundisho yake ya uongo, hata kupata kwasababu umejengwa juu ya mwamba imara YESU KRISTO.

Ubarikiwe sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments