IFUATE KANUNI SAHIHI YA MUNGU

by Admin | 11 October 2024 08:46 am10

Zipo kanuni za ki-Mungu tunaweza kuzifuata na zikaleta matokeo kabisa halisi, lakini zisiwe na manufaa kwetu katika suala la wokovu.  Sasa kabla ya kuangalia ni kwa namna gani? 

chukulia mfano wa kawaida.

Mwanamke yeyote anaweza kubeba ujauzito katika mazingira mbalimbali, kwamfano anaweza akatwezwa nguvu (akabakwa), na akapata ujauzito, lakini pia anaweza kwenda kujiuza kama kahaba na bado akapata ujauzito, vilevile anaweza akasubiri aolewe kwanza katika ndoa halali ndipo apokee ujauzito na likafanikiwa vilevile tu, kuleta kiumbe duniani, kama angefanya hayo kabla ya ndoa, au atokapo nje ya ndoa yake.

Sasa unaweza jiuliza, katika njia zote hizo ambazo angepata ujauzito ni ipi iliyo halali inayokubalika mbele za Mungu na wanadamu. Bila shaka ni hiyo njia ya mwisho ambayo ni ya kuolewa kwanza, ndipo apokee ujauzito kutoka kwa mume wake mmoja wa halali. Na ndio mtoto huyo hujulikana kama halali sio haramu.

Lakini cha ajabu ni kuwa ijapokuwa njia halali ipo lakini feki pia huleta matokeo yaleyale mfano wa halali. Kwasababu gani? Kwasababu kanuni ya kupata mtoto, si kanuni ya uhalali. Hivyo ni vitu viwili tofauti, 

Hata Ibrahimu, alikuwa na watoto wengi, alitangulia Ishmaeli, kisha baadaye wakazaliwa na watoto wengine sita kwa suria mwingine, mbali na Isaka. Wote walikuwa wanadamu, viumbe wa Mungu, wenye akili na nguvu na baraka, wasio na hatia. Lakini lilipokuja suala la urithi, ndipo kubaguliwa  kulipokuja, Watoto wote wa masuria walifukuzwa wakapewa zawadi tu bali Isaka alipewa vyote.

Mwanzo 25:5-6

[5]Ibrahimu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo. 

[6]Lakini wana wa masuria aliokuwa nao Ibrahimu, Ibrahimu akawapa zawadi, naye akawaondoa katika mahali alipokaa Isaka mwanawe, wakati wa uhai wake, waende pande za mashariki, mpaka nchi ya Kedemu. 

Hii ni kutufundisha nini hasaa katika maisha yetu ya wokovu.

Zipo kanuni nyingi sana za kiroho ambazo mtu yeyote, hata ambaye  hajamwamini Yesu anaweza zitumia na zikatoa matokeo yaleyale sawa tu na mtu ambaye ameokoka.

Kwamfano, kufanya miujuza na ishara kwa jina la Yesu. Watu hawajui kuwa jambo hili huhitaji imani tu, katika jina lake. Hivyo wale wafikiao kiwango hicho haijalishi ni mwizi, ni mpagani, anaweza pokea muujiza na akafanya pia muujiza sawa tu na yule aliyeokoka.

Kwasababu gani? kwasababu amefanikiwa kufuata kanuni ambayo ni Imani.

Akijua lile neno linalosema  ‘yote yawezekana kwake yeye aaminiye’’ (Marko 9:23). Ndio maana walikuwepo watu wengi wasiokuwa wayahudi kipindi kile cha Yesu walipokea miujiza mikubwa, zaidi ya wayahudi kwasababu tu ya ukubwa wa imani zao. Na sio haki zao.

Vivyo hivyo hata katika kuomba. Mtu yeyote aombaye hupokea. Ni kanuni ya asili ya rohoni, haijalishi ni nani.

Mathayo 7:8

[8]kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. 

Watu hawajui hata kufanikiwa kwa shetani hutegemea maombi, na yeye pia huenda mbele za Mungu kuomba na hupewa..hajiamulii tu mambo yake ovyo ovyo bila idhini ya Mungu, kwasababu hii dunia si yake… utauliza kwa namna gani, ? unamkumbuka shetani kipindi cha Ayubu, yeye naye alikwenda kujihudhurisha mbele za Mungu, ndipo akaleta uharibifu. Akapeka haja zake akasikiwa, dua zake na magoti yake.

Ayubu 1:6

[6]Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao. 

Watu wengi wanapoona wanamwomba Mungu wanajibiwa wanadhani, ndio wamekubaliwa na Mungu. Kumbe unaweza kuomba kama mwana-haramu usiyekuwa na urithi wa uzima wa milele, bali haki ya kupokea tu unachokiomba.

Unaweza ukafanya miujiza kama mwana-haramu. Lakini usiende mbinguni.

Mathayo 7:22-23

[22]Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? 

[23]Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu. 

 Unaweza ukamwamini Yesu, na kumuhofu,  lakini ukaamini kama mashetani.

Yakobo 2:19

[19]Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka. 

unaweza ukawavuta watu kwa Kristo na wakaokoka, lakini ukawa mtu wa kukataliwa kama tu Paulo alivyosema katika; 

1 Wakorintho 9:27

[27]bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa. 

Sasa kanuni sahihi ya Mungu ni ipi ili tuonekane kamili na halali?

Kanuni Mungu anayoitazama kwetu ni Wokovu uliokamilishwa kwa matendo yake.

Angalia mwishoni pale kwenye Mathayo 7:23 Bwana Yesu alichokisema;

“ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”

Umeona je unaishi maisha gani?. hicho ndio kipimo cha ki-Mungu, 

Alisema pia.

Yakobo 2:24

[24]Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake. 

Hakikisha maisha yako yanaendana na ukiri wako, wa imani yako, usiishi tu kama mtu ambaye hajaamini ukijitumainisha, kuona maombi yako yanajibiwa, karama yako inafanya kazi, imani yako inatenda kazi..hizo ni kanuni za kupokea lakini sio kanuni za uhalali wa kuurithi uzima wa milele. Ishi kama mtu ampendezaye Bwana wake kimwenendo, ndipo hayo mengine yakifuata huna hasara.

Nyakati hizi za mwisho, adui anaweka uzito kwenye mioyo ya watu wasipende kutafuta maisha matakatifu, kinyume chake wabakie tu kwenye miujiza, uponyaji, utabiri…Siku ile hivyo vitu havitafuata na wewe ndugu, bali matendo yako.

Ufunuo wa Yohana 14:13

[13]Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao. 

Tuanze sasa kujipima mienendo yetu. Kisha tutumie nguvu nyingi hapo kujirekebisha, sawasawa na imani tuliyoipokea, ili tuwe wana halali waliozaliwa kweli ndani ya Kristo, watakaorithi uzima wa milele.

Wokovu wa kweli hufunuliwa kwa mwenendo mzuri. Tuitazame sana kanuni hii.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

KANUNI JUU YA KANUNI.

KANUNI YA KUOMBA NA KUPOKEA.

JE NI HALALI KUOA WAKE WENGI AU KUTOA TALAKA?

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/10/11/ifuate-kanuni-sahihi-ya-mungu/