KUWA MAKINI NA MATANGO MWITU, SIKU HIZI NI ZA MWISHO!

by Admin | 4 October 2024 08:46 am10

Kuna wakati Elisha alifika Gilgali na mahali pale palikuwa na njaa kali, na watu wengi (manabii) pia walikuwa  wamekusanyika kusikiliza mashauri ya mtu wa Mungu.

Hivyo akawaambia waweke sufuria motoni waandae chakula.

Lakini mmojawao akatoka akaenda mashambani kutafuta mboga. Na huko akafanikiwa kweli kukusanya zilizo bora, lakini kwasababu hakuwa na maarifa ya kutosha jinsi ya kutambua mboga sahihi ziwafaazo wanadamu akaona huko matango mwitu, na bila kujua, akidhani ni matango halisi, akayachuma na kuyaleta sufuriani. Matango yale yalikuwa ni sumu.

Lakini walipoonja kwa neema za Mungu walijua kuna kitu ambacho sio sahihi kimewekwa sufuriani, hivyo waacha wote kula. Ndipo Elisha akataarifiwa, juu ya jambo hilo, kama kimwagwe lakini kile chakula hakikumwagwa, bali aliwaagiza watie unga mule (kwa Neno la Bwana), na chakula kitaponyeka.  Wakafanya hivyo, kikawa sawa, wakala wakashiba.

2 Wafalme 4:38-41

[38]Elisha akafika Gilgali tena; na kulikuwa na njaa katika nchi; na hao wana wa manabii walikuwa wakikaa mbele yake. Akamwambia mtumishi wake, Teleka sufuria kubwa, uwapikie wana wa manabii.

[39]Na mmoja wao akaenda nje kondeni ili kuchuma mboga, akaona mtango-mwitu, akayachuma matango-mwitu, hata nguo yake ikawa imejaa, akaja akayapasua-pasua sufuriani; kwa maana hawakuyajua.

[40]Basi wakawapakulia hao watu ili wale. Ikawa, walipokuwa katika kula chakula, wakapiga kelele, wakasema, Mauti imo sufuriani, Ee mtu wa Mungu. Wala hawakuweza kula.

[41]Lakini yeye akasema, Leteni unga. Naye akautupa ndani ya sufuria; akasema, Wapakulie watu, ili wale. Wala hakikuwamo kitu kibaya sufuriani.

Habari hiyo inafunua nini?

Inatueleza hali ya kiroho ya watu iliyopo sasa.

Palipo na njaa ni rahisi mtu kula kila kitu, ilimradi tu asife. si rahisi akae chini na kufikiria ubora wa kile anachokula. Leo hii njaa ya Neno la kweli la Mungu ni kubwa, hivyo kila mtu anaenda kondeni kuokota kitu kimfaacho, huko huko tunakutana na vizuri lakini pia tunakutana na vibaya..

shida ipo hapo, je tunaweza kupambanua?

Kwasababu ukila sumu, ile sumu haitakuambia ngoja nisikuletee madhara kwasababu hukukusudia kunila, au hukujua kuwa mimi ni sumu, utakufa tu  sawasawa na yule anayejua anachokifanya.Kumbe ujinga una gharama kubwa.

Bwana Yesu alisema..

Mathayo 7:15

[15]Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.

Mafundisho yasiyomhubiri Kristo na utakatifu, ni kuwa makini nayo, ni heri usiyasikilize kabisa kwa usalama wako wa kiroho. Yanayokuambia tunaokolewa kwa neema tu, hivyo matendo yako ni kazi bure mbele za Mungu, ukiokolewa umeokolewa milele, hata ukiwa unatenda dhambi vipi huwezi potea, yapime sana hayo mafundisho.

Mafundisho ya kuzimu-kuzimu tu na majini na wachawi epukana nayo, Mafundisho ya sanamu ibadani, ni mauti chunguni. Mafundisho yanayopinga habari za mwisho wa dunia, ambayo hayana habari na unyakuo au kumfanya mtu atazame kurudi kwa pili kwa Kristo, kinyume chake ni kukuweka kidunia, ufikirie mafanikio ya mwilini ni matango mwitu.

Manabii wa uongo ni wengi, wapo wanaotenda kazi kwa uwazi, lakini  wapo wanaotenda kazi kwa siri.

Jifunze kusoma biblia, jinsi usomavyo Neno la Mungu utagundua kuwa mtu uliyeokoka  kwa wakati uwapo hapa duniani Bwana anakutana Utembee katika utakatifu (Waebrania 12:14). Lakini pia uelekeze macho yako mbinguni kwa yale mambo yajayo, ya mbingu mpya na nchi mpya.

Luka 12:35-36

[35] Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; [36]nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara.

Jihadhari na matango mwitu.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii  >>>> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

UNAWAFAHAMU MANABII WA UONGO?

Kusanyiko la makini/ mkutano wa makini ni upi?

USIPOTEZWE NA MANENO YA MANABII WA UONGO.

 

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/10/04/kuwa-makini-na-matango-mwitu-siku-hizi-ni-za-mwisho/