KANUNI YA KUOMBA NA KUPOKEA.

KANUNI YA KUOMBA NA KUPOKEA.

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia Neno la Mungu wetu lililo taa ya miguu yetu na Mwanga wa njia yetu (Zab.119:105).

Ni muhimu kujua kanuni kadhaa za kuomba ili maombi yetu yawe na majibu.

Tumewahi kujifunza kanuni kadhaa huko nyuma na leo imempendeza Bwana tujifunze kanuni nyingine.

Neno la Mungu linasema yafuatayo katika kitabu cha Yakobo 4:2-3.

Yakobo 4:2 “ Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!

3  Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu”.

Kumbe sababu ya kutopata yale tunayoyaomba ni jinsi tunavyoomba!.. (kwamba tunaomba vibaya!).

Na kuomba vibaya kunakozungumziwa hapo si kukosea kupangilia maneno wakati wa kuomba, bali ni kuomba kusikompendeza Bwana, ambako ni nje na mapenzi ya Mungu, mfano wa maombi hayo ni yale mtu anaomba Bwana ampatie fedha ili awe nazo awakomeshe wanaomdharau. (Maombi ya namna hii ni maombi mabaya, na mara nyingi hayana majibu)

Hivyo unapoomba zingatia mambo yafuatayo.

1.Kuwa na Nia Njema:

Nia njema, maana yake ni kusudi jema… Kama unahitaji Bwana akupe mafanikio Fulani ya kiroho au ya kimwili, hakikisha Nia yako ni njema, kwamba utokane tu na ugumu unaoupitia, na pia upate kitu cha kuwasaidia wengine, na si kwa lengo la kuwakomesha wanaokudharau. Ukiwa na Nia ya kupata vitu ili wengine waone, maombi hayo yanaweza yasijibiwe kabisa.

2. Mwombe Mungu mahitaji na si Fedha.

Wengi wetu tunapenda kupeleka maombi ya kupata fedha kutoka kwa Mungu.. Lakini kiuhalisia hayo si maombi bora. Tunasahau kuwa tunachokihitaji sana ni mahitaji yetu kama chakula, mavazi, makazi, afya na mengineyo, ambayo hayo Mungu anaweza kukutimizia pasipo fedha.

Ukiwa na haja ya chakula, mwambie Bwana naomba chakula na yeye anajua namna ya kukupatia hicho chakula kama kwa njia ya kukupatia fedha ukanunue, au kwa kukuletea mtu atakayekupa hicho chakula, (usikimbilie moja kwa moja kumwambia Bwana akupe fedha ya chakula), kwani yeye anazo njia nyingi za kukulisha wewe, si lazima kwa kutumia fedha.

Vile vile ukitaka mavazi, makazi, biashara, afya n.k  Mwambie Bwana akupe vitu hivyo, na wala usiombe fedha za kupata mavazi, au za kupata makazi, au za kufanya biashara.. wewe mwambie naomba mavazi, yeye anajua jinsi ya kukupatia kama kupitia mlango huo wa fedha au kupitia watu yeye anajua, vile vile usiombe mtaji kwa Mungu, badala yake iombe ile kazi kwasababu wakati wewe unawaza kupata mtaji kwanza kumbe pengine Mungu amekuandalia mahali utakapoanza kufanya kazi pasipo mtaji.

Ukihataji Bwana akupe kifaa cha kazi au chombo za kukurahisishia usafiri, usimwambie Bwana akupe Pesa za kununua chombo hicho, badala yake mwombe Bwana akupe hicho chombo, kwa njia anayoijua yeye.

Ukitaka kusafiri usimwombe Bwana fedha za kusafiri, wewe mwombe akusafirishe, yeye atajua njia atakayotumia kukufikisha kule unakotaka kwenda, kama amtanyanyua mtu na kukusafirisha kwa gharama zake au bure, au atafungua mlango wa wewe kupata fedha hizo, ila usijifunge kwa kanuni ya fedha.

Vile vile unapoumwa usimwombe Mungu pesa za matibabu, mwombe afya, yeye anajua njia atakayotumia kukupa hiyo afya, na mambo mengine yote, epuka Kutaja “Pesa” mbele za Mungu!!.. bali taja lile hitaji!.

Kwanini maombi mengi ya kuomba Pesa hayajibiwi?

Kwasababu kuna roho nyuma ya pesa, inayowasukuma watu katika tamaa mbaya za kidunia, na kuwatoa wengi kwenye Imani, ndivyo maandiko yanavyosema.

1Timotheo 6:10  “Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi”

Ndio maana utaona asilimia kubwa ya watu waliopata pesa wanakuwa na kiburi!. Lakini waliopewa na Bwana ni wanyenyekevu. Mtu aliyezawadiwa baiskeli na yule aliyenunua baiskeli kwa fedha, utaona yule aliyenunua anakuwa na kiburi Zaidi ya yule aliyepewa. Ingawa wote wana baiskeli!.

Yule aliyezawadiwa nyumba na yule aliyejenga kwa fedha yake, utaona yule aliyejenga anakuwa na kiburi Zaidi ya yule aliyezawadiwa. Na mapenzi ya Mungu ni sisi tuwe wanyenyekevu na si watu wenye viburi, hivyo kamwe hawezi kukupa kitu ambacho baadaye kitakuja kukupa kiburi.

Ni wachache sana ambao Mungu anawabariki kwa fedha, kwasababu anajua tayari ameshawatengeneza mioyo yao, hawawezi kuwa na kiburi hata wawe na kiasi gani cha fedha, na hiyo naweza kusema ni asilimia 1% lakini wengi Mungu hawapi hizo fedha wanazozihitaji kwasababu anajua tamaa tulizo nazo. Na ukiona mtu ana fedha nyingi na ana kiburi (hizo fedha hajapewa na Mungu!!).

Kama mkristo biblia inatufundisha tusiwe watu wa kupenda fedha, wala kuzisifia wala kuzitukuza, badala yake tumtukuze Mungu na tumfanye Mungu siku zote kuwa MPAJI WETU (YEHOVA YIRE)!!. Kwamba fedha ziwepo au zisiwepo bado tutaishi, bado tutavaa, bado tutakula, bado tutamiliki vitu.. Tuliookoka tuna uwezo wa kuishi bila fedha wala vitu vilivyotukuzwa na wanadamu na bado tukawa na maisha bora kuliko watu wenye mambo hayo.

Mhubiri 5:10 “Apendaye fedha hatashiba fedha, Wala apendaye wingi hatashiba maongeo. Hayo pia ni ubatili”.

Bwana atusaidie.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JE UMEJIANDAA KUTIMIZA UNABII UPI?

Ni kwa namna gani haki huinua taifa? (Mithali 14:34)

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

Ni lini na wapi Ibrahimu aliioona siku ya Bwana akashangilia?.

JE UNA MATUMAINI YA KUPATA TENA KILE ULICHOPOTEZA?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Elizabeth
Elizabeth
10 months ago

Ameen