SHAMBA HUWA HALIMTAMBUI WALA KUMSUBIRIA MKULIMA.

SHAMBA HUWA HALIMTAMBUI WALA KUMSUBIRIA MKULIMA.

Karibu tujifunze hekima, zilizo katika Neno la Mungu, Tukisoma Mithali 4:30-34 inasema..

30 “Nalipita karibu na shamba la mvivu, Na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili.

31 KUMBE! LOTE PIA LIMEMEA MIIBA; Uso wake ulifunikwa kwa viwawi; Na ukuta wake wa mawe umebomoka.

32 Ndipo nilipoangalia na kufikiri sana; Naliona, nikapata mafundisho.

33 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi!

34 Hivyo, umaskini wako huja kama mnyang’anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha”.

Sulemani anaeleza, tukio alilokutana nalo katika shamba la huyu mtu ambaye alimtambua kama mvivu, Na tukio lenyewe lilimtafakarisha sana.. Yeye alidhani, kwa kulala kwake, na  kuchelewa kwake kulilima shamba lake, basi ndio litabakia vilevile, bila chochote kuwepo juu yake. Lakini kilichomstaajabisha ni kuona mazao mengi sana, tena makubwa yaliyostawi, lakini hayakuwa yale aliyoyapanda bali ni miiba.

Kuonyesha kuwa shamba halimsubirii wala halimtabui mkulima, kazi yake ni kuchepusha chochote kile kinachokuja kupandwa juu yake.. Kama ni mchicha, kama ni gugu, kama ni mwiba, kama ni mbigili, kama ni bangi, kama ni tumbaku, haijali kipandacho, hiyo ndio tabia ya shamba lolote Maandiko yanasema hivyo katika (Marko 4:26-29)

Hivyo mtu asipowajibika mwenyewe, kusafisha shamba lake, na kuhakikisha, anayatoa yale yasiyostahili, au analipalilia mara kwa mara, ajue kuwa ataangukia hasara, na mwisho wa siku kazi yake inakuwa bure. Sikuzote kazi nzito ya ukulima ipo katika kupalilia na kulitunza shamba, dhiki ya wavamizi, na magugu, na sio katika kupanda. Kwasababu kupanda kunaweza kuchukua siku moja au mbili basi. Lakini kulitunza shamba ni jambo lingine, linalomgharimu mkulima, kila siku awe anaamka asubuhi na mapema, na mara kwa mara kulitembelea shamba lake, kulitazama na kulipalilia.

Hii ikifunua nini?

Mioyo yetu ni mashamba..Chochote kinachopandwa iwe na Mungu, au ibilisi, au mwanadamu, ni lazima kimee tu, tupende  tusipende.. Hapo ndipo umakini unapohitajika sana, Hii ndio sababu kwanini maandiko yanasema, tuilinde mioyo yetu kuliko yote tuyalindayo (Mithali 4:23). Kwasababu chochote kile kinamea.

Hivyo, ikiwa huna tabia ya kuutazama tazama moyo wako, basi rohoni unatafsirika  kama mvivu wa hali ya juu, unalala,  pale unaposema, aaa, kesho nitasoma Neno, wiki ijayo, nitakwenda Ibadani, hujui kuwa shamba lako (moyo wako), unamea miiba  usiyoijua wewe na viwavi kila siku…

Ndugu kusema nimeokoka tu, hakutoshi, ni lazima kila siku uhakikishe umeongeza jambo jipya katika maisha yako ya kiroho, jiulize, je! Lile Neno ulilohubiriwa au ulilolisoma, umeliishi vipi katika siku yako, au wiki yako yote. Ni lazima ufanye hivyo kila siku.  Usijisahau, ukawa unaikumbuka roho yako, jumapili kwa jumapili, hiyo ni hatari kubwa sana,..Hata hiyo ibada haiwezi kukusaidia chochote, kwasababu magugu ni mengi kuliko ngano, hivyo utalemewa tu, ukristo wako utakuwa ni mzito sana..

Kama hujui kila inapoitwa leo shetani anaturushia mbegu zake mioyoni mwetu, unapopita barabarani na kusikia miziki ya kidunia, unapokuwa ofisini na kusikia lugha za mizaha kwa wafanyakazi wenzako, hizo ni mbegu, unapokuwa shuleni na kusikia matusi kwa wenzako, unapofungua tv, internet, whatsapp, youtube, na kuona mambo yasiyokuwa na maadili, zote hizo ni mbegu, ambazo kama usipozushughulikia mapema ndani ya siku, zitamea tu, haijalishi wewe ni nani…

Hivyo tunazishughulikia , kwa kusali kila siku, kutafakari maneno ya uzima, kujitenga na uovu, kukaa katika utulivu, kuomba rehema, na kujizuia sana. Tukizingatia haya kila siku. Basi mbegu halisi za Mungu tu, ndio zitakazokuwa zinamea mioyoni mwetu. Na matokeo yake tutakuja kula matunda yake baadaye.

Hivyo tusiwe watu, wa kukumbushwa kumbushwa habari za maisha yetu ya kiroho, tuamke usingizini, tuondoe uvivu, tukayatazame mashamba yetu kila siku. Anza sasa kuwajibika kwa kila kitu kinachoukaribia moyo wako, ikiwa hakimpendezi Mungu, hakikisha unashughulika nacho, hadi kiondoke.

Waefeso 5:14 “Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza.

15 Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima;

16 mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu.

17 Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana”.

Bwana atusaidie.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NI NANI ATAKAYEUCHUKUA MSALABA WA YESU?

MWENGE WAKO WA UHURU UPO WAPI?

AINA TATU ZA WAKRISTO.

Kwanini Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake wasichukue chochote isipokuwa fimbo tu?

UTENDAJI KAZI MWINGINE WA ROHO MTAKATIFU USIOUFAHAMU.

Wakati wakina Shadraka wanatupwa katika tanuru la moto, Danieli alikuwa wapi?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments