NIONYESHE MARAFIKI ZAKO, NIKUAMBIE TABIA ZAKO.

by Admin | 29 September 2024 08:46 pm09

Mithali 13:20 Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.

Tulipokuwa watoto wazazi wetu walitufundisha kubagua baadhi ya marafiki tuliokuwa nao, na cha ajabu vigezo walivyotumia  havikuwa hata rangi zao, au kimo chao, au afya zao, bali tabia zao na akili zao. Wale watoto waliokuwa na nidhani, na akili shuleni wazazi wetu walitushurutisha sana kukaa nao karibu, kwasababu waligundua kuwa na sisi tutaambukizwa tabia zao, lakini wale waliokuwa watukutu, hata tulipokutwa tunacheza nao tu, tuliadhibiwa, sisi tuliona kama ni uonevu usio kuwa na tija, lakini baadaye tulipokuwa watu wazima, na kuona hatma ya wale watoto, ndio tulijua ni nini wazazi wetu walikuwa wanakiona.

Vivyo hivyo katika maisha ya rohoni, tunaambiwa.

Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.

Mbele za Mungu wenye hekima ni watu gani?

Ni watu waliookoka, wenye hofu ya Mungu ndani yao.

Mtu yeyote aliyemwamini Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yake, huku akiendelea katika kumcha Mungu kwelikweli, huyo ni wa kukaa karibu naye sana. Kwasababu na wewe utajifunza njia za wokovu, utaambukizwa kuomba, utaambukizwa mifungo, utaambukizwa upendo wa ki-Mungu, lakini pia na maarifa ya Neno la Mungu, pamoja na uinjilisti.

Watu hawafahamu kuwa hata hekima ya mwokozi wetu Yesu haikuja tu kwa kutegemea hekima kutoka juu kwa baba yake, hapana, ilichangiwa pia  na watu aliowachagua kukaa nao karibu, tangu alipokuwa mdogo, tunalithibitisha hilo pindi alipokuwa amekwenda Yerusalemu na wazazi wake kwa ajili ya kuila sikukuu, kama kijana angeweza kukaa na wenzake, kujifunza uchezaji wa kamari, au kutembea mitaani kutafuta wasichana, au kwenda kwenye dansi na sinema, na kujiunga na makundi ya wavuta bangi. Lakini, haikuwa hivyo kwake, yeye alichagua watu ambao wangekuwa ni wa muhimu kwake, ndio wale viongozi wa imani na waalimu waliotwa marabi, akawa akiwasikiliza hao na kuwauliza maswali, na ghafla akaambukizwa tabia zao, mpaka akawa yeye ndio RABI wao mkuu.

Luka 2:40  Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake. 41  Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka.

42  Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu;

43  na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari.

44  Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao;

45  na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. 46  Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, AMEKETI KATIKATI YA WAALIMU, AKIWASIKILIZA NA KUWAULIZA MASWALI.

47  Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. 48  Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni.

49  Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? 50  Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia

Mambo mengine hutaweza kuyaacha, au tabia nyingine hutaweza kuziondoa ndani yako. Kama hutaweka machaguzi ya watu sahihi wa kuongozana nao. Utakuta ni mkristo analalamika ni mzito wa kuomba, au kushuhudia, au kufunga. Ukiangalia kampani ya watu wake muda wote, ni wafanyakazi wenzake wa ofisini, ni marafiki zake wa chuo, ni majirani zake hapo mtaani. Lakini wapendwa, au watumishi wa Mungu waaminifu, ni jumapili tu kukutana nao kanisani, hata anapotafutwa, kukumbushwa wajibu wake kiroho, anawakwepa. Na wakati huo huo anatumainia awe moto kiroho. Hapo ni kujidanganya.

Tunahitaji  kupashana moto, kamwe huwezi simama kipeke yako, haijalishi wewe ni nani, au unamjua Mungu kwa ukubwa kiasi gani. Tembea na waombaji  ili  uwe mwombaji, tembea na washuhudiaji ili uweze  kushuhudia, kaa na waalimu ili uwe mwalimu. Nje ya hapo utageuzwa na ulimwengu,.

 Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Usimwache rafiki yako mwenyewe, wala rafiki ya baba yako.

NGUVU YA HEKIMA NA AKILI

IVUMBUE INJILI YA KRISTO KUTOKA KATIKA KILA JAMBO.

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/09/29/nionyeshe-marafiki-zao-nikuambie-tabia-zako/