MWOMBENI BWANA WA MAVUNO APELEKE WATENDA KAZI.

by Admin | 5 September 2024 08:46 am09

(Masomo ya kanuni za kuomba).

Mathayo 9:38 “Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake”.

Maombi ni jambo kuu na la msingi sana.

Hapa biblia inasema TUOMBE (Bwana apeleke watenda kazi).

Kumbe Maombi ya kuomba uamsho wa watenda kazi ni muhumu!. Kwasababu hiyo basi ni lazima tujiwekee utaratibu wa mara kwa mara kuomba Bwana aongezee watenda kazi.

Na yafuatayo ni baadhi ya maeneno yanayohitaji watenda kazi zaidi.

1.KANISANI.

Hii ni sehemu ya kwanza inayohitaji watenda kazi. Waalimu wa madarasa ya jumapili wanahitajika zaidi ndani ya kanisa, halikadhalika waalimu wa watoto, pia watendakazi katika kuongoza sifa na maombi na wengine wengi.

Hivyo ni muhimu kutenga muda wa kutosha kumwomba BWANA anyanyue watenda kazi yeye anajua yupi anatafaa mahali fulani sisi kazi yetu ni kuzidi kumsihi Bwana awanyanyue wengi.

2. MASHULENI.

Shule kuanzia zile za awali (chekechea) mpaka zile za juu (vyuoni) panahitajika sana watenda kazi, watakaofanya kazi ya mavuno..

Hivyo ni muhimu watu wa Mungu kuomba ili Bwana anyanyue jeshi la watenda kazi (wahubiri) kwenye mashule.

Kwani mbali na mambo mazuri yanayopatikana mashuleni lakini.huko huko pia ndio kitovu cha watoto kujifunza tabia chafu na kupokea maroho ya mapepo.

Na wakati mwingine ni ngumu mtu wa nje kuwafikia na kuwahubiria, hivyo mimi na wewe tukisimama kumwomba Bwana anyanyue watenda kazi katikati yao, basi Bwana atatusikia na kunyanyua vijana miongoni mwao huko huko waliko ambao watawatengeneza wenzao au atawanyanyulia walimu miongoni mwa walimu wanaowafundisha na watawafundisha na kuwakuza kiroho.

3. MAHOSPITALINI.

Hii ni sehemu ya tatu inayohitaji watenda kazi.  Vituo vingi vya afya vinategemea kupokea watumishi kutoka nje kwaajili ya maombi kwa wagonjwa…

Wakati mwingine jambo hili linakuwa ni gumu sana, kutokana ni vizuizi vya kiserikali na uchache wa watenda kazi…na hivyo wagonjwa wengi wanakufa katika dhambi na wengine kuonewa vikali na ibilisi na mapepo yake yachocheayo magonjwa.

Lakini tukisimama kuomba kwamba Bwana anyanyue watenda kazi basi, Bwana atasikia kwasababu ndiye aloyetuambia tuombe.

Na matokeo ya kuomba ni madaktari wengi kuokoka na manesi na wahudumu wa vituo hivyo vya afya na hivyo wagonjwa wengi wataombewa na kufunguliwa na kumpokea BWANA YESU, pasipo kusubiri watumishi kutoka nje.

4. SERIKALINI.

Hii ni sehemu ya nne inayohitaji watenda kazi wengi…kwani huko serikalini ikiwemo katika mabunge, wizara na mahakama, adui anadhulumu wengi na kuwapoteza wengi, na hiyo ni kutokana na upungufu wa watenda kazi.

Lakini tukisimama kuomba, Bwana YESU atasikia na kunyanyua watenda kazi ndani ya serikali..Watanyanyuka watu mfano wa akina Danieli na Yusufu ambao watahubiri na kufundisha na kukemea kazi za ibilisi katika mahakama, bunge na katika asasi zote za serikali.

5. MITAANI.

Hili ni eneo la tano linalohitaji watenda kazi wengi…Kwani katika mitaa ndiko watu wanakofanyia kazi, wanakokusanyika katika vigenge vya mizaha, au wanakofanyia mabaya.

Hivyo kunahitajika injili sana, ili watu waokolewe… na wakati mwingine inakuwa ni ngumu kufika kila mtaa kuhibiri, au watumishi wa Mungu kuzunguka kila mahali kuhubiri na kuombea watu.

Lakini kama tukisimama kumwomba BWANA anyanyue watenda huko basi kazi (katikati ya hao hao wahuni, au hao hao wanaofanya kazi haramu, au wanaoketi katika vijiwe vya mizaha) basi kazi ya injil itakuwa nyepesi sana na yenye matunda mengi.

Tutashangaa kuona wale waliokuwa walevi namba moja ndio wahubiri namba moja, wale waliokuwa makahaba namba moja ndio wainjilisti namba moja n.k

6. MITANDAONI

Hii ni sehemu ya sita na muhimu sana inayohitaji watenda kazi.

Kwani katika mitandao ndiko watu wanakojifunzia mambo yote maovu, ndani ya mitandao watu wanajifunza  mauaji, kiburi, uasherati, uchawi, utapeli, wizi na mambo yote mabaya ambayo biblia inayataja kama malango ya kuzimu.

Na wanaotumia mitandao hiyo kuhubiri habari njema ni wachache ukikinganisha na wale wanaoitumia kusambaza maovu.

Lakini tukisimama na kumwomba Bwana awageuze watu na kuwafanya watenda kazi shambani mwake, tutaona mageuzi makubwa.

Kwani wale waliokuwa wanahamasisha wizi, uasherati, utapeli na uhuni ndio watakaokuwa vipaumbele kuitumia mitandao hiyo hiyo kumhubiri YESU na kusaidia wengi,..

Wale waliokuwa watangazaji watageuzwa na kutangaza habari njema, wale waliokuwa waigizaji wa tamthilia za mapenzi ya kishetani sasa wanatengeneza mafundisha ya kuwajenga watu kiroho n.k

Lakini ikiwa tutaomba kwa bidii sana.

Hayo ni meneo sita yanayohitaji watenda kazi, yapo na maeneo mengine mengi lakini haya sita ndio yenye vipaumbele zaidi.

Hivyo kama mtu uliyeokoka usiishie tu kuombea familia yako, au kazi zako au ndugu zako au kanisa lako..

Piga hatua zaidi kuombea ongezeko la watenda kazi katika shamba la Mungu, kwani maombi hayo ni ya muhimu na yenye thawabu nyingi.

Mathayo 9:38 “Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake”.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

 MAVUNO NI MENGI

MWISHO WA MAVUNO, NI MWISHO WA DUNIA.

Kuomba katika roho ni kupi? na je nifanye nini ili niweze kuomba hivyo?

Fahamu Namna ya Kuomba.

VIACHENI VYOTE VIKUE HATA WAKATI WA MAVUNO.

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/09/05/mwombeni-bwana-wa-mavuno-apeleke-watenda-kazi/