KWA KUWA FURAHA YA BWANA NI NGUVU ZENU. 

by Admin | 6 October 2024 08:46 pm10

Nehemia 8:10

[10]Kisha akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa BWANA wetu; wala msihuzunike; KWA KUWA FURAHA YA BWANA NI NGUVU ZENU.

Ni habari ya kutafakarisha, lakini zaidi sana ya kuwafariji watu wote wampendao Mungu. Tukisoma katika biblia ile habari ya Ezra na Nehemia, katika juhudi zao wa kuwarejesha Israeli katika ibada na njia za Mungu Yerusalemu.

Tunaona wakati ule ukuta wa Yerusalemu ulipomalizwa kujengwa baada ya kurudi kwao utumwani Babeli, Ezra hakuwaacha tu hivi hivi, wafurahie kukamilika kwa majengo, bali alitaka wakamilishwe na mioyo yao hivyo, alikichukua kitabu cha Torati na kuanza kuwasomea wayahudi wote tangu asubuhi mpaka adhuhiri, ili wajue ni nini Bwana anataka kwao (Nehemia 8).

Na waliposikia waliona makosa yao mengi sana, na hukumu nyingi za Mungu, alizowatamkia kufuatana na makosa yao, yaliyowapelekea mpaka wakachukuliwa mateka. Ikumbukwe kuwa kitabu hicho cha torati hakikuwahi kusomwa tangu zamani walipochukuliwa utumwani, ndio ilikuwa mara yao ya kwanza kukisoma baada ya miaka mingi kupita.

Hivyo wayahudi kusikia vile wakaanza kulia sana na kujuta na kuomboleza. Lakini tunaona kuna jambo lilifanyika la kitofauti.

Nehemia, alitambua wazo la Mungu…Hivyo akawazuia watu kulia na kuomboleza kwa ajili ya makosa yao. Kinyume chake akawaambia leo ni siku takatifu kwa Bwana, hivyo mle ,.mnywe, mtoe sadaka, mfurahi mbele za Mungu wenu kwasababu “furaha ya BWANA ni nguvu zenu” 

Hivyo watu wakasheherekea, badala ya kulia, Sio kwamba Nehemia alisheherekea makosa yao, hapana, bali alipewa kujua kwamba  furaha ya mtu kwa Mungu wake, ndio chanzo cha nguvu ya kumtumikia yeye. 

Ndio hapo baada ya wayahudi kujua makosa yaowakimfurahia Mungu, siku hiyo, na wakapokea nguvu nyingi za kuishika sheria ya Mungu. 

Yaani kwa namna nyingine, Mungu kuwakemea makosa yao,lengo lake lilikuwa sio awahukumu, au wainamishe vichwa vyao wakidhani kuwa wao ni kichefu-chefu kwake. Hapana..Bali anawapenda na hivyo anatarajia wajue nia ya makemeo yake.

Nehemia 8:10 Kisha akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu.

11 Hivyo Walawi wakawatuliza watu wote, wakasema, Nyamazeni, kwa maana siku hii ni takatifu; wala msihuzunike. 

12 Na watu wote wakaenda zao kula na kunywa, na kuwapelekea watu sehemu, na kufanya furaha nyingi, kwa sababu walikuwa wameyafahamu maneno yale waliyohubiriwa

 

Ni hata sasa, unaposoma biblia na kuona inakushitaki, inakuambia usiibe, usisengenye, amchukiaye ndugu yake ni sawa na muuaji, wazinzi wote sehemu yao ni katika lile ziwa la moto, inapokukemea maovu yako ya siri.. Usiinamishe kichwa na kusema “mimi sifahi mbele za Mungu, mimi ni mkosefu sistahili kuitwa mwana wake”..Ukaacha kukisoma kabisa, ukawa unalia tu, umenyong’onyea, na kujihisi wewe ni wajehanamu tu, Mungu hakupendi, ameshakuacha, ona sasa unamkosea kosea kila siku… Fahamu kuwa hilo sio kusudi la Mungu.

Kusudi la Mungu sio usome biblia, ujawe na hisia za Mungu kukuhukumu, au kukulaumu, au kukushitaki, bali kusudi la Mungu ni ujue  upendo wake uliozidi sana kwako, kiasi cha yeye kuonyesha hisia zake kwako namna ambavyo unapaswa uwe kama yeye.

Hivyo ukitoka kuonywa na kukemewa, unapaswa utoke kwa kufurahi moyoni  na kuruka-ruka, na hapo ndipo utapokea nguvu ya kuishinda hiyo dhambi. Lakini ukitoka kinyonge na mashaka utashindwa kwasababu furaha ya Bwana ndio chanzo cha nguvu zetu. Ukilipenda hilo katazo, utalitenda, usipolipenda kamwe huwezi litenda.

Mtunga Zaburi alisema,

Zaburi 119:52

[52]Nimezikumbuka hukumu zako za kale, Ee BWANA, nikajifariji.

Bwana anataka tuone upendo wake kwetu katika makemeo yake, tufarijike tupokee nguvu ya kushinda. Pengine umetoka kufanya dhambi fulani ya makusudi na Roho Mtakatifu akakumbusha kuwa watu wa namna hii, huangukia katika mtego mbaya wa shetani bila kunasuka, Sasa hapo usianze kupoteza ladha na Mungu wako, au biblia, ukauchukia wokovu, kabisa,  maanisha kutubu, jifunze kutokana na makosa, kisha furahia mwambie Bwana asante kwa kunipenda,

hata wachezaji wa mpira, wafungwao kipindi cha kwanza, wanapotulia na kujihamasisha tena, hupokea nguvu ya kucheza vema kipindi cha pili, lakini wajilaumupo, hufanya vibaya zaidi

Na sisi pia tuiamshe furaha ya Bwana daima.Kila tusomapo Neno lake, tufurahi kwasababu ni barua ya upendo wa Mungu kwetu Ili tuweze kuwa na nguvu.

Kwasababu furaha ya Bwana ndio nguvu yetu.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

SHUKURU KWA KILA JAMBO.

Furaha ni nini?

Fahamu maana 1Wakorintho 14:20  “Ndugu zangu msiwe watoto katika akili zenu;

 

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/10/06/kwa-kuwa-furaha-ya-bwana-ni-nguvu-zenu/