NYOSHA MKONO WAKO, UUGUSE MFUPA WAKE NA NYAMA YAKE.

by Admin | 10 September 2024 08:46 am09

Shetani huwa ana kauli zake, za uongo ambazo hupenda kuwaaminisha watu, kuwa kuna mambo mwanadamu hawezi kuyafanya akiwa hapa duniani hata iweje.

Tukisoma habari ya Ayubu wakati ule shetani alipokwenda kumshitaka kwa Mungu.

Mungu alipomuuliza kuhusu mwenendo wake, majibu ya shetani yalikuwa ni kwamba Mungu amemzungushia wigo, kutunza alivyonavyo, Na kama atapotezewa alivyonavyo, basi atamkufuru Mungu waziwazi. Hivyo Mungu akaruhusu shetani amjaribu Ayubu, amchukulie alivyo navyo vyote, lakini uongo wa kwanza, ukashindwa, alipoona Ayubu anamtukuza Bwana katika misiba yake. Hiyo ni kuonyesha kuwa mwanadamu yoyote anaweza  kuishi bila msukumo wa mali,wala mtu wala kitu chochote katika hii dunia.

Lakini baadaye tena, akaendelea mbele kuzungumza uongo mwingine, alipoona Ayubu bado yupo na Mungu, akamwambia Mungu, yote yanawezekana kwa mwanadamu kuvumilia, lakini hili la kuugusa mfupa wake,kumtesa, kamwe hawezi kuvumilia atakukufuru tu. Mimi ninawajua wanadamu uwezo huo hawana, nilishawafundisha pia huko duniani.

Ayubu 2:4 Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake.

5 Lakini sasa nyosha mkono wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye atakukufuru mbele za uso wako.

6 Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake.  7 Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu wayo wa mguu hata utosi wa kichwa.

8 Naye akashika kigae cha kujikunia; akaketi majivuni.  9 Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu, ukafe.

10 Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.

Hilo nalo likashindikana. Kumbe mtu, hata kuupoteza uhai wake kwa ajili ya Kristo, linawezekana.

Ni nini Bwana anatufundisha kwa mawazo ya adui kwetu sisi ?

Leo hii ni rahisi sana kusikia, kauli kama, hakuna mtakatifu duniani! Ni rahisi kuona mtu anaanguka ovyo katika dhambi, na kutumia kisingizio kuwa yeye sio malaika. Utasikia kauli kama haiwezekani mtu kuacha vyote alivyonacho kwa ajili ya Kristo. Ndugu tambua kuwa hizo ni kauli za ibilisi ndani ya moyo wako. Adui anapenda kumshusha thamani mtu, kumweka kama kiumbe ambaye hawezi kujisimamia, hafundishiki, haaminiki.

Ni kweli mwanadamu kuwa na ukamilifu wa Mungu haiwezekani (Ndio sababu Yesu akaja kutukomboa), lakini kuna viwango Fulani Mungu anajua tunaweza kuvifikia, akalithibitisha hilo kwa Ayubu. Kama Ayubu ameweza kwanini wewe ushindwe, usijishushe thamani.

Neema haijaja kutuambia kuwa sisi hatuwezi, bali  imekuja kutuwezesha zaidi kuwa wakamilifu mbele za Mungu, yaani pale Ayubu aliposhindwa sisi tunasaidiwa kwa hiyo, na kutufanya tupokelewe kikamilifu mbele za Mungu, hiyo ndio kazi ya Neema (Soma Tito 2:11-12).

Kamwe usiruhusu hayo maneno ya kushushwa thamani na ibilisi, kwamba wewe huwezi mpendeza Mungu, huwezi kuacha vyote kwa ajili yake. Yesu  alisema tutakuwa wakamilifu kama Baba yetu alivyomkamilifu. Tunachopaswa kufanya ni kuamini kuwa hilo linawezekana na kuonyesha bidii katika hilo kumpendeza yeye. Na neema ya Mungu itatusaidia kufikia kilele Hicho cha juu kabisa.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

ILI TUONEKANE WAKAMILIFU MBELE ZA MUNGU.

Kwanini Labani aseme Yakobo ni Mfupa wake na nyama yake?(Mwanzo 29:14)

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/09/10/nyosha-mkono-wako-uuguse-mfupa-wake-na-nyama-yake/