by Admin | 16 September 2024 08:46 pm09
SWALI: Katika Yakobo 1:5 inasema tuombapo Mungu hakemei, maana yake ni nini.
JIBU:
Yakobo 1:5
[5]Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.
Kabla ya kuona maana hilo neno “wala hakemei naye atapewa”. Tuone kwanza tafsiri ya kifungu chote.
Hapa mtume Yakobo kwa uongozo wa Roho, anandika juu ya suluhisho la kupungukiwa kwa jambo muhimu sana ndani ya mwanadamu. Nalo ni Hekima.
Haandiki ikiwa mtu amepungukiwa na mali, au na umaarifu au na fursa, au watoto…hapana bali na hekima, na aombe dua.
Lakini hekima aisemayo sio hekima ya duniani, bali hekima ya ki- Mungu. Ambayo ni ufahamu wa Ki-Mungu unaoingia moyoni mwa mtu kumsaidia aweze kupambanua vema mambo yote, katika ufasaha wote ili kuleta matokeo aliyoyatarajia.
Hivyo sisi wote tunaihitaji hekima katika yote tuyatendayo. Vinginevyo hatutaweza kuzalisha chochote.
Lakini bado anatoa kanuni ya kuipata, hasemi tukae chini tuwaze, au tukahubiri, au tukatoe sadaka, au tuende kwenye shule za biblia. Hapana anasema na tuombe dua kwa Mungu.
Tunaipata kwa kuomba. Kwa kuchukua muda kupiga magoti na kuomba. Sio kuomba dakika mbili, na kusema Amen au yale maombi ya kumalizia siku unapokwenda kulala. Hapana bali ni maombi yaliyochanganyikana na kiu ya dhati kupata hekima ya Ki-Mungu katika eneo fulani, unalotaka Bwana akusaidie.
Vilevile hatupaswi kuomba bila dira. Kwamfano kusema.. “Mungu naomba unipe hekima”.. Hapana tunaomba tukielekeza eneo ambalo tunataka Bwana atusaidie kupata hiyo hekima ya kupambanua.
Kwamfano hekima katika kuyaelewa maandiko, hekima katika kuhubiri, hekima katika kufundisha, katika kuombea wagonjwa, katika kufanya biashara, katika kuimba. n.k.
Na hapo ndipo Mungu mwenyewe anaongeza ufahamu wake juu ya hicho unachokiomba na hatimaye utaona tu, mabadiliko, au njia ya kitu hicho unachotaka akusaidie.
Sasa tukirudi kwenye swali, pale anaposema
“awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa”
Maana yake, kwasababu Mungu ana ukarimu, basi hachagui wa kumpa, anawapa wote. Hii ahadi yake kuwa kila aombaye humpa. Haleluya.
Na tena anasema “hakemei”. Tofauti na sisi wanadamu
Kwamfano sisi tuwafuatapo wazazi wetu na kuwaomba kitu, wakati mwingine, hutugombeza, au huwa wakali, au kutaka utoe kwanza hesabu ya kile cha nyuma ulikitumiaje, kabla ya kukupa hichi kingine. Na ndio maana ulikuwa na hofu, kujifikiria mara mbili mbili hicho unachotaka kwenda kuomba, ukiulizwa hivi, ujibu vipi. Sio tu kwa wazazi, lakini kwa wanadamu wote, sifa hiyo wanayo tuwafuatapo kuwaomba kitu, si kivyepesi vyepesi kama tunavyodhani.
Lakini kwa Mungu wetu sio, hakemei, haangaali ya nyuma kukushutumu, hakuuliza makosa yako. Anakupa tu, bila sharti lolote.
Ni furaha iliyoje. Mimi na wewe tuliomwamini tunapokwenda kumwomba Mungu hekima, hatushutumiwi kwa lolote, au kwa madhaifu yetu. Bali kinachohitajika tu ni kumwamini yeye asilimia mia, bila kutia shaka katika hilo unaloomba, kwasababu ukitia shaka, maombi hayo hayaendi kwake bali kwa mungu mwingine asiyeweza yote.
ndio maana anataka tumfuatapo tusiwe na shaka ya kutojibiwa, ili maombi yetu yafike kwake kwelikweli, yeye aliyemweza wa yote.
Anasema hivyo katika vifungu vya mbeleni.
Yakobo 1:6-8
[6]Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku.
[7]Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.
[8]Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Je Elisha alimdanganya Ben-hadadi kuwa hatakufa kwa ugonjwa wake?
Rudi Nyumbani
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/09/16/yakobo-15-awapaye-wote-kwa-ukarimu-wala-hakemei-naye-atapewa/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.